UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa umelipa kisasi kikatili kwa timu zote za Dar ambazo zilipoteza pointi tatu ndani ya dakika 90 dhidi ya Tabora United kwenye mechi za Ligi Kuu Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika.
Ikumbukwe kwamba mabingwa watetezi wa ligi ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex.

Yanga imekuwa kwenye mwendo bora ndani ya KMC Complex kwenye mechi zake zote za ushindani ilizocheza hapo baada ya kuhamia wakitokea Azam Complex ni mechi tano wamecheza na kupata ushindi mechi nne za ligi na mechi moja ya CRDB Federation Cup.
FADLU NA BALAA LAKE

Simba imecheza mechi 16 ikipata ushindi kwenye mechi 14, ilitoshana nguvu mchezo mmoja ilikuwa Simba 2-2 Coastal Union mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex na ilipoteza mchezo mmoja ilikuwa Simba 0-1 Yanga bao la kujifunga na Kelvin Kijili mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ni namba moja kwenye msimamo ikiwa na pointi 43 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 42 zote zimecheza jumla ya mechi 16 ambazo ni dakika 1,440.
Fabruari 2 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulisoma Tabora United 0-3 Simba kwa mabao ya Leonel Ateba ambaye alifunga mabao mawili dakika ya 12 na 33 huku bao moja likifungwa na Shomari Kapombe dakika ya 65 akitumia pasi ya Ateba.
Ateba kwenye mchezo huo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kwa kuhusika kwenye mabao yote matatu yaliyofungwa na timu hiyo na langoni alianza Moussa Camara kwa Simba akifikisha hati safi 13 kati ya mechi 16 ambazo alianza langoni.
SEMAJI LA CAF HILI HAPA

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wamelipa kisasi kwa timu zote za Dar ambazo zilifungwa na Tabora United kwenye mechi za ligi ndani ya dakika 90.
“Tumelipa kisasi kikatili mbele ya Tabora United kwa kupata pointi tatu na ushindi huu ikiwa ni furaha kwetu huku wale waliofungwa na timu hii tukiwalipia kisasi hivyo kwa sasa Dar ipo salama.
“Ni mchezo uliokuwa mgumu unaona kwamba Tabora United ina timu imara na yenye ushindani lakini tumepata matokeo hivyo kwa wale waliofungwa watakuwa wamefurahi. Kwa kilichotokea kwa sasa Tabora United tunawapa ruksa kurudia kuwafunga tena wale waliowafunga kwa kuwa kazi yetu sisi tumekamilisha.”
Ndani ya msimu wa 2024/25 Simba imevuna pointi sita mbele ya Tabora United na kufunga mabao sita huku safu ya ushambuliaji ya Tabora United ikiwa haijaifunga Simba kwenye ligi. Mchezo wa mzunguko wa kwanza ilikuwa Uwanja wa KMC Complex ubao ulisoma Simba 3-0 Tabora United, mchezo wa ugenini Tabora United 0-3 Simba.
Timu ambazo Tabora United ilipata kuzifunga kwenye ligi ambazo zipo ndani ya tatu bora ni Azam FC ugenini baada ya dakika 90 ubao ulisoma Tabora United 2-1 Azam FC na Yanga 1-3 Tabora United mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
MKWARA WA TABORA UNITED

Ofisa Habari wa Tabora, United, Christina Mwagala amesema kuwa wanaamini kuwa ni mara ya mwisho Tabora United yenye Offen Chikola, Heritier Makambo, Yacouba Sogne amkufungwa na Simba kutokana na mwendo ambao wanao wapinzani wao.
“Wametufunga Simba duru ya kwanza na mchezo wa kwanza kwenye duru ya pili wamepata ushindi ila tunaona kwamba Simba wamepata ushindi na hawatatufunga tena kwa kuwa walikuja kwa uoga walikuwa wanajua kwamba wanakuja kucheza na kiboko ya wanaume wa Dar.
“Tunawapongeza kwa matokeo ambayo wamepata na tunatambua kwamba wachezaji wao watakuwa wamepata tabu na hawaamini kama wamepata matokeo kwenye mchezo dhidi ya Tabora United.”
MECHI ZINAZOFUATA KWA SIMBA HIZI HAPA

Fountain Gate v Simba, Februari 6 2025, mchezo huu Simba itakuwa ugenini, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Simba ilipata ushindi wa mabao 4-0, Simba v Tanzania Prisons, Februari 11 2025, mchezo huu Simba itakuwa Uwanja wa KMC, Complex.
Simba v Dodoma Jiji, Februari 15 2025, mchezo huu unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 lilifungwa na Jean Ahoua kwa pigo la penati. Simba v Azam FC, Februari 24 2025 mchezo huu unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC, Complex kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Simba ilipata ushindi wa mabao 2-0.

