
KIUNGO wa kazi ngumu ndani ya kikosi cha Yanga kinachoongoza Ligi Kuu Bara baada ya kucheza jumla ya mechi 24 kikikomba pointi 62 kibindoni ameweka wazi kuwa kulikuwa na nafasi kubwa kwa timu hiyo kutinga hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ipo wazi kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ilifanya kazi kubwa ndani ya dakika 180 kwenye mechi kimataifa dhidi ya Mamelodi Sundowns mwisho iligotea hatua ya robo fainali kwa kufungashiwa virago. Ilikuwa ni changamoto ya penalti ambazo ziliwaondoa Yanga kimataifa.
Kwenye mechi zote mbili hatua ya robo fainali kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua hakuwa sehemu ya kikosi kilichocheza mechi zote mbili jambo ambalo amebainisha kwamba lilimpa maumivu makubwa ila hakuwa na jambo la kufanya.
Sababu kubwa ya kiungo huyo kukosekana kwenye mechi zote mbili ni kutokuwa fiti hivyo alikuwa anapambania hali yake kurejea kwenye ubora wake ambapo kwa sasa taratibu anazidi kuwa imara.
MKALI WA MABAO KIMATAIFA
Kimataifa kwenye hatua za makundi nyota huyo alitupia mabao matatu. Anashikilia rekodi ya kuwafunga Al Ahly Uwanja wa Mkapa bao ambalo linatajwa kuwa miongoni mwa mabao bora katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Pia katika hatua ya makundi, Al Ahly ilifungwa bao moja pekee nalo lilifungwa na mwamba Pacome kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa na baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 1-1 Al Ahly. Ikumbukwe kwamba tayari A Ahly ya Misri imetinga hatua ya nusu fainali.
Mabao mawili alifunga kwenye mchezo dhidi ya Medeama ya Ghana ilikuwa nje ndani, ugenini alifunga bao moja na walipokutana Uwanja wa Mkapa nyota huyo alifunga bao moja pia.
KWENYE LIGI MOTO

Katika Ligi Kuu Bara Pacome amehusika kwenye mabao 11, akifunga mabao 7 na kutengeneza pasi za mabao 4 baada ya kucheza jumla ya mechi 17 huku akikomba dakika 1,224.
Yanga ni namba moja kwa safu kali ya ushambuliaji msimu wa 2023/24 ikiwa imefunga jumla ya mabao 55 baada ya kucheza jumla ya mechi 24 amekosekana kwenye mechi 7 pekee ndani ya uwanja.
Mbali na kuwa Yanga inaongoza kwenye safu kali ya ushambuliaji pia ni namba moja kwenye timu iliyoruhusu mabao machache ambayo ni 12. Timu iliyoruhusu mabao mengi ni Mtibwa Sugar baada ya kucheza mechi 22.
HUYU HAPA PACOME
Nyota huyo amesema kuwa ni furaha kubwa kuwa ndani ya Yanga na aliumia kukosekana kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa lakini hakuwa na jambo la kufanya zaidi ya kuwafuatilia wachezaji wenzake uwanjani.
“Kwa maoni yangu naona kwamba tulikuwa tunastahili kucheza hatua ya nusu fainali Ligi ga Mabingwa Afrika lakini bahati haikuwa yetu kwa kuwa tulikosa matokeo.
“Niliumia kukosekana uwanjani ila nilifurahishwa na namna wachezaji walivyokuwa wakicheza katika kutimiza majukumu yao walifanya kazi kubwa katika kutafuta ushindi,”.
GUEDE GARI LIMEWAKA

Mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede gari limewaka kutokana na kasi yake kwenye kufunga katika mechi ngumu zenye ushindani mkubwa ndani ya uwanja.
Nyota huyo timu yake ya kwanza kuifunga katika ligi ilikuwa ni Singida Fountain Gate ambapo alifunga mabao mawili na aliwafunga Simba bao moja kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi Aprili 20 ubao wa Uwanja wa Mkapa uliposoma Yanga 2-1 Simba.
Wakati wakiwa kwenye msako wa pointi tatu dhidi ya Coastal Union mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Azam Complex alifunga bao pekee la ushindi lililopeleka pointi tatu Jangwani.
Bao pekee la ushindi la Guede lilifungwa dakika ya 76 lilitosha kuwatuliza Coastal Union iliyokuwa ikicheza kwa kujilinda mwanzo mwisho kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Nyota huyo amesema: “Furaha kubwa ni kuona kwamba tunapata matokeo kwenye mechi ambazo tunacheza hivyo kikubwa ni kuona kwamba tunapata pointi tatu hilo ni jambo kubwa na mechi zote tunacheza kwa kujituma.
“Ushindani ni mkubwa hilo lipo wazi nasi tunafanya kazi kubwa kuona kwamba mechi zetu tunafanya vizuri hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,”.

