MZIZIMA DABI

 

Ngoma v Bangala
NYOTA wa Azam FC, Bangala na Ngoma wa Simba wakionyeshana ubabe kwenye moja ya mchezo wa ushindani. Source: Simba.

MZIZIMA Dabi Dar itazima kwa muda wababe 22 wakiwa mzigoni kwenye msako wa pointi tatu muhimu ndani ya uwanja kwa kila timu kuanza na wachezaji wake 11 kikosi cha kwanza kuvuja jasho la haki ndani ya dakika 90 kujua nani atakuwa mbabe kwenye mchezo huo.

Ni Mei 9 Uwanja wa Mkapa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Azam FC dhidi ya Simba unatarajiwa kuchezwa kwa kilatimu kupambania malengo yake kusaka ushindi uwanjani ikiwa ni mzunguko wa pili na kila timu inahitaji pointi tatu.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa mchezo huo kikubwa ni kupata pointi tatu huku Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba akibainisha kwamba bado hawajamaliza kazi inaendelea.

WAKALI WA MABAO HAWAPO

Chama
Chama Clatous, mwamba wa Lusaka kiungo mshambuliaji wa Simba akishangilia moja ya bao kwenye mchezo wa ushindani. Source: Simba.

Nyota waliofunga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba ilikuwa ni Simba 1-1 Azam FC kwa timu zote kugawana pointi mojamoja baada ya dakika 90.

Ni Clatous Chama alifunga bao kwa Simba, alifunga kwa pigo huru akiwa nje ya 18. Hatakuwa kwenye kikosi dhidi ya Azam FC kwa kuwa alifungiwa mechi tatu kwa kosa la kumchezea faulo Nickson Kibabage nyota wa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa katika Kariakoo Dabi.

Prince Dube mwenye zali la kufunga kwenye Mzizima Dabi yeye aliomba kuvunja mkataba na timu hiyo hivyo kwa sasa hayupo kambini kwenye kikosi cha matajiri wa Dar.

 

MWAMBA FEI AMEWAKA

Fei Toto
Fei Toto kiungo mshambuliaji wa Azam FC mwenye mabao 15 ndani ya ligi. Source: Azam FC.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum amewaka kutokana na kasi yake kwenye kucheka na nyavu akiwa ni namba moja kwa mastaa wote watakaokuwa kazini, Mei 9 2024 kwenye Mzizima Dabi.

Mabao 15 kafunga akitengeneza pasi sita za mabao hivyo kahusika kwenye mabao 12 ndani ya timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo. Bao la 15 alifunga kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Manungu, Morogoro.

 

DAKIKA 270 ZA MGUNDA NOMA

Mrithi wa mikoba ya Abdelhak Benchikha ndani ya kikosi cha Simba Juma Mgunda ameanza kwa mwendo mzuri kwenye mechi tatu ambazo amekaa kwenye benchi la ufundi kuwapa nondo  wachezaji wa timu hiyo.

Ikumbukwe kwamba Benchikha aliomba kuvunja mkataba wake na Simba kutokana na kile ambacho alieleza kuwa ni matatizo ya kifamilia  hivyo kwa sasa hayupo ndani ya timu hiyo.

Mchezo wa mwisho kwa kocha huyo kuiongoza Simba ndani ya ligi ilikuwa ni Kariakoo Dabi, Aprili 20 2024 na baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 2-1 Simba. Mabao ya Yanga  yalifungwa na Aziz KI na Joseph Guede na bao la Simba lilifungwa na Michael Fred.

Mgunda katika mechi tatu ambazo ni dakika 270 kwenye ligi ameshuhudia timu hiyo ikiambulia sare moja, ikishinda mechi mbili. Msako wa pointi tisa kakomba pointi saba akidondosha pointi mbili mbele ya Namungo, Uwanja wa Majaliwa.

Nyota Willy Onana anaingia kwenye orodha ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika mchezo dhidi ya Namungo alipoanza kikosi cha kwanza wakati kocha huyo akianza kazi na mfungaji wa bao la pili ni mwamba Edwin Balua.

Kete yake ya pili ilikuwa Uwanja wa Azam Complex ambapo walikuwa nyumbani na mchezo wa tatu pia Simba ilikuwa nyumbani dhidi ya Tabora United walipokomba pointi tatu mazima.

Pia ni mabao sita Simba imefunga katika mechi zote ilikuwa mwendo wa mbilimbili, Namungo 2-2 Simba, Simba 2-0 Mtibwa Sugar, Simba 2-0 Tabora United hivyo pointi mbili Simba ilidondosha ikiwa ugenini baada ya kugawana pointi mojamoja na Namungo.

USHAMBULIAJI AZAM FC BALAA

Kuelekea kwenye Mzizima Dabi, Azam FC wanabalaa kwenye eneo la ushambuliaji kutokana na kasi waliyonayo kwenye mechi wanazocheza na rekodi kuonekana kuwa upande wao mazima.

Safu ya ushambuliaji ya Azam FC imetupia jumla ya mabao 52 ikiwa ni namba mbili kwa timu zenye mabao mengi ndani ya msimu wa 2023/24. Namba moja kwenye utupiaji ni Yanga wenye mabao 56.

Azam FC inawakaribisha Simba ambayo ni namba tatu kwa timu zenye mabao mengi ambapo ni mabao 47 yamefungwa na timu hiyo ambayo kwenye msimamo ipo nafasi ya tatu.

 

ULINZI SIMBA TATIZO

Ulinzi ni tatizo kubwa kwa Simba ndani ya tatu bora ikiwa ni namba moja kwa timu iliyoruhusu mabao mengi kwa msimu wa 2023/24. Licha ya kucheza mechi 24 huku Yanga na Azam FC zikiwa zimecheza mechi 25 bado Simba ni namba moja katika kuruhusu mabao.

Ukuta wa Simba umeruhusu jumla ya mabao 23 wakikusanya pointi 53 kibindoni ndani ya ligi. Namba moja kwa kuruhusu mabao machache ni Yanga iliyokusanya jumla ya mabao 12 inafuatiwa na Azam FC iliyoruhusu mabao 16.

Kiujumla timu iliyoruhusu mabao mengi ndani ya ligi ni Mtibwa Sugar baada ya kucheza jumla ya mechi 25 ni mabao 43 timu hiyo imefungwa ikiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo.

 

Share this: