USAJILI ni karata ambayo imekuwa ni pasua kichwa ndani ya timu mbalimbali kutokana na kile ambacho wanatarajia kukipata kutoka kwa wachezaji kukosekana na wakati mwingine wachezaji kufanya vizuri kisha kupata timu mpya ambazo zinahitaji huduma zao jambo linalopelekea kukutana na Thank You katika timu zao ambazo walikuwa wanazitumikia kusaka ushindi kwenye dakika 90 za kazi.
Ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 ulipogota mwisho kuna wachezaji wengi walikuwa wanatajwa kuondoka katika timu zao kupata changamoto mpya kwenye timu nyingine. Miongoni mwa wachezaji hao ni Aziz Ki mfungaji bora aliyetupia jumla ya mabao 21 ndani ya kikosi cha Yanga kinachodhaminiwa na SportPesa.

Mwisho hakutoa Thank You wala kukutana na Thank You aliongeza dili jipya hivyo bado yupo ndani ya Yanga huku ikitajwa kuwa anakunja mshahara mrefu zaidi ya milioni 24 kwa mwezi hiyo ni nje ya bonus ambazo atakuwa anakunja ndani ya kikosi hicho chenye maskani yake pale Jangwani wakiwa ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Ndani ya Bongo sio Simba, Yanga, Azam FC mpaka Geita Gold wamekuwa wakifanya sajili ambazo mwisho wa siku hazijawapa matokeo hivyo wachezaji wamekuwa wakikutana na Thank You kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa upande wa kikosi cha Simba kwa hivi karibuni kumekuwa na orodha ndefu ya wachezaji wanaosajiliwa kwenye kisha hawadumu ndani ya kikosi kutokana na sababu mbalimbali pengine kiwango kuwa cha chini kwa kutoa kile ambacho hawakufikiria na wakati mwingine benchi la ufundi kutokuwa na uhitaji wa mchezaji husika.
Hapa tunakuletea baadhi ya wachezaji ambao walikutana na Thank You ndani ya kikosi cha Simba namna hii:-
BABACARR SARR
Mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika ni 3 alikomba dakika 241 kwenye ligi ni mechi 13 akikomba dakika 822 alifunga bao moja raia huyu wa Senegal ilikuwa ni usajili wa mapema ndani ya Simba kwenye kuimarisha eneo la kiungo alishiriki Mapinduzi 2024.
PA JOBE

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mrithi wa mikoba ya Moses Phiri ni mechi mbili alicheza akikomba dakika 144 alifunga bao moja. Kwenye ligi ni mechi 16 alicheza alifunga bao moja akikomba dakika 533.
MICHAEL FRED
Mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/24 ni tatu akikomba dakika 30 uwanjani. Kwenye ligi alicheza jumla ya mechi 17 dakika 985 alifunga mabao 6 anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga kwa ajili ya kuanza changamoto mpya. Mshambuliaji huyo ameweka wazi kuwa kuna mengi alitarajia kufanya mwisho wa siku anaondoka katika timu hiyo.
“Mwanzo wa msimu nilikuwa nina amini kwamba kuna mengi ambayo tungefanya kwa kushirikiana na wachezaji wengine uwanjani ila mwisho wa siku sitakuwa ndani ya kikosi cha Simba. Ninawashukuru viongozi kwa muda ambao walinipa, mashabiki kwa namna ambavyo walikuwa pamoja nasi kwenye kila hatua hivyo tunaamini kwamba maisha yanaendelea na ninawashukuru sana.”
JEAN BALEKE

Msimu wa 2023/24 wakati anakutana na Thank You alifunga mabao 8 kwenye ligiĀ baada ya kucheza mechi 9 akikomba dakika 496 na mabao yake yote alitumia mguu wa kulia. Atakuwa ndani ya Yanga 2024/25. Msimu wa 2022/23 alicheza mechi 9 alikomba dakika 616 alifunga mabao 8 timu ya kwanza kufunga akiwa Bongo ni Dodoma Jiji dakika ya 45 alitumia pasi ya Kibu Dennis.
Baleke tayari amekamilisha masuala yote ya usajili ndani ya Yanga na mchezo wake wa kwanza wa ushindani kucheza ilikuwa dhidi ya CBE SA ya Ethiopia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na bao la ushindi katika mchezo huo lilifungwa na Prince Dube dakika ya 45.
SAIDO NTIBANZOKIZA

Kiungo mshambuliaji alikutana na Thank You 2023/24 alipogotea kufunga mabao 11 kwenye mechi 25 akikomba dakika 1870 katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni mechi 8 alicheza akikomba dakika 626. Msimu wake wa kwanza Simba ilikuwa ni 2022/23 akitokea Geita Gold. Jumla alifunga mabao 17, ni mabao manne alifunga akiwa ndani ya Geita Gold.Mechi 10 alizocheza Simba alikomba dakika 986.
SAWADOGO
Kiungo mkabaji Ismail Sawadogo aliibuka ndani ya Simba kwenye usajili wa dirisha dogo alikuwa anatajwa kuwa atafanya makubwa tofauti na matarajio ngoma ilikuwa nzito. Ni mechi tatu alicheza ndani ya Ligi Kuu Bara akikomba dakika 99 ndani ya msimu wa 2022/23 hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba msimu wa 2023/24.
MOHAMED MUSSA
Hakucheza mchezo hata mmoja wa ligi mshambuliaji huyu akakutana na Thank You.

