MABINGWA mara 30 ndani ya Ligi Kuu Bara wana kazi kubwa ndani ya Septemba kutokana na ratiba yao kuwa yamoto kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kuna mechi nne kali ambazo ni dakika 360 za kusaka ushindi uwanjani na jasho kwa wachezaji wa Yanga.
Tayari Yanga imecheza mchezo mmoja kwenye ligi ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaiataba baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kagera Sugar 0-2 Yanga na bao la kwanza likifungwa na Maxi Nzengeli. Ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 ni beki wa kazi Dickson Job yeye alifungua ukurasa wa mabao ndani ya Yanga na alifunga kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Katika mchezo huo wa kwanza wa Yanga kwenye ligi iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 ukiwa ni ushindi mkubwa kwa msimu wa 2023/24 ndani ya uwanja kwenye mechi za ushindani. Dozi hiyo ya Yanga haikukomea hapo kwani hata watani zao wa jadi Simba walikutana na kisanga hicho.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Yanga inayodhaminiwa na SportPesa baada ya dakika 90 ilishuhudia ubao ukisoma Simba 1-5 Yanga ambapo bao la Yanga la ufunguzi lilifungwa na Kennedy Musonda huku lile la Simba likifungwa na Kibu Dennis.
HUYU HAPA MAXI NZENGELI
Maxi Nzengeli kutoka kwa mabingwa watetezu yeye alikuwa na zali kwenye mechi za ushindani ndani ya uwanja akiwa ni mchezaji wa kwanza kufunga pia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali ilikuwa dhidi ya Simba alifunga bao hilo dakika ya 44 na kuwafungashia virago Simba katika kusaka tiketi ya kutinga fainali.
Taji la Ngao ya Jamii lipo mkononi mwa Yanga ilishinda mbele ya Azam FC iliyokuwa inanolewa na Yusuph Dabo ambaye alikutana na mkono wa Thank You kutoka kwa mabosi wa timu hiyo. Kwenye ligi Maxi alifunga bao la kwanza ilikuwa ni Agosti 29 2024 mabingwa hao watetezi walicheza mchezo wa kwanza wa ligi. Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi Maxi alianza kikosi cha kwanza na alipachika bao hilo akitumia pasi ya Pacome katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.
NENO LA MAXI

Kiungo huyo amesema: “Ninafurahi kufunga kwenye mechi ya kwanza ya ligi na mwisho timu kuchukua pointi tatu jambo ambalo ni la msingi. Tunaamini tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye mechi zetu kikubwa ni ushirikiano.”
KIKOSI CHA KWANZA CHA GAMONDI
Gamondi kwenye mchezo wa kwanza wa ligi akiwa ugenini alianza na Diarra wengi hupenda kumuita mdaka mishale langoni, Boka, Bakari Mwamnyeto ambaye ni nahodha, Dickson Job nahodha msaidizi, Bacca beki wa kazi chafu, Khalid Aucho, Maxi, Mudathir Yahya, Prince Dube, Aziz Ki na Pacome Zouzoua.
MZIZE NAYE YUMO

Bao la pili lilifungwa na Clement Mzize ambaye anaingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji mzawa wa kwanza kufunga ndani ya Yanga msimu wa 2024/25 akitokea benchi.
MAXI MPAKA ZAKIRAFIKI ANAPETA
Septemba 6 2024 Maxi alikuwa miongoni wa wachezaji waliocheza mchezo wa kirafiki, Uwanja wa KMC Complex dhidi ya Cosmopolitans FC huku Yanga ikishinda kwa mabao 2-0.
DAKIKA 360 ZAMOTO KWA MABINGWA
Timu hiyo kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya mchezo wa kimataifa dhidi ya Ethiopian Nigd Bank unaotarajiwa kuchezwa Septemba 14 2024 ambapo Yanga itakuwa ugenini.
Mchezo wa marudio unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa itakuwa ni Septemba 21 2024 ambapo mshindi wa jumla atasonga mbele katika hatua inayofuata.
Septemba 25 Yanga itakuwa na mchezo wa ligi dhidi ya Ken Gold itakuwa ugenini na mchezo wake wa kwanza ndani ya ligi kuwa nyumbani ni dhidi ya KMC itajuwa Septemba 29.
Ndani ha Septemba Yanga ina mechi nne za moto ambazo ni dakika 360 kwenye kusaka ushindi uwanjani. Mechi mbili ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi mbili itakuwa za Ligi Kuu Bara.
SEMAJI KAMWE HUYU HAPA

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema kuwa maandalizi yanahitajika kwenye kila idara ili kupata matokeo mazuri kutokana na ushindani uliopo na malengo ni kufanya vizuri kwenye mechi zote ambazo wanacheza.
“Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku tunakwenda kufanya kweli lakini kinachohitajika ni maandalizi, tunaamini kwamba ushindani ni mkubwa nasi tunafanya maandalizi mazuri ili kuwa imara uwanjani.”

