Saed na Aziz KiSaed na Aziz Ki

KUMEKUCHA Yanga baada ya benchi jipya kuwa kamili kwa kazi kuendeleza makali ndani ya uwanja kwenye msako wa pointi tatu ndani ya dakika 90 kitaifa na kimataifa baada ya kuachana na Miguel Gamondi.

Ipo wazi kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa imefanya maboresho makubwa kwenye benchi la ufundi baada ya kutokuwa kwenye mwendo mzuri katika mechi za hivi karibuni.

Gamondi alikiongoza kikosi cha Yanga kwenye mechi 10 za ligi ambapo alipata ushindi kwenye mechi 8 na kupoteza katika mechi mbili mfululizo zilichezwa Uwanja wa Azam Complex ambao ulikuwa unatumika na Yanga kwenye mechi za nyumbani.

KAZI IMEANZA JANGWANI

Mustafa
Mustafa kocha msaidizi wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Baada ya utambulisho wa Kocha Mkuu Sead Ramovic ambaye anarithi mikoba ya Gamondi na Mustafa Kodro ambaye atakuwa kocha msaidizi ndani ya Yanga tayari wameanza kazi ndani ya timu hiyo kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal unaotarajiwa kuchezwa Novemba 26, 2024 Uwanja wa Mkapa.

Abdi Moalin aliyekuwa kocha wa KMC yeye ametambulishwa kuwa Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi baada ya kusitisha mkataba wake na waajiri wake wa zamani ambapo sasa KMC ni Kali Ongala huyu ametambulishwa kuwa kocha mkuu.

Moalin amesema kuwa ni furaha kwake kuwa ndani ya timu kubwa na malengo ni kuona wanafikia mafanikio kwa kuwa inawezekana.

“Ni furaha kubwa kwangu kuwa kwenye timu hii kubwa yenye historia na kikubwa, furaha ni kuona kuwa ninakuwa sehemu ya mafanikio siku zijazo.”

 

MASHABIKI WAITWA KWA MKAPA

Ali Kamwe
Ali Kamwe Ofisa Habari wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao ujao kimataifa dhidi ya Al Hilal kwa kuwa wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu na wanahitaji matokeo.

“Huyu Al Hilal mara ya mwisho alituachia simanzi hapa kwa Mkapa, sasa hiki ni kisasi na tusikiache kipite, twendeni pamoja tukalipe kisasi hiki, tuwaambie tu, vita ya Yanga safari hii asikatize mtu mbele, kuna Bendera ya Yanga na Bendera ya Taifa tunaibeba hapa, twendeni tukaweke heshima Wananchi.

“Mashabiki tujitokeze kwa wingi uwanjani kwenye mchezo wetu muhimu kwani Yanga haijawahi kufungwa mechi tatu mfululizo, viingilio ni rafiki kabisa mzunguko ni 3,000, VIP C 10,000, VIP B 20,000 na VIP A 30,000.”

MWISHO WA GAMONDI

Gamondi
MIGUEL Gamondi aliyekuwa kocha wa Yanga na Kibabage: Source: Yanga.

Mwisho wa Gamondi ndani ya Yanga ilikuwa ni Novemba 15 2024 ambapo taarifa rasmi kutoka Yanga ilieleza kuwa Yanga imevunja mkataba na kocha huyo kuendelea kuwa kwenye benchi la ufundi.

Ni mkataba wa mwaka mmoja kocha huyo aliongeza baada ya msimu wa 2023/24 kugota mwisho hivyo alikuwa na kazi kupambania 2024/25 kabla ya mechi 15 upepo umebadilika hatakuwa ndani ya Yanga.

Mbali na Gamondi kocha msaidizi Moussa Ndaw naye mkataba wake ulivunjwa ambapo uongozi wa Yanga uliwashukuru kwa kazi ambayo waliifanya na kuwatakia kila la kheri kwenye majukumu yao mengine.

 JEMBE KUHUSU MRITHI WA GAMONDI

Saed
Saed kocha mpya wa Yanga mrithi wa mikoba ya Miguel Gamondi 2024/25. Source: Yanga.

Mwandishi wa Habari za Michezo Bongo ambaye ni Legend pia katika anga la kimataifa Saleh Ally maarufu kwa jina la Jembe ameweka wazi kuwa uongozi wa Yanga umepatia kumleta kocha mpya wakati huu lakini hukumu inakuja ikiwa atashindwa kupata matokeo mazuri.

Yanga wamepatia kwenye kumtambulisha kocha mpya licha ya kuwa hana CV kubwa inayomuonesha kuwa anauwezo wa kuhimili yote katika ushindani ndani ya kikosi cha Yanga lakini hilo halishangazi kwani kinachohitajika kwenye timu ni ushindi.

“Lakini kwa kuwa viongozi wameona ni muda wa kuachana na Miguel Gamondi kisha mikoba yake ikawa mikononi mwa Saed Ramovic ninaweza kusema kwa wakati huu wamepatia. Hivyo tusubiri matokeo ya uwanjani namna yatakavyokuwa.

“Unajua mwalimu hahukumiwi kulingana na CV yake ametoka wapi? Alifanya nini huko? Na huku kuna nini hapana! Kinachotoa hukumu ni matokeo uwanjani.

“Nilisema hivyo wakati anakuja Nasreddine Nabi na hata alipoondoka na nafasi yake kuwa mikononi mwa Gamondi bado nilisema kwamba Yanga wamepatia kwa kumleta kocha mpya kwa kuwa ni mwanzo.

“Kumbuka Gamondi anakuja Yanga Nabi akiwa ametoka kufanya vizuri na timu yeye alianza kupata matokeo na timu ikafika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya muda mrefu kupita na ameondoka.

“Huyu kocha mpya atahukumiwa kwa matokeo uwanjani katika mechi za ushindani. Kumbuka Uchebe, (Patrick Aussems) alikuja Simba akiwa hana rekodi kubwa ila alifanya vizuri akiwa na kikosi hicho kwenye mechi za ushindani na ameacha rekodi nzuri mpaka anaondoka.”

Share this: