Kagoma YusuphKagoma Yusuph

 

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema kuwa watafanya kazi kubwa kutafuta matokeo kwenye mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Al Ahli Tripoli ndani ya dakika 90 unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa huku akibainisha kwama walishindwa kutengeneza nafasi za wazi kwenye mchezo wao uliopita ugenini.

Ikumbukwe kwamba Septemba 15 2024 ubao ulisoma Al Ahly Tripoli 0-0 Simba ambapo mchezo huo ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi. Timu zote ziliingia uwanjani kwa hesabu ya kusaka matokeo mwisho walitoshana nguvu.

Mchezo ujao wa kimataifa unatarajiwa kuchezwa Septemba 22 na tayari tiketi zimeanza kuuzwa kwa mashabiki wa Simba. Katika mchezo uliopita mpango mkubwa kwa Simba ulifanikiwa eneo la ulinzi kwa kuwa kipa Musa Camara alikuwa akifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na mabeki wote waliokuwa wakiongozwa na Che Malone.

REKODI YA SIMBA KIMATAIFA

Shomari
SHOMARI Kapombe kwenye majukumu kimataifa na uzi wa Simba 2024/25. Source: Simba.

Simba katika mechi za nyumbani kimataifa ilikuwa na rekodi nzuri ndani ya dakika 90 ambapo katika jumla ya mechi 6 sawa na dakika 540 kimataifa ni mchezo mmoja pekee Simba ilipoteza.

Mchezo iliopoteza ilikuwa zama za beki Pascal Wawa, Joash Onyango ambapo mabao matatu walifungwa na Jwaneg Galaxy kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakafungashiwa virago jumlajula katika anga la kimataifa.

Mechi nyingine ilikuwa Simba 3-1 Nkana, Simba 4-0 FC Platinum, Simba1-3 Jwaneng, Simba 3-0 Red Arrows, Simba 1-0 de Agosto, Simba 1-1 Power Dynamos na mchezo huu pekee walicheza Uwanja wa Azam Complex.

MWAMBA FADLU HUYU HAPA

Fadlu
FADLU Davids, Kocha Mkuu wa Simba 2024/25. Source: Simba.

Fadlu amebainisha kuwa walikuwa na kazi kubwa ugenini lakini hawakutengeneza nafasi nyingi za wazi jambo ambalo lilikuwa gumu kwao hivyo watafanyia kazi kwenye mchezo wa marudio wakiwa nyumbani kupata matokeo.

“Ulikuwa ni mchezo wenye ushindani kwa timu zote mbili hilo lipo wazi. Wachezaji walijitahidi kutimiza majukumu yao uwanjani lakini hatukutengeneza nafasi nyingi za wazi kwenye eneo la ufungaji.

“Hayo tumeyaona na tumefanyia kazi kwa kuwa tuna mchezo mwingine ambao tutacheza hivyo hapo tunaamini yale makosa yaliyopita tutafanyia kazi ili kupata matokeo mazuri. Ugenini wao walikuwa na mashabiki wengi waliokuwa wakishangilia kwenye mchezo huo nasi ni muda wetu mashabiki kujitokeza.”

WAMESHINDA KWENYE MASHABIKI

Mashabiki Simba
Mashabiki Simba wameitwa kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa, Septemba 22 2024. Source: Simba.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa kwenye upande wa matokeo uwanjani ni 0-0 ila kwa mashabiki wao wameshinda kwa kuwa walijitokeza wengi uwanjani.

“Kwenye mchezo wetu ugenini hakika kwa upande wa matokeo yatabaki kuwa 0-0 ila upande wa mashabiki wao wanaongoza. Walikuwa wengi mno uwanjani hasa ukiangalia na sisi ambao tulikuwa wachache kweli pale.

“Hatukuzudi 15 hapo ukiwahesabu na waandishi hivyo niliweka wazi kwa mashabiki wa Dar wao waongeze dua kwa ajili ya timu kupata matokeo na mwisho tulipata matokeo ambayo hayakuwa kwenye mpango wetu kwa kuwa ni ugenini haya ni matokeo mazuri vibaya mno.

“Kwenye mchezo wetu ambao tutakuwa Uwanja wa Mkapa ni muda wetu kuonyesha kwamba nasi tunaweza kushangalia na kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yetu kwani haya mashindano ni makubwa na ushindani ni mkubwa vibaya mno.

“Unajua kuna timu ambazo zinacheza mashindano mengi lakini hakuna mvuto huko waliko kumepoa kwelikweli, kikubwa kwenye mechi yetu ijayo ni mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuwapa nguvu wachezaji.”

NAHODHA HUYU HAPA ZIMBWE

Zimbwe Jr
Zimbwe Jr nahodha wa Simba 2024/25. Source: Simba.

Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein, Zimbwe Jr amebainisha kuwa wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo wao ujao kutokana na kushindwa kupata matokeo ugenini hivyo wajitokeze kwa wingi uwanja wa Mkapa kuwapa sapoti.

“Tulikuwa ugenini kazi imeisha sasa mchezo ujao tutakuwa nyumbani tunaamini kwamba utakuwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa lakini tupo tayari kwa ajili ya kupata ushindi kwani hili ni jambo kubwa.

“Mashabiki wamekuwa pamoja nasi kwenye mechi nyingi na katika mchezo wetu huu tunawaomba wajitokeze kwa wingi. Wachezaji tupo tayari na tunahitaji kupata matokeo katika mchezo wetu kufikia malego ambayo tunahitaji.”

MWAMBA KAPOMBE HUYU

Shomari Kapombe
Shomari Kapombe beki wa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu Fadlu Davids. Source: Simba.

Shomari Kapombe beki wa Simba amesema wanatambua umuhimu wa mchezo ujao wakiwa nyumbani watatumia mbinu watakazopewa na benchi la ufundi kupata matokeo mazuri uwanjani.

“Tuna kazi kubwa kwenye mchezo wetu ujao lakini tutakuwa nyumbani, tutafuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kupata matokeo mashabiki tunawaomba mjitokeze kwa wingi.”

Tayari kikosi cha Simba kimewasili Bongo baada ya kumaliza mchezo huo wakianza maandalizi kuelekea mchezo wa maamuzi unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili uwanjani.

 

Share this: