Sead RamovicSead Ramovic

KIBOKO ya Simba masta Miguel Gamondi mbinu zake hazitatumika kwenye mechi zote za ushindani ndani ya msimu wa 2024/25 baada ya mkataba wake kusitishwa rasmi Novemba 15 2024 hivyo ni kocha mpya atakuwa ndani ya Yanga hivyo lile kuti kavu alilokalia limekatika.

 

MIGUEL
Miguel Gamondi, aliyekuwa kocha wa Yanga akiwa na Kibabage. Source: Yanga.

Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ni mabingwa watetezi wa ligi walitwaa taji hilo wakiwa na jumla ya pointi 80 baada ya kucheza jumla ya mechi 30 msimu wa 2023/24.

 

Ni masta Gamondi alikuwa benchi akitumia mbinu ambazo zilikomba pointi sita mazima mbele ya Simba kwa ushindi nje ndani na mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu wa 2024/25 alikomba pointi tatu tena za Simba.

 

Sead
Sead Kocha Mkuu wa Yanga akiwa na CEO wa Yanga. Source: Yanga.

Ni Saed Ramovic raia wa Ujerumani huyu atakuwa mchora ramani wa mbinu za ushindi za kikosi cha Yanga yupo Bongo na anatarajiwa kuanza kazi yake kukinoa kikosi hicho kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan unaotarajiwa kuchezwa Novemba 26 2024.

 

Ikumbukwe kwamba mchezo wa mwisho kwa Gamondi kukaa benchi alishuhudia ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Yanga 1-3 Tabora United.

 

 

 

Pacome- Aziz na Maxi
Mastaa wa Yanga wakishangilia kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi msimu wa 2023/24 waliposhinda 5G dhidi ya Simba. Source: Yanga.

Gamondi masta aliwapa tabu watani zao wa jadi Simba atakumbukwa kwa kutembeza 5G kwenye Kariakoo Dabi ilikuwa 2023/24, alianza kwa ushindi kwenye mechi 8 mfululizo 2024/25 ila upepo ulibadilika baada ya ubao wa Azam Complex kusoma Yanga 0-1 Azam FC.

 

Kabla hajatulia ubao ukasoma Yanga 1-3 Tabora United, Novemba 15 2024 Yanga rasmi wamebainisha kuwa hawatakuwa na Gamondi na wamemtangaza Saed Ramovic kuwa mrithi wa mikoba yake Jangwani.

REKODI ZA GAMONDI YANGA KWENYE LIGI

Kagera Sugar 0-2 Yanga mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Kaitaba, Agosti 29 2024 na mtupiaji wa bao la kwanza ni Maxi Nzengeli ndani ya Yanga kwenye ligi. Ken Gold 0-1 Yanga huu ulikuwa mchezo wa pili kwa Yanga ugenini ilikuwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya mtupiaji alikuwa ni Ibrahim Bacca ambaye alitumia pasi ya Aziz Ki Septemba 25 2024.

 

Sillah Gibril
Nyota wa kwanza kuifunga Yanga kwenye ligi 2024/25 Sillah. Source: Azam FC.

Yanga 1-0 KMC, mchezo wa kwanza wakiwa Uwanja wa Azam Complex msimu wa 2024/25 ilikuwa Septemba 29 2024.

Yanga 4-0 Pamba Jiji ushindi mkubwa kwa Yanga ndani ya 2024/25 walikuwa Azam Complex  ilikuwa Oktoba 3 2024. Kwenye mechi nne za Yanga ilikuwa haijapoteza wala kufungwa ndani ya uwanja.

Oktoba 19 2024 ilikuwa ni Kariakoo Dabi baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga, bao la kujifunga la Kelvin kijili dakika ya 86 liilipa pointi tatu Yanga chini ya masta Gamondi.

Oktoba 22 2024 ilikuwa Yanga 2-0 JKT Tanzania mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Azam Complex ambapo Yanga ilikuwa haijafungwa bao langoni alikuwa ni Djigui Diarra.

Coastal Union 0-1 Yanga mchezo huu Yanga ilikomba pointi tatu kwa bao la Jean Baleke likiwa ni bao lake la kwanza akiwa na uzi wa Yanga chini ya Gamondi.

Kete ya nane ilikuwa ugenini ambapo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Singida Black Stars 0-1 Yanga, bao la ushindi lilifungwa na Pacome ambaye alifunga akiwa nje ya 18 kwa shuti ambalo lilimshinda mlinda mlango Metacha Mnata.

 

HAPA TATIZO LILIANZIA YANGA

Kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Azam FC uliochezwa Uwanja wa Azam Complex Novemba 2 2024 hapo ndipo tatizo lilianzia kwa Yanga kuonja joto ya jiwe kwa mara ya kwanza ndani ya msimu wa 2024/25 wakiwa nyumbani.

Nyota Gibril Sillah alifunga bao pekee la ushindi kwenye mchezo huo dakika ya 33 lilidumu mpaka mwisho wa mchezo ambapo Yanga ilipoteza pointi tatu kwa mara ya kwanza na Diarra akatunguliwa bao moja kwenye mchezo huo.

Kete ya 10 ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Tabora United nao ulichezwa Uwanja wa Azam Complex baada ya dakika 90 ubao ukasoma Yanga 1-3 Tabora United, hapo upepo ukabadilika na tetesi zikaanza kueleza kuwa Gamondi amekalia kuti kavu.

Ikumbukwe kwamba Gamondi aliweka wazi kuwa baada ya kupoteza pointi tatu kwenye mchezo dhidi ya Tabora United hakuwa na wakumlaumu kwani wachezaji wake walipata nafasi hawakuzitumia kwenye mchezo huo.

“Tulikuwa na mchezo mgumu lakini hakuna wa kumlaumu kwa kuwa wachezaji walipata nafasi hakuna ambaye alizitumia, unaona Aziz Ki alikosa penalti kwenye mchezo wetu na Kened Musonda alikosa nafasi ya kufunga hivyo ni matokeo ya mchezo.”

 

 

 

Share this: