Kibu v Prisons SokoineKibu v Prisons Sokoine

KIVUMBI cha Ligi Kuu Bara kinatarajiwa kuendelea leo Oktoba 29 2024 kwa baadhi ya timu kuwa uwanjani kusaka pointi tatu muhimu ndani ya uwanja  huku mabingwa watetezi Yanga wakiwa na kibarua kwenye funga Oktoba ugenini na mchezo wa ligi uliotarajiwa kuwakutanisha Simba dhidi ya JKT ukiahirishwa.

Yanga inayodhaminiwa na SportPesa baada ya kucheza mechi 7 zote imesepa na pointi tatu kibindoni ikiwa na jumla ya pointi 21 huku vinara wakiwa ni Singida Black Stars ya Singida ambayo inatumia Uwanja wa Liti kwa mechi za nyumbani.

Jean Baleke
NYOTA wa Yaga, Jean Baleke kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union ya Tanga. Source: Yanga.

Mchezo uliopita Yanga ilikuwa ugenini dhidi ya Coastal Union ya Tanga ambapo baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ulisoma Coastal Union 0-1 Yanga, hiyo ilikuwa ni Oktoba 26 2024.

Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa ushindi ambao walipata mbele ya Coastal Union ulikuwa ni muhimu kutokana na hesabu ambazo wanazo kwenye mechi zote kuwa na ushindani mkubwa na ambacho kinahitajika ni pointi tatu muhimu.

“Kwenye mechi zetu zote ambazo tunacheza kila mchezaji anatambua kwamba ugumu upo, pongezi kwa wachezaji namna wanavyojituma kwenye kutimiza majukumu yao tuna amini itakuwa ni mwendelezo kwenye mechi zetu.”

 

Bao pekee la ushindi kwenye mchezo huo lilifungwa na Jean Baleke dakika ya 23 likiwa ni bao lake la kwanza kwenye ligi baada ya kutambulishwa na kikosi cha Yanga kwa msimu wa 2024/25.

 

HII HAPA RATIBA BONGO

Oktoba 29 Coastal Union yenye pointi 8 baada ya kucheza mechi 9 itawakaribisha Kagera Sugar yenye pointi 5 baada ya kucheza jumla ya mechi 8 ndani ya ligi na mchezo huo unatarajiwa kuchezwa saa 10:15 jioni.

Ken Gold ambayo haijawa kwenye mwendo mzuri baada ya kupanda daraja ikiwa nafasi ya 16 na pointi 4 baada ya kucheza mechi 9 mapema saa 8:00 mchana watakuwa na kazi ya kusaka ushindi dhidi ya Dodoma Jiji.

Ipo wazi kwamba Dodoma Jiji ipo nafasi ya 7 kwenye msimamo ina pointi 12 baada ya kucheza mechi 9 mchezo wake uliopita ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania ilipokomba pointi tatu mazima nyumbani kwa ushindi wa bao 1-0.

WASIOFUNGIKA MECHI YAO INAKUJA

PACOME
NYOTA wa Yanga ambayo haijafungwa kweye ligi msimu wa 2024/25; Source: Yanga.

Kwenye ligi msimu wa 2024/25 wababe wote 14 kila mmoja kaonja ladha ya kufungwa na miongoni mwa vigogo hao ni Simba ilifungwa na Yanga huku Azam FC ikifungwa na Simba huku Ken Gold ikiwa inashikilia rekodi ya kufungwa mechi nyingi ambazo ni 7 kati ya 9 ilizocheza.

Oktoba 30 ni Singida Black Stars dhidi ya Yanga timu hizi mbili zote hazijapoteza kwenye mechi walizocheza na mchezo huu unatarajiwa kuchezwa saa 2:30 usiku itakuwa Zanzibar, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Mshindi wa mchezo huo ataongeza nafasi ya kuwa namba moja kwa kuwa Singida Black Stars inaongoza ligi ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 8 inafuatiwa na Yanga iliyo nafasi ya pili pointi zake kibindoni ni 21.

MATOKEO YA OKTOBA 28 HAYA HAPA

 

Kihimbwa Fountain
NYOTA wa Fountain Gate kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mashujaa. Source: Yanga.

Oktoba 28 2024 ligi ilikuwa hewani na kuna mechi za kukata na shoka zilichezwa ndani ya dakika 90 kwenye msako wa pointi tatu muhimu na matokeo ilikuwa hivi:-

Fountain Gate 2-2 Mashujaa. Moja ya mchezo bora kwa washindani hawa wawili ikiwa ni Fountain Gate inayodhaminiwa na SportPesa, Mashujaa kutoka mwisho wa reli Kigoma.

Namungo FC 1-0 Pamba Jiji baada ya kupoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Simba kwa kufungwa mabao 3-0 Namungo waliibuka na kupata ushindi dhidi ya Pamba Jiji ya Mwanza.

 

KOCHA Mkuu wa Simba
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids. Source: Simba.

SIMBA NA JKT TANZANIA KUPANGIWA TAREHE

 Karimu Boimanda, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania amebainisha kuwa wamepokea taarifa kutoka uongozi wa JKT Tanzania kuhusu kupata ajali na maombi ya mechi kuahirishwa ambapo mchezo wao wa ligi dhidi ya Simba uliotarajiwa kuchezwa Oktoba 29 2024 umeahirishwa hivyo utapangiwa tarehe.

Boimanda amesema: “Mara nyingi huwa ninakuwepo hapa pamoja na wachezaji, manahodha kwenye eneo hili, imekuwa tofauti. Tumepata taarifa kuwa Klabu ya JKT Tanzania ilipata ajali wakati ikirejea kutoka Dodoma ambapo walikuwa na mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji.

“Basi walilokuwa wamepanda lilipata ajali maeneo ya Mbweni kwa niaba ya Bodi ya Ligi Tanzania tunawaombea warejee kwenye ubora. Kwanza tumepokea barua kutoka JKT Tanzania kuhusu kuomba kuahirishiwa michezo miwili inayofuata ilikuwa dhidi ya Simba na Namungo na tumepokea barua kutoka kwa daktari wa JKT Tanzania kuhusu hali za wachezaji.

“Mchezo mwingine ulikuwa ni dhidi ya Namungo ambao ulitarajiwa kuchezwa Uwanja wa Majaliwa Novemba 4 na wenyewe umeahirishwa kutokana na sababu ambazo zimetajwa. Hii ni taarifa ambayo tumeipokea hivyo mechi hizi zitapangiwa tarehe, tunawapa pole sana JKT Tanzania tukiwaombea wachezaji na viongozi waliopata ajali wapate nafuu mapema.”

 

Share this: