
KUELEKEA mchezo wao wa kesho Alhamisi dhidi ya Azam, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema baada ya ushindi wa mabao 2-0 tuliopata dhidi ya Tabora United wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mechi yao inayofuata dhidi ya Azam FC itakayopigwa kesho Alhamisi jinini Dar es Salaam.
Mgunda amesema mchezo wao dhidi ya Tabora United ulikuwa mgumu na walipata upinzani mkubwa, lakini mchezo huo umemalizika na wamerudi kambini kujiandaa na vita ya kusaka ushindi dhidi ya Azam FC.
Akizungumzia mchezo huo ambao Simba wanatarajiwa kuwa ugenini, Mgunda amesema: “Kila mchezo kwetu una maandalizi yake ya tofauti, hivyo mchezo uliopita dhidi ya Tabora United umeisha na tumerudi kambini kujiandaa kwa ajili ya mchezo wetu ujao dhidi ya Azam.
Akizungumzia mchezo wenyewe dhidi ya Azam, Mgunda amesema: “Hii ni mechi muhimu kwetu na kwa Azam kwa kuwa itaamua nani anatakiwa kukaa juu ya mwenzie, na huenda ikaamua vita ya mshindi wa pili msimu huu.
“Kitu kingine msisahau kuwa hii ni Dabi ambayo inatakutanisha timu bora ambazo zinapigania ubingwa, kwahiyo haiwezi kuwa rahisi lakini tumejipanga kwa ajili ya mchezo huo kuhakikisha tunaibuka na ushindi.”
KUHUSU MCHEZO DHIDI YA TABORA

Mgunda akiiongoza Simba kwenye mchezo wake wa tatu tangu akabidhiwe mikoba ya Benchikha wamefanikiwa kuzipata alama tatu za nyumbani dhidi ya Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi. Mchezo huo ulianza kwa kasi ya kawaida huku ukichezwa zaidi katikati ya uwanja mashambulizi yakiwa machache yaliyofika kwa walinda milango.
Sadio Kanoute wa Simba ndio alikuwa wa kwanza kuwainua mashabiki wa timu hiyo baada ya kuifungia bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 19, baada ya kumalizia mpira wa kona uliopigwa na Ladaki Chasambi.
Baada ya bao hilo Simba ya Mgunda waliongeza kasi ya kutafuta mabao mengine zaidi, lakini hata hivyo walipoteza umakini wa kuzitumia. Ni usajili wa dirisha dogo wa, Edwin Balua ndio uliowapatia Simba bao la pili dakika ya 76 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Mzamiru Yassin.
Ushindi huo uliifanya Simba kufikisha pointi 53 na kuendelea kusalia nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 24. Kikosi cha Simba ya Mgunda kwenye mchezo huo kilikuwa kama ifuatavyo; Lakred, Israel, Zimbwe Jr, Kennedy Che Malone, Ngoma (Hamis 86′), Balua (Karabaka 79′), Mzamiru, Freddy (Jobe 79′), Kanoute, Chasambi (Duchu 90+2), huku walioonyeshwa kadi akiwa ni Jobe 88′.
Kwa upande wa Tabora kikosi chao kilikuwa kama ifuatavyo; Noble, Maulid, Madirisha, Pemba, Bikoko, Milandu (Jarome 83′), Daniel (Nakibinge 53′), Najim, Okutu (Lembo 87′), Kalumba, Mbombo
ALICHOSEMA AHMED KUHUSU MASHABIKI KUISUSA TIMU

Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba ambao kwa sasa wapo chini ya Mgunda na wamewahi kulamba dili la Kampuni ya michezo ya SportPesa, Ahmed Ally kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram alielezea kile kinachoendelea kwa mashabiki wa timu hiyo ambao wanaonekana kama kususia timu kwa kusema: “Mashabiki wa Manchester United waliwapigia makofi wachezaji wao baada ya kufungwa bao 4-0 dhidi Crystal Palace. Mashabiki wameamua kusimama na Wachezaji wao katika kipindi hiki cha msoto
“Wamegundua kuwa hakuna mwingine wa kuwapigania zaidi yao, hivyo ni vyema kuwatia moyo baadala ya kuwakatisha tamaa kwa kuwatukana na kuwadhalilisha. Mashabiki wa United wanajua kwamba tukiwatisha tamaa wachezaji wetu timu itaporomoka zaidi kutoka nafasi ya 8 hadi ya chini zaidi.
“Hii ndio inapaswa kuwa ari ya Mashabiki hasa Mashabiki wa Simba, Sisi tunapaswa kuwa na moyo huo, mapenzi ya kweli ya timu hayapimwi kwa kiwango cha kutukutana Wachezaji au Viongozi, kuonesha kuwa una uchungu na timu sio lazima kudhihaki Wachezaji wako, uchungu ni kusimama na timu yako katika nyakati zote, Nyakati za furaha na nyakati za huzuni
KUHUSU TIMUATIMUA YA MAKOCHA

Ahmed pia ameongezea kuhusu uongozi wa Simba kukosolewa juu ya timuatimua ya makocha kwa kusema: “Simba miaka 7 Makocha 9, wapo wanaodhani kuwa huo ni uzembe wa viongozi na wengine tunadhani kuwa hatuapati mafanikio makubwa kwa sababu ya kubadilisha Makocha kila wakati.
“Kwanza lazima itambulike kuwa hakuna anaependa Kocha aondoke kwani suala la kutafuta kocha mpya pia ni changamoto sana, kila wakati kuanza upya. Al Ahly ndani ya kipindi cha miaka 10 yaani 2014 hadi 2024 Wamefukuza Makocha 12. Wydad katika kipindi cha miaka 11 yaani 2013-2024 wamefukuza Makocha 25.
“Raja Casablanca Kipindi cha Miaka 10 Wamefukuza Makocha 20, nimetoa mifano hiyo michache ili Wana Simba tujiridhishe kuwa si uzembe wa Viongozi wetu kuondoka au kufukuzwa kwa Walimu bali ni mazingira ya mpira wa Afrika, lakini pia hoja kubadilisha Makocha na Mafanikio haina uhalisia maana Al Ahly anabadilisha Makocha kila wakati na ndio kinara wa soka la Afrika.
“Ni Makocha wachache sana Afrika wanaodumu kwenye klabu moja kwa muda mrefu tena ni wale ambao timu zao hazina presha. Si jambo la kujivunia kuachana Makocha lakini huo ndio mpira wa Afrika. Muhimu kwetu Simba Sports ni kutengeneza misingi imara kama Al Ahly ambapo hata Mwalimu akiondoka kikosi kinabaki na ubora wake.”
