
Baada ya siku chache zilizopita kupitia jukwaa hili kuripoti kuwa taarifa kuhusu Simba kuwa kwenye mchakato wa kusaka straika mpya hatimaye taarifa hizo zimethibitishwa na kuelezwa straika huyo ni raia wa Cameroon na anatua leo Jumanne.
Zimesalia siku chache kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili na kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davis amekiri kuwa timu yao ipo katika mpango wa kusajili straika mpya wa kuiongezea nguvu.
Ikumbukwe kocha, Fadlu alizungumzia mahitaji ya kikosi chake kupitia kwenye mkutano na waandishi wa habari wa maandalizi ya mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ambao ulipigwa Jumapili iliyopita ambapo kocha huyo alikiri kuwa jambo hilo aliliweka wazi kwa viongozi wao kabla ya mchezo wa kilele cha Simba day tamasha ambalo limewahi kudhaminiwa na Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa wakati ikiwa mdhamini mkuu wa timu hiyo.
ALICHOSEMA KOCHA, FADLU
“Kabla ya mchezo wetu wa kilele cha siku ya Simba Day niliweka wazi kuwa bado tuna mahitaji kwenye eneo la ushambuliaji na tuna kazi ya kufanya.
“Nafurahia ubora wa kikosi nilichonacho, napewa sapoti kubwa kutoka kwa viongozi, najua wanafanya kazi kubwa nyuma ya pazia, tuna siku 5 kabla dirisha la usajili halijafungwa subiri tuone nini kitatokea.”
STRAIKA MCAMEROON ATUA
Taarifa za ‘kiintelijensia’ kutoka ndani ya Simba methibitisha kuwa timu hiyo tayari imemsainisha straika, Lionel Ateba aliyekuwa akikipiga USMA ya Algeria.
Akithibitisha taarifa hizo mchambuzi, Hans Raphael amechapisha andiko kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa instagram leo Jumanne akisema: “Muda huu Leonel Ateba yuko angani kuja Tanzania ila kuanza majukumu yake mapya na Simba. Ateba ataitumikia Simba kwa miaka miwili ijayo.”
Kwa taarifa hizi ni wazi muda wowote kutoka sasa Ateba atatambulishwa rasmi.
KAGOMA, MASHAKA KIMEELEWEKA, AWESU BADO KIZUNGUMKUTI

Wakati Simba wakiendelea na mchakato wa kumtangaza, Ateba ambaye anaelezwa kusaini mkataba wa miaka miwili imeelezwa kuwa pia wako katika hatua nzuri ya kumalizana na kesi zao tatu dhidi ya wachezaji wao, Yusuph Kagoma, Awesu Awesu na Valentino Mashaka ambao walikuwa na kesi za mapingamizi ya kuichezea timu hiyo kwa sababu mbalimbali.
KUHUSU KAGOMA, MASHAKA
Ikumbukwe kiungo, Yusuph Kagoma yeye aliwekewa pingamizi na Yanga ambao wanadai ni mchezaji wao kwa kuwa alisaini Yanga kabla ya kwenda kwa Wanamsimbazi, huku Mashaka ishu yake ikiwa ni Simba kumalizana na mchezaji bila kuihusisha klabu.
ALICHOSEMA MCHAMBUZI FARHAN JR

“Kwa mujibu wa vyanzo vyangu shauri la Yusuph Kagoma pale TFF ambapo Yanga walishtaki ni kuwa Mchezaji huyo amesaini timu mbili kati ya Yanga na Simba, hivyo adhabu ya ‘double signing’ ingekuwa ni kufungiwa kwa muda kujihusisha na soka.
“Upande wa utetezi wa Yusuph Kagoma ni kuwa ni kweli alisaini kandarasi na Yanga na klabu hiyo iliilipa Fountain Gate ada ya uhamisho ya Mchezaji huyo kutoka Kigoma.
“Lakini kwenye mkataba ambapo Kagoma alisaini na Yanga ambao wanadhaminiwa na Kampuni ya michezo ya kubashbiri ya SportPesa kulikuwa na suala la maslahi binafsi ambapo Yanga walipaswa kutekeleza ndani ya muda maalum na mkataba unakuwa halali punde baada ya mambo hayo kukamilika na kupandishwa kwenye mfumo.
“Taarifa kutoka kwenye vyanzo ni kuwa Yanga hawakutekeleza matakwa ya Mchezaji ndani ya muda hivyo mkataba ukafa kifo cha asili, ndipo Wanamsimbazi walipoingia wakipeleka dau kubwa zaidi Singida na maslahi mazuri zaidi kwa Mchezaji na nyota huyo akasaini Msimbazi.
“Fedha ambayo Yanga walishailipa kuelekea Fountain Gate kwa ajili ya Kagoma ndio ikabadilishwa na kuwa ndio ada ya uhamisho wa Mchezaji Aziz Andambwile ambaye kwasasa yupo Jangwani.
“Kwa maana hiyo Yusuph Kagoma ni Mchezaji halali wa Simba na hakupokea malipo yoyote kutoka kwa Yanga bali Yanga walifanya malipo kwa klabu yake ambapo kwakuwa wao ndio Wamiliki wa Mchezaji ndio waliofanya biashara na mabosi wa Msaimbazi ambayo ilikuwa kubwa zaidi.
“KAGOMA kwasasa ni Mchezaji halali wa Simba pamoja na VALENTINO MASHAKA, imesalia ya AWESU AWESU dhidi ya KMC ambapo majibu yake yanatarajiwa kutolewa hivi karibuni.”

