Zidane SereriZidane Sereri

MZIZIMA Dabi, wababe wawili wamekamilisha dakika 180 ndani ya msimu wa 2024/25 Simba ikiibuka na ushujaa kwa kuvuna pointi nne huku Azam FC wakivuna pointi moja baada ya dakika 90 ndani ya msimu wa 2024/25 kwenye msako wa pointi sita katika ligi namba nne kwa ubora.

Licha ya kuvuna pointi nne bado benchi la ufundi la Simba limeweka wazi kuwa matokeo ya sare kwenye mchezo wa mzunguko wa pili hayajawafurahisha kutokana na nafasi ambazo walizipata kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Februari 24 2025 na ubao baada ya dakika 90 kusoma Simba 2-2 Azam FC.

Hamza v Azam
Hamza beki wa Simba akishangilia moja ya bao kwenye mchezo wa ligi, Uwanja wa Mkapa. Source: Simba.

Ikumbukwe kwamba mtupiaji wa bao la kwanza kwenye mchezo wa Mzizima Dabi ni Gibril Sillah ambaye aliwatungua Yanga ambao ni watani wa jadi wa Simba kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex .Yanga inayodhaminiwa na SportPesa kwenye mchezo huo ilipoteza pointi tatu mazima kwa kuwa baada ya dakika 90 Novemba 2 2024 ubao ulisoma Yanga 0-1 Azam FC.

Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wababe hawa wawili Simba na Azam walipokutana baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa New Amaan Complex, Septemba 26 baada ya dakika 90 ulisoma Azam FC 0-2 Simba na bao la kwanza kwa Simba lilifungwa na Leonel Ateba ambaye ndani ya ligi amefunga mabao 8 katika hayo manne ni kwa mapigo ya penati.

DAKIKA 90 ZA MAAJABU

Kwenye Mzizima Dabi ilikuwa ni dakika 90 za maajabu kwa kuwa Azam FC walifunga bao la kwanza ndani ya dakika 15 za mwanzo likiwa ni bao la mapema zaidi kwa Mousa Camara kutunguliwa akiwa langoni dakika ya kwanza na bao la pili kwa Azam FC lilifungwa dakika 15 za mwisho kuelekea dakika 90 za mchezo.

Mtupiaji Zidane Sereri ambaye aliingia kipindi cha pili alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ambao unakuwa ni mchezo wake wa kwanza kucheza dhidi ya Simba kwa msimu wa 2024/25 akiwa na uzi wa Azam FC kwa kuwa ni ingizo jipya ndani ya kikosi hicho kwenye dirisha dogo la usajili.

Kiungo Feisal Salum pasi yake ndefu akiwa nje ya 18 dakika ya 87 inaingia kwenye rekodi ya kuwa pasi ya ajabu iliyowanyanyua mashabiki wa Azam FC kwa furaha ya bao la Zidane katika dakika za lala salama kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.

HIZI HAPA NAFASI ZAO SASA

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha jumla ya pointi 51 kibindoni baada yakucheza mechi 20 kwenye msimamo na nifasi ya pili huku vinara wakiwa ni watani zao wa jadi Yanga wenye pointi 55 tofauti ya pointi nne huku Simba wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Dodoma Jiji ambao utapangiwa tarehe.

Toto Fei
Fei kiungo wa Azam FC kinara wa pasi za mwisho akiwa nazo 11 ndani ya msimu wa 2024/25. Source: Azam FC.

Azam FC ni nafasi ya tatu kwenye msimamo pointi zao ni 44 baada ya mechi 21, safu ya ushambuliaji ya Azam FC imetupia mabao 31 na kinara wa pasi za mwisho ni Feisal Salum ambaye ametoa jumla ya pasi 11 ndani ya ligi akitupia mabao manne akihusika kwenye jumla ya mabao 15 katika kikosi hicho huku safu ya ushambuliaji ya Simba ikiwa imetupia mabao 43

REKODI ZATIBULIWA KWA MKAPA

Kipa namba moja wa Simba, Mousa Camara rekodi yakutoka na hati safi mbele ya Azam FC Uwanja wa Mkapa ilitibuliwa mapema Camara dakika ya kwanza na nyota wa Azam FC, Gibrill Sillah na bao hilo liliwekwa usawa na Ellie Mpanzu dakika ya 25 na kuweka usawa mpaka dakika 45 za mwanzo kwenye mchezo wa Mzizima Dabi.

Camara Kwa Mkapa
Camara Kwa Mkapa

Kipindi cha pili ni beki Hamza Jr alipachika bao la pili kwa Simba likiwa ni bao lake la kwanza ndani ya msimu akitumia pasi ya Jean Ahoua ambaye alipiga faulo dakika ya 76 kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Simba wakiwa wanaamini mchezo umegota mwisho watasepa na pointi tatu wakapoteana baada ya bao la Zidane Sereri dakika ya 88 akitumia pasi ya maelekezo kutoka kwenye miguu ya Feisal Salum ikiwa ni pasi yake ya 11 ndani ya msimu  akiwa mkali namba moja kwa vinara wa pasi za mwisho ndani ya ligi namba nne kwa ubora.

Kwenye msimamo Simba ni namba mbili akiwa na pointi 51 baada ya mechi 20 huku Azam FC ikiwa nafasi ya tatu na pointi 44 baada ya mechi 21 vinara wakiwa ni Yanga wenye pointi 55 baada ya mechi 21.

Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa hawajafurahia matokeo hayo kwa kuwa walikuwa wanapambana kusaka pointi tatu makosa ambayo walifanya yamewaadhibu huku akipongeza kiwango cha wapinzani wao Azam FC.

“Hatujawa na furaha kutokana na matokeo ambayo tumeyapata tulicheza vizuri unaona tuliruhusu bao la mapema mwanzo wa mchezo na kipindi cha pili mwisho wa mchezo tukaruhusu bao kwenye mchezo wetu, hatujafurahia tunakwenda kufanyia kazi makosa.”

Share this: