WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho Simba wakiwa hatua ya makundi wamewaomba wachezaji wa Pamba Jiji ya Mwanza kucheza mpira ndani ya dakika 90 za ushindani na kuacha tabia za kukamia mechi na kuwaparura wachezaji wao.
Simba yenye pointi 25 ni vinara kwenye ligi baada ya kucheza mechi 10 ina kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya Pamba Jiji, Novemba 22 Uwanja wa Kirumba mchezo wa ligi mzunguko wa kwanza.

Ipo wazi kwamba mabingwa watetezi ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa hawa wapo nafasi ya pili kwenye msimamo watapeperusha bendera kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa anawaomba wachezaji wa Pamba Jiji kucheza mpira na sio kuwaumiza wachezaji.
“Ninarudia tena wachezaji wa Pamba waje tucheze mpira wasije kucheza kama wametumwa, wasije kucheza mpira wa hovyo wakutaka kuwaumiza wachezaji wetu wasicheze mechi za kimataifa.
“Tunawaomba waamuzi wawe macho kwenye hili waangalie wachezaji ambao watakuja kucheza kwa nia ovu, tunakumbuka suala la Moses Phiri inatuuma mpaka leo wamemuharibia kabisa kijana.
“Simba tuna kibarua kigumu cha kufanya kwenye michuano ya kimataifa. Kila mmoja acheze kwa uwezo wake. Pamba nit imu nzuri na ina wachezaji wazuri hivyo wacheze mpira.
SIMBA NDANI YA MWANZA

Novemba 20 jioni wachezaji wa Simba, benchi la ufundi na viongozi walikwea pipa na kuibukia Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao dhidi ya Pamba ambao ni mzunguko wa kwanza kisha watarejea Bongo kwa maandalizi ya kuwakabili wapinzani wao Bravos.
Mchezo wao dhidi ya Bravos ya Angola utakuwa ni wa Kombe la Shirikisho Afrika unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Novemba 27 kwa wababe hao wote kila mmoja kusaka pointi tatu muhimu ndani ya uwanja.
Miongoni mwa wachezaji ambao wapo Mwanza ni Mousa Camara kipa namba moja wa Simba ambaye alikuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Guinea, Fabrince Ngoma, Mzamiru Yassin, Leonel Ateba ambaye ni mshambuliaji huku Mukwala akitarajiwa kuungana na timu leo kwa kuwa alikuwa kwenye majukumu ya taifa.
KIMATAIFA HESABU ZIPO NAMNA HII

“Novemba 24 utakuwa uzinduzi rasmi wa hamasa, hekaheka zitaanza siku hiyo. Tutaanzia kwenye tawi la Simba Bomba Mbili kwa Chela lipo Mombasa Midizini. Tutafanya balaa kubwa kuanzia saa 5 asubuhi. Tukimaliza hapo tutakwenda uzinduzi part two Kiwalani Minazi Mirefu. Siku hiyo toka nyumbani umejiandaa.
“Novemba 25 siku ya Jumatatu itakuwa siku ya kuchangia damu, mmemsikia Mwenyekiti Mangungu amelisema hilo. Tutawatangazia vituo vya Mbagala, Karume kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wenzetu. Na inaweza kukusaidia wewe mwenyewe au ndugu yako.
“Novemba 26 tutakuwa na tour kuanzia Temeke, Mtoni kwa Aziz Ally kwenda hadi Mbagala kuwambia Wanasimba umuhimu wa mchezo huo na kuwauzia tiketi.
“Novemba 27 itakuwa siku ya mchezo na uchaguzi wa Serikali za mtaa lakini pia siku hiyo itakuwa siku ya mapumziko. Mwanasimba asubuhi utapiga kura na baada ya hapo moja kwa moja safari Uwanja wa Mkapa kwenda kuishangilia timu yako ya Simba.
“Mchezo huo ni wa kwanza wa makundi na lazima tuanze vizuri kwa kupata ushindi na ili kupata ushindi lazima kufanya kazi kubwa. Siku hiyo lazima tukaujaze uwanja, mkiujaza uwanja tutakuwa katika sehemu nzuri ya kupata ushindi. Tutumie nguvu zetu zote kuhakikisha tunapata ushindi.
SEMAJI LATAMBA MECHI KUWA NA MVUTO

“Tunataka mechi zetu ndio ziwe zenye mvuto zaidi kuliko mechi zote kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Kama unajijua hujawahi kwenda Uwanja wa Mkapa hii ndio mechi yako.
“Mara ya mwisho Kombe la Shirikisho Afrika tulitolewa na Orlando Pirates pale Afrika Kusini, mwaka huu breki ya kwanza ni nusu fainali na pale na fainali ni karibu sana. Na timu ya kutufikisha hapo tunayo.
VIINGILIO HIVI HAPA
“Viingilio kwenye mchezo mzunguko Tsh. 5,000 Machungwa Tsh. 10,000, VIP C Tsh. 15,000, VIP B Tsh. 20,000, VIP A – Tsh. 50,000, Platinum Tsh. 150,000 (usafiri wa pamoja wakiwa na escort, eneo maalumu kukaa na chakula) Tanzanite Tsh. 250,000 (VVIP, Gate Pass na jezi mpya).

