Kibu- AwesuKibu- Awesu

AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wachezaji wao wanahitaji pongezi kwa kwa kupata ushindi dhidi ya SC Sfaxine mchezo wa kimataifa uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho katika dakika 90 za kazi Uwanja wa Mkapa.

Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 2-1 SC Sfaxine huku mabao yote kwa Simba yakifungwa na Kibu Dennis dakika ya 7 na 90 lile la SC Sfaxine likifungwa na Hazem Hasen dakika ya 3 kwa makosa ya safu ya ulinzi ya Simba.

Ally amesema kuwa ulikuwa ni mchezo wenye presha kubwa huku wengi wakiamini kazi imeisha kwa kuvuna pointi moja mpaka bao la Kibu lilipofungwa na kuibua shangwe kubwa Uwanja wa Mkapa.

Ahmed
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba. Source: Simba.

“Ilikuwa kazi kubwa unaona namna timu ilivyokuwa ikipambana kusaka matokeo na hakuna ambaye alikuwa anajua nini ambacho kitatokea na mwisho ushindi umepatikana hili ni jambo kubwa pongezi kwa wachezaji kwa kuwa wametuheshimisha.

“Hawa wapinzani wetu kwenye mechi zilizopita walipoteza hivyo wakaona hamna namna lazima wapambane kupata angalau alama moja kwetu jambo ambalo liliongeza ugumu, hali ilikuwa ngumu kwa mashabiki lakini furaha imepatikana mwishoni kabisa.”

KUNDI A LAMOTO

Simba kimataifa
Nyota wa Simba kwenye anga la kimataifa 2024 Uwanja wa Mkapa. Source: Simba.

Baada ya mechi tatu katika kundi A kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika limekuwa ni moto kwa kuwa timu tatu zimevuna pointi sita.

Simba nafasi ya tatu kwenye msimamo, Costantine ni nafasi ya pili na vinara ni FC Bravos wakiwa na pointi sita kibindoni ndani ya dakika 270.

Anayeburuza mkia ni CS Sfaxine ambaye huyu kwenye mech izote tatu alizoshuka uwanjani aliambulia kichapo kwa kufungwa ndani ya dakika 270 hivyo hajawa na mwendo mzuri kwenye mechi zake kimataifa.

KIMATAIFA KETE ILIPIGWA HIVI

FADLU
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, Source: Simba.

Kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa kazi ya Fadlu Davids ambaye ni Kocha Mkuu wa Simba ilikuwa kuwaongoza vijana wake kwenye mpango kazi wa kusaka pointi tatu na mwisho ikawa hivyo kwa ushindi.

 

Kikosi kazi cha Fadlu kilikuwa namna hii:-Mousa Camara, Fabrice Ngoma, Jean Ahoua, Shomari Kapombe, Leonel Ateba , Hamza, Zimbwe Jr ambaye ni nahodha mwenye bao moja katika anga la kimataifa kwenye hatua ya makundi alipachika bao kwenye mchezo dhidi ya Constantine ugenini.

 

Mavambo, Che Malone kiongozi kwenye safu ya ulinzi, Awesu Awesu ikiwa ni mchezo wake wa kwanza kuanza kikosi cha kwanza katika hatua ya makundi kimataifa   na mkandaji Kibu Dennis.

 

Kwa wachezaji wa akiba ni Yusuph Kagoma huyu alirejea kikosini baada ya kuwa nje kwa muda kwa kuwa hakuwa fiti, Aishi Manula naye karudi kundini, Chamou, Nouma, Mzamiru Yassin, Okejapha, Mutale, Chasambi na Mukwala.

REKODI ZA MCHEZO KWA SIMBA

Kibu na Ahoua
Kibu na Ahoua kwenye anga la kimataifa 2024.Source: Simba.

Katika dakika 90 za mchezo huo wa kimataifa, rekodi zinaonyesha kuwa Simba ilikuwa imara kwenye upande wa umiliki wa mpira na kufanya mashambulizi zaidi kwa wapinzani wao licha ya kupata mabao mawili.

Jumla ilipiga mashuti 17 huku wapinzani wakipiga mashuti 5 na ambayo yalilenga lango kwa Simba ni 6 huku wapinzani wao mashuti mawili pekee yalilenga lango na moja likiwa ni bao kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa. Kwa upande wa umiliki wa mpira, Simba ilimiliki asilimia 75.8 na SC Sfaxine ilikuwa ni asilimia 24.2 ndani ya dakika zote 90. Faulo jumla kwa Simba walicheza 14 na walichezewa faulo  14.

 

MECHI YAO HII HAPA YA LIGI

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imefanya maboresho ya ratiba ya michezo miwili ya klabu ya Simba ambapo mchezo wa kwanza dhidi ya Singida Big Stars ambao awali haukupangiwa tarehe sasa utachezwa Desemba 28, 2024 kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Mchezo wa pili dhidi ya Tabora United ambao ulipangwa kuchezwa Desemba 28, 2024 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora umeondolewa na utapangiwa tarehe mpya. Ikumbukwe kwamba mchezo wa kwanza kwenye mchezo dhidi ya Tabora United, Uwanja wa KMC, Simba iliibuka na ushindi na kukomba pointi tatu mazima.

Share this: