WAKUBWA watakuwa kazini ndani ya New Amaan Complex kusaka pointi tatu ndani ya uwanja ambapo Singida Black Stars baada ya kucheza mechi 8 ambazo ni dakika 720 hawajapoteza wanakutana na Yanga.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa baada ya kucheza mechi 7 ambazo ni dakika 630 haijapoteza pia hivyo mchezo huu ni wakubwa wa kazi ambao hawajakutana na balaa la kupoteza pointi tatu.
HIZI HAPA MECHI ZA YANGA

Kagera Sugar 0-2 Yanga mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Kaitaba, Agosti 29 2024 na mtupiaji wa bao la kwanza ni Maxi Nzengeli ndani ya Yanga kwenye ligi.
Ken Gold 0-1 Yanga huu ulikuwa mchezo wa pili kwa Yanga ugenini ilikuwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya mtupiaji alikuwa ni Ibrahim Bacca ambaye alitumia pasi ya Aziz Ki Septemba 25 2024.
Yanga 1-0 KMC, mchezo wa kwanza wakiwa Uwanja wa Azam Complex msimu wa 2024/25 ilikuwa Septemba 29 2024.
Yanga 4-0 Pamba Jiji ushindi mkubwa kwa Yanga ndani ya 2024/25 walikuwa Azam Complex ilikuwa Oktoba 3 2024.
Oktoba 14 2024, Simba 0-1 Yanga mchezo wa kwanza kupoteza mtupiaji ni Maxi Nzengeli dakika ya 86.
Oktoba 22 2024, Yanga 2-0 JKT Tanzania, Uwanja wa Azam Complex.
DIARRA ALIKOSEKANA HAPA

Kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union mwamba Diarra alikosekana kikosi cha kwanza ukiwa ni mchezo wake wa kwanza msimu wa 2024/25 kutoanza kwenye majukumu yake na haya yalitokana na adhabu ya kadi tatu za njano.
Kipa Khoemeny Aboubhakar aliaza kwenye mchezo huo ugenini ikiwa ni mchezo wake wa kwanza kukaa langoni baada ya kukabidhiwa uzi wa timu hiyo inayonolewa na Gamondi.
Baada ya dakika 90 Oktoba 26 2024, ilikuwa Coastal Union 0-1 Yanga, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, bao la ushindi likifungwa na Jean Baleke dakika ya 23 ikiwa ni bao la kwanza kwenye ligi.
YANGA HAIJARUHUSU BAO LA KUFUNGWA
Yanga kwenye mechi zake saba mfululizo ndani ya ligi haijaruhusu bao la kufungwa, ikiwa ni timu pekee Bongo kutotambua ladha ya kufungwa kwenye mechi za ligi uwanjani. Kipa namba moja ni Djigui Diarra alikaa langoni kwenye mechi sita na zote hakufungwa huku mchezo wa saba ni Khomeiny Aboubhakar alianza kikosi cha kwanza dhidi ya Coastal Union.
GAMONDI HUYU HAPA

Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Singida Black Stars ni mkubwa kutokana na aina ya timu ambayo wanakutana nayo lakini mpango ni kupata pointi tatu muhimu.
“Unajua huu ni mchezo muhimu na tunakutana na timu ambayo haijapoteza mchezo ikiwa juu kwenye msimamo wa ligi, tunahitaji kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu ili kupata pointi tatu muhimu hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwa pamoja nasi.”
UCHEBE AUNGURUMA KIBABE
Patrick Aussems, Kocha Mkuu wa Singida Black Stars amebainisha kuwa hawana hofu na mchezo wao dhidi ya Yanga wataingia kuwanjani kwa tahadhari kutafuta matokeo mazuri kwenye mchezo huo.
“Ikiwa unakutana na timu kubwa kinachohitajika ni ushindi, kila mchezaji yupo tayari na hatuna sababu ya kuwahofia wapinzani wetu kwani wote tunacheza mpira mmoja, makosa tutafanyia kazi na ambacho tunakitafuta ni matokeo.”
HAWA HAPA SINGIDA BLACK STARS
Metacha Mnata kwenye mechi ambazo alikuwa langoni ilikuwa namna hii:-Ken Gold 1-3 Singida Black Stars, Agosti 24 2024.
Agosti 24 2024, Kagera Sugar 0-1 Singida Black Stars, huu ulichezwa Uwanja wa Kaitaba.
Septemba 12 2024, Singida Black Stars 2-1 KMC ngoma ilipigwa Uwanja wa Liti.
Septemba 17 2024, Pamba Jiji 0-1 Singida Black Stars hii ilikuwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Septemba 29 2024, Singida Black Stars 1-1 JKT Tanzania huu ulichezwa Uwanja wa Liti.
Oktoba 4 2024, Mashujaa 0-1 Singida Black Stars mchezo huu ulichezwa mwisho wa reli, Kigoma Uwanja wa Lake Tanganyika.
Oktoba 20 2024, Singida Black Stars 2-0 Namungo hii ilikuwa Uwanja wa Liti.
Oktoba 25 2024, Singida Black Stars 2-0 Fountain Gate mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Liti.
MABAO YAKUFUNGWA KIDUCHU

Singida Black Stars imekuwa kwenye mwendo wake ndani ya uwanja ambapo imefungwa mabao machache katika mechi za ushindani msimu wa 2024/25 ndani ya dakika 720.
Ukuta wa Singida Black Stars yenye Kenedy Juma ambaye ni nahodha umeruhusu mabao matatu ikiwa ni wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 240.
Kwenye mechi hizo kipa namba moja ni Metacha Mnata ambaye anaingia kwenye orodha ya makipa waliookoa penalti ndani ya msimu wa 2024/25 kwenye mechi za ligi.Ikumbukwe kwamba nyota huyu aliwahi kucheza katika kikosi cha Yanga msimu wa 2023/24.

