
VYUMA vya kazi vipo ndani ya Yanga tayari kwa msimu mpya wa 2024/25 unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote. Kwa sasa usajili unaendelea tambo zimekuwa haziishi kuhusu wachezaji wapya ambao wanatambulishwa na timu husika.
Ipo wazi kwamba Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi ni mabingwa watetezi kwa msimu ujao baada ya kutwaa taji la ligi msimu wa 2023/24.Ni pointi 80 Yanga ilikamilisha nazo baada ya mechi 30.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ipo sokoni na mchezaji wa kwanza kutambulishiwa ni Clatous Chama ilikuwa Julai Mosi 2024. Kiungo huyo mshambuliaji aliibuka ndani ya kikosi cha Gamondi akiwa mchezaji huru kwa kuwa mkataba wake na Simba ulikuwa umegota mwisho.
VYUMA VYA KAZI HIVI HAPA
Nyota wa kwanza kutambulishwa ndani ya Yanga kwa upande wa wale ambao waliongeza kandarasi mpya ni Farid Mussa. Julai Mosi alitambulishwa kuongeza kandarasi mpya kutoka 2024 mpaka 2026 hivyo bado ni Mwananchi.
DIARRA
Kipa Djigui Diarra maarufu kama mdaka mishale yeye Julai 5 mkataba wake uliongezwa. Ni kutoka 2024 mpaka 2027. Nyota huyo raia wa Mali ni chaguo la kwanza la Gamondi.
MWAMNYETO
Nahodha Bakari Mwamnyeto alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada ya timu mbalimbali Bongo ikiwa ni pamoja na Simba. Julai 3 alitangazwa kuongeza mkataba mwingine utakaomfaya awepo hapo mpaka 2026.
KIBABAGE
Julai 4 ilikuwa ni kwa Nickson Kibabage ambaye aliongezewa kandarasi nyingine.Kutoka 2024 yupo mpaka 2027 ndani ya kikosi hicho. Yeye ni mbavu ya kushoto.
MSHERY
Mlinda mlango Aboutwalib Mshery ambaye alisajiliwa na Yanga akitokea Mtibwa Sugar Julai 4 ilitangazwa kuwa bado ni njano na kijani baada ya kuongeza mkataba wake. kipa huyo ni mpaka 2027.
DUBE

Ule usiku wa kuamkia Julai 7 2024 ilitolewa zawadi ya 7/7 kwa mashabiki kwa utambulisho wa mshambuliaji Prince Dube kuwa ni mali ya Yanga.
Dube 2023/24 alikuwa akicheza ndani ya Azam FC alipovunja mkataba wake kwa makubaliano ya pande zote. Raia huyo wa Zimbabwe amesaini dili la miaka miwili kuitumikia timu ya Yanga.
BOKA
Beki wa kushoto kutoka FC Lupopo anaitwa Boka Chadrak alitambulishwa usiku wa kuamkia Julai 8. Anakuja kuwa mbadala wa Joyce Lomalisa ambaye hatakuwa ndani ya kikosi cha Yanga kwa msimu wa 2024/25 baada ya mkataba wake kugota mwisho.
KHOMEINY
Mwanzo wa siku mpya mapema kabisa ilikuwa Julai 8 2024 Yanga walimtambulisha kipa Aboubhakar Khomeiny ambaye msimu wa 2023/24 alikuwa ndani ya Ihefu.
KIBWANA
Kibwana Shomary beki wa kushoto yupo ndani ya Yanga baada ya mkataba wake kufanyiwa maboresho kutoka 2024 mpaka 2026 hivyo bado atazidi kuwa ndani ya Jangwani. Ilikuwa ni Julai 9 2024 alitambulishwa.
Beki huyo ameweka wazi kuwa wanatambua watakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwa msimu wa 2024/25 lakini wapo tayari kuwapa furaha Wananchi.
“Tuna kazi kubwa kufanya kwenye msimu mpya ambao utakuwa na ushindani mkubwa lakini tupo tayari kwa ushindani na malengo ni kuona tunawapa furaha Wananchi.”
ANDAMBWILE
Aziz Andambwile kiungo mkabaji ni ingizo jipya ndani ya Yanga aliibuka hapo akitokea kikosi cha Singida Black Stars. Ni Julai 9 alitambulishwa kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Gamondi.
VYUMA VILITIKISA
Aziz Ki, kiungo mshambuliaji namba moja kwa mabao msimu wa 2023/24 alitambulishwa Yanga kuwa bado yupo rasmi Julai 10 2024. Nyota huyo alifunga jumla ya mabao 21 akiwa namba moja kwa watupiaji Bongo. Alikuwa anatajwa kuw huenda angesepa katika kikosi cha Yanga ili kupata changamoto mpya mwisho kasalia kwa dili la miaka miwili.
Utambulisho wa chuma hiki ulitikisa kutokana na mvutano mkubwa ambao ulikuwa unatajwa hasa kwenye upande wa maslahi mwisho kabaki Yanga.
DUKE

Duke Abuya ni ingizo jipya ndani ya Yanga ambapo alitambulishwa rasmi kuwa Mwananchi Julai 12 2024 kutoka Singida Big Stars yeye ni kiungo mshambuliaji.
Abuya ana uwezo wa kupiga mapigo huru ikiwa ni pamoja na penalti, faulo. Spidi na maamuzi ya haraka ni miongoni mwa sifa ambazo anazo nyota huyo.
SEROTO
Chuma kingine cha kazi kilitambulishwa ndani ya Yanga huyu ni maalumu kwenye sekta ya afya. Sekhwela Seroto jina lake yeye ni mtaalam wa Tiba ya Viungo (Physiotherapist) raia wa Afrika Kusini atakuwa ndani ya Yanga.

