Leo saa 10 jioni huenda sehemu kubwa ya shughuli zote za nchi zitasimama kwa ajili ya kupisha dakika 90 za mchezo mkali na unaosubiriwa kwa hamu kati ya vinara wa Ligi Kuu Bara mpaka sasa kikosi cha Simba ambao watashuka uwanjani kuvaana na Singida Black Stars kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu unatarajia kupigwa katika Uwanja wa Liti uliopo mkoani Singida, ambapo pia unatarajia kuwa mchezo wa 15 na wa mwisho kwa Simba wakiwa wanakamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi.
Mpaka sasa Simba wanaendelea kusalia kileleni mwa ligi Kuu Bara mara baada ya kufanikiwa kukusanya pointi 37 na endapo watafanikiwa kushinda mechi ya leo watafikisha 40 ambazo hata timu nyingine zikicheza mechi zao haziwezi kuwafikia.
Kumbuka unaweza kubashiri mchezo huu na michezo ya ligi mbalimbali kupitia Kampuni bora ya michezo ya kubashiri ya SportPesa kwa kutembelea tovuti ya www.sportpesa.co.tz
KOCHA SIMBA, FADLU ANASEMAJE?

Kocha Mkuu wa kikosi cha Simba, Fadlu Davids ameweka wazi kuwa wanatarajia mchezo huo utakuwa mgumu, lakini wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanafanya vizuri na kuondoka na alama zote tatu ugenini.
Kocha Fadlu pia aliongeza kuwa kikosi chake kipo kwenye hali nzuri na wamepata siku mbili kwa ajili ya mazoezi tangu walivyocheza mechi ya mwisho dhidi JKT Tanzania na wako tayari kwa mchezo dhidi ya Singida.
“Maandalizi ya mchezo yamekamilika, jana jioni tumefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Liti na wachezaji wote wapo timamu kwa mchezo,” amesema Fadlu.
WACHEZAJI SIMBA WAPO TAYARI

Akizungumzia kwa niaba ya wachezaji wa vinara hao wa ligi, kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema kila mmoja anafahamu umuhimu wa mchezo wa leo na yupo tayari kupambana ili timu yao ipate ushindi.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha tunapata matokeo ya alama tatu ugenini.
“Tulikuwa kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya mchezo wetu huu na jana jioni tulifanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Liti tayari kwa mchezo wa kesho,” amesema Fadlu.
Naye Kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma ambaye msimu uliopita alikuwa Singida Black Stars amesema itakuwa furaha kwake kama ataisaidia timu hiyo kupata alama tatu leo.
“Singida ni timu iliyonipa heshima kubwa lakini sasa nipo Simba hivyo nitahakikisha napambana mpaka mwisho kuisaidia timu kupata ushindi na hiyo itakuwa furaha kubwa kwangu,” amesema Kagoma.
SIMBA KUENDELEZA WIMBI LA USHINDI?

Ikumbukwe Simba wanaingia katika mchezo huu wakiwa na kumbukumbu nzuri ya mwendelezo wa matokeo ya ushindui mfululizo katika michezo yao iliyopita ambapo mechi ya mwisho walikutana na JKT Tanzania ambapo Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika mchezo huo, bao la dakika ya mwisho lililofungwa kwa mkwaju wa penati na kiungo mshambuliaji wao, Jean Charles Ahoua liliwawezesha kuwapa ushindi dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa KMC Complex.
Ahoua alifunga bao hilo dakika ya tano ya nyongeza kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi David Bryson kufanya madhambi ndani ya 18 akiwa katika harakati za kuokoa.
Katika mchezo huo Simba walianza kwa kasi, huku tukishambulia lazidi lango la JKT lakini kikwazo kikubwa kilikuwa mlinda mlango, Yakubu Mohamed. Kiungo mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu alifanya jitihada za kuipambania timu yake kupata bao la uongozi lakini hata hivyo mashuti yake matatu yaliishia mikononi mwa Yakubu.
Kiungo mshambuliaji wa JKT Tanzania, Mohamed Bakari alitolewa baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya tano ya nyongeza baada ya kumchezea madhambi Shomari Kapombe ndani ya 18. Ushindi huo uliwafanya Simba pointi 37 baada ya kucheza mechi 14 ambapo wanaendelea kuwa kileleni mwa msimamo.
Kikosi cha Simba kilichoanza mchezo uliopita ambacho kina nafasi kubwa ya kuanza le ni Pamoja na; Camara, Kapombe, Nouma (Zimbwe Jr 70′), Che Malone, Hamza, Ngoma, Awesu (Ahoua 45′) Fernandez (Mashaka 77′) Ateba (Mukwala 59′), Mpanzu (Mutale 59′), Chasambi
