
Mara baada ya kuwepo kwa tetesi za muda mrefu juu ya uwezekano wa Azam kuvunja benchi lao la ufundi lililokuwa linaloongozwa na kocha mkuu Msenegal, Youssoupha Dabo, hatimaye rasmi leo Septemba 3, mwaka 2024 uongozi wa timu hiyo umetoa taarifa rasmi ya kusitisha mkataba wa kocha huyo.
Dabo anaondoka Azam akiwa ameiongoza timu hiyo katika kipindi cha miezi 15 tangu alipowasili Tanzania akitokea ndani ya kikosi cha ASC Jaraaf ya kwao Senegali. Dabo anaondoka na benchi lake lote la ufundi alilokuja nalo.
Uongozi wa Azam pia pia umetangaza kuwa kwa sasa program za timu hiyo zitakuwa chini ya makocha wa timu za vijana mpaka pale kocha mkuu mpya atakapotangazwa.
NINI KIMETOKEA?

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu wa Bodi ya Azam FC zimethibitisha kuwa, uamuzi huu unafuatia mwanzo mbaya wa msimu kwa Azam FC, ambapo licha ya ushindi mnono dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Nusu Fainali ya mashindano ya Ngao ya Jamii mwaka huu, walijikuta wakikubali kipigo cha mabao 4-1 walipokutana na Yanga ambao wanadhaminiwa na Kampumi ya michezo ya kubashiri ya SportPesa katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo.
Mara baada ya kupoteza mchezo wa fainali, Azam waliendelea na kibarua chao cha ushiriki wa mashindano ya kimataifa ambapo wakishiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam walijikuta wakiondoshwa kwenye hatua ya awali kwa matokeo ya jumla ya kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya APR, wakianza kwa ushindi wa 1-0 kwenye mchezo wa nyumbani kabla ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 ugenini nchini Rwanda.
Isivyo bahati kwa Azam wamekuwa na mwanzo wa kusuasua kwenye ligi baada ya kuanza kwa matokeo ya suluhu katika mchezo wao wa ufunguzi ambapo walivaana na JKT Tanzania. Kwa kiasi kikubwa matokeo hayo ndiyo kwa kiasi kikubwa yaliibua tetesi na kocha Dabo kuondolewa kazini.
AZAM WANASEMAJE?

Baada ya kuwa na mwanzo wa kusuasua kwenye Ligi msimu huu, uongozi wa Azam ulikiri ni matokeo ambayo hawakuyatarajia, lakini kwa kuwa bado ni mwanzo wa msimu wao kama kikosi wana nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko na kurejesha furaha ya ushindi kwenye michezo ijayo.
“Angalia vizuri msimamo hapo ndio kwanza tumecheza mechi ya kwanza na tuna alama moja. Bahati mbaya tumetoa suluhu ambayo hatukuitaka lakini tumeipokea japo kinyonge. Tunaendelea kujiimarisha vizuri, bahati nzuri ni kwamba ligi haijafika mbali msituchukulie poa wengi walitaka tupoteze watuzomee kama wafanyavyo katika hii sare ya leo. Hatukati tamaa, hatuchoki tutapambana na kurudi katika staili yetu ya uchezaji, kufunga mabao na kushinda mechi na furaha itarejea.
“Poleni mashabiki wetu kwa sare ushindi wa mpira mwingi unakuja siku sio nyingi, wala hamhitaji D 2 kuelewa aminini hili neno langu. Utamu waja.”
SIMBA WAITEKA SHOO YA MWEZI AGOSTI

Huku hali ikiwa tete kwa Azam FC, washindani wao kwenye kuisaka nafasi ya pili msimu uliopita Simba wameanza na moto wa hatari ambapo wameshinda ndani na nje ya uwanja.
Wakiwa kileleni na pointi zao 6 mara baada ya kucheza michezo 2, Simba wamepokea taarifa nyingine ya kujivunia hii ni baada ya kiungo wao wa kimataifa wa Ivory Coast, Jean Charles Ahoua mwenye umri wa miaka kufanikiwa kutajwa kama mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa mwezi Agosti, huku kocha wake, Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids akishinda Tuzo ya Kocha Bora.
Kwa pamoja, wawili hao, Fadlu na Ahoua wameisaidia Simba kukusanya pointi sita katika mechi mbili za mwanzo za msimu, wakiichapa Tabora United 3-0 katika mchezo wao wa ufunguzi, kabla ya kuishushia mvua ya mabao Fountain Gate kwenye mchezo wa pili ambapo walishinda kwa mabao 4-0. Michezo yote miwili ilichezwa kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Dar es Salaam.
Pamoja na hao kwa mwezi huo wa kwanza wa msimu, Ashraf Omar akibeba Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja kwa kazi yake nzuri Uwanja wa Meja Jenerali Mstaafu Isamuhyo, uliopo Mbweni Jijini Dar es Salaam.

