- Bonasi za ubingwa Ligi kuu, Kombe la shirikisho na robo fainali CAF msimu 2023/2024.
Kampuni ya burudani na michezo SportPesa leo imekabidhi mfano wa hundi ya shilingi Milioni 537.5 kwa timu ya Yanga, ikiwa ni bonasi na kufanya vizuri kwa msimu wa 2023/24.
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika kwenye ukumbi wa Urban City by Blue maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam, Waliohudhuria kutoka SportPesa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tarimba Abbas, Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Sabrina Msuya na kutoka Yanga ni Afisa mtendaji mkuu wa Yanga (CEO) Andre Mtine, Rais wa Klabu ya Yanga Eng. Hersi Said, benchi la ufundi, baadhi ya wachezaji Pamoja na waalikwa kutoka kampuni mbali mbali.

Akiwakaribisha waandishi wa Habari Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano SportPesa Sabrina H. Msuya aliwapongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa na kwa mafanikio waliyoyapata msimu huu, ambapo wameweza kushinda taji la ligi kuu bara NBC premier League, CRDB Federation Cup, na kuingia hatua ya robo fainali ligi ya mabingwa barani Africa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi SportPesa Tarimba Abbas alianza kwa kuwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Yanga kwa kulitwaa kombe hilo mara tatu mfululizo,
“SportPesa siku zote imekuwa ikijivunia mahusiano ya kiudhamini kati ya kampuni na Young Africans na hapajawahi kutokea muda tukajutia kwa sababu tumejihusisha na klabu ambayo inaendeshwa kiweledi. Hapa tungependa kupongeza uongozi unaoongozwa na raisi Eng. Hersi Said, uongozi ambao umeweza kujenga timu ambayo ni imara, aina ya wachezaji ambao inawasajili, benchi la ufundi kiasi kwamba Yanga imekuwa ni timu inayojitosheleza kwa ushindani wa aina katika bara la Afrika.
Ni jambo ambalo SportPesa tunaona tumefikia malengo yetu.
Kila tunachokiahidi kimkataba tumekitekeleza bila kuchelewa na Yanga inahitaji mdhamini wa sampuli kama SportPesa. Leo tumekabidhi mfano wa hundi ya shilingi 537.5M.”
Tarimba anaendelea kwa kusema “Tunaomba Yanga wasibweteke, waendelee kuboresha timu yao, kwani tunaona mwaka 2024/25 utakuwa ni mwaka wa ushindani sana.”
Akiongea kwa upande wa Yanga, Rais Eng, Hersi Said alianza kwa kushukuru SportPesa
Kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na klabu ya Yanga kama mdhamini mkuu katika kutekeleza mipango na majukumu ya kila siku.
“Nichukue nafasi hii kuishukuru Sportpesa kwa kutekeleza kwa wakati makubaliano yaliyopo kwenye mkataba kwa kutoa bonus ya Tsh 537,500,000 baada ya klabu yetu kutwaa ubingwa huu wa NBC Premier league na Kombe la Shirikisho.
Sisi kama Young Africans SC tumefurahi sana kupokea rasmi zawadi hii ya bonasi ambayo kimkataba kwa sisi kushinda Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na kufika hatua yar obo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabigwa Afrika.
Huu ni msimu wa tatu mfululizo tumekuwa tukichukua Ubingwa na kupata bonus hizi kutoka SportPesa.

Tulianza na kuingia robo fainali ya Kombe la shirikisho barani Africa, baada ya hapo tumechukua taji la ligi kuu Tanzania bara NBC premier League na mwisho tumechukua kombe la shirikisho, yaani CRDB Federation Cup.”
Akimalizia Hersi, amesema “tunawaahidi SportPesa kuwa tutaendela kujenga timu imara ya ushindani ndani na nje ya Tanzania ili kuitangaza zaidi Sportpesa ambaye ndiye mdhamini wetu mkuu”
