VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids balaa lao sio la kitoto kutokana na mwendo wao ndani ya uwanja msimu wa 2024/25 kwenye msako wa pointi tatu muhimu ndani ya uwanja baada ya kucheza mechi 10 ambazo ni dakika 900.
Ikumbukwe kwamba ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa hawa ni mabingwa watetezi walitwaa taji hilo msimu wa 2023/24 walikamilisha msimu wakiwa na pointi 80 zama za Miguel Gamondi.

MWENDO WA SIMBA BONGO KWENYE LIGI
Simba 3-0 Tabora United mchezo huu ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 18 2024 ni mchezo wa kwanza kwa Simba kwenye ligi na mtupiaji bao la kwanza ni Che Malone ilikuwa dakika ya 14.
Simba 4-0 Fountain Gate, huu ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Simba ulichezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa Agosti 25 2024.
Azam FC 0-2 Simba huu ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kucheza ugenini ulichezwa Uwanja wa New Amaan Complex Septemba 26 2024.
Dodoma Jiji 0-1 Simba ilikuwa Septemba 29 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma walisepa na pointi tatu kwenye mchezo huu.
Simba 2-2 Coastal Union kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ilikuwa ni Oktoba 4 2024.

Simba 0-1 Yanga ni Oktoba 19 2024 kwenye Kariakoo Dabi, Simba ilipoteza pointi tatu kwa bao la kujifunga lake Kelvin Kijili, Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo huu nyota Yusuph Kagoma alipata maumivu.
Tanzania Prisons 0-1 Simba ilikuwa Uwanja wa Sokoine, ilikuwa ni Oktoba 22 2024. Simba 3-0 Namungo ilikuwa Uwanja wa KMC, Mwenge, Oktoba 25 2024.
Mashujaa 0-1 Simba, Novemba Mosi 2024, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma. Simba 4-0 KMC ilikuwa Novemba 6 2024 Uwanja wa KMC, Mwenge.
HAPA NDIPO WALIPO
Baada ya mechi 10 ndani ya ligi ambazo ni dakika 900, ni nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi wakikomba jumla ya pointi 25 na safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 21 na ukuta umeruhusu mabao matatu ya kufungwa.
Ni mchezo mmoja pekee Simba ilifungwa mabao mengi ilikuwa dhidi ya Coastal Union ambapo kipa namba moja Moussa Camara alitunguliwa mabao mawili kwenye mchezo huo walipogawana pointi mojamoja wakiwa Uwanja wa KMC, Mwenge.
Mchezo wao uliofuata ilikuwa dhidi ya Yanga ni Camara alianza langoni na kufungwa bao moja akiwa shuhuda wakiyeyusha pointi tatu mazima kwa mara ya kwanza ndani ya msimu wa 2024/25 ambao una ushindani mkubwa mwanzo mwisho.
CAMARA NAMBA MOJA

Kwenye rekodi za makipa ambao hawajafungwa mechi nyingi, kipa wa Simba Camara ni namba moja akiwa hajafungwa kwenye mechi 8 ndani ya uwanja huku mbili akitunguliwa kati ya 10 ambazo ameanza langoni.
Camara ambaye kwenye mchezo dhidi ya Azam FC alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo hu oni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids ambaye ameweka wazi kuwa kipa huyo anafanya kazi kubwa kwa ushirikiano na wengine kutafuta matokeo muhimu.
“Ushindi ambao unapatikana uwanjani ni muhimu na kila mchezaji anatimiza majukumu yake vizuri. Utaona kwamba kwenye mchezo wetu ambao tuliruhusu mabao dhidi ya Coastal Union, haina maana kwamba ni makosa ya kipa peke yake hapana.
“Makosa ambayo yanatokea uwanjani hayoni ya timu nzima ndio maana unaona kwamba tukishinda tunashangilia Pamoja, hakuna ambaye atasema huu ushindi ni wa mchezaji Fulani, Kinachotokea makosa tunafanyia kazi ili kuwa imara kwenye mechi zinazofuata.”
SEMAJI HILI HAPA

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema ubaya ubwela kwa sasa unaendelea kufanya kazi kwa vitendo hivyo wengi watapata kile ambacho kinawastahili na wapo ambao watashtuka zaidi.
“Mwendo wa kusaka ushindi kwenye mechi zetu na ubaya ubwela kwa sasa unakwenda kwenye vitendo zaidi, lazima wapate tabu na watashtuka zaidi kwa kuwa kazi inaendelea na hakuna ambaye alitarajia kuona haya yote yakitokea.
“Ipo wazi kwamba ushindani ni mkubwa kwa kuwa kila timu ina malengo ya kupata matokeo mazuri uwanjani hilo tunalifahamu, wachezaji wanapambana bado viwango vinazidi kuwa imara kwani kila mchezaji hajafikia ule ubora wake wa hali ya juu.”

