Kazi-Kennedy JumaKennedy Juma
  • Kazi kubwa kufanyika kimataifa na wachezaji wa Simba kupata ushindi ugenini kimataifa
  • Bosi atembeza mkwara wa maana kwamba watafanya maajabu makubwa kweli
  • Maandalizi yameanza nchini Misri kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa shauku kubwa

KAZI kubwa inatarajiwa kufanyika ndani ya dakika 90 kwa mastaa wa Mnyama Simba kupata matokeo dhidi ya Al Ahly kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa robo fainali  wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa Aprili 5 2024 nchini Misri.

Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 0-1 Al Ahly hivyo kazi kubwa kwa Simba kutoka Tanzania ni kupambana kupata matokeo mazuri ugenini.

Hesabu kubwa za Simba ni kutinga hatua ya nusu fainali hivyo li hayo yatimie hakuna changuo lingine ni kushinda mabao zaidi ya mawili katika mchezo huo unaosubiriwa kwa shauku kubwa.

KAZI IMEANZA MISRI

Fred Michael
Fred Michael mshambuliaji wa Simba akiwa kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo dhidi ya Al Ahly, nchini Misri. Source: Simba

Mastaa wa Simba ikiwa ni pamoja na Henock Inonga, Ayoub Lakred, Clatous Chama, Fred Michael, Ally Salim, Kibu Dennis wapo nchini Misri kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.

Mapema Aprili 3 msafara wa Simba uliwasili salama nchini Misri na kuanza mazoezi mepesi chini ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha ambaye anaamini kwamba kuna matumaini ya kupata ushindi.

Kocha huyo amebainisha kuwa ushindani kimataifa ni mkubwa na wanatambua aina ya timu ambayo wanakutana nayo hivyo watajitahidi kupata matokeo.

“Tupo kwenye ushindani mkubwa ukizingatia hii ni Ligi ya Mabingwa Afrika kila mchezaji anatambua, makosa yaliyopita tutayafanyia kazi ili kuwa bora mbele ya wapinzani wetu Al Ahly.

“Wachezaji wapo tayari na wanatimiza majukumu yao hivyo ni suala la kusubiri muda na tunaamini tutakuwa na mchezo mzuri tukiwa ugenini,”.

HAPA NDIPO TATIZO LILIANZIA

Kennedy Juma
Kennedy Juma beki wa Simba pamoja na wachezaji wengine wakiwa kwenye mazoezi. Source: Simba

Simba hesabu zao ilikuwa kumaliza mchezo Uwanja wa Mkapa Machi 29 lakini ngoma ilikuwa nzito kwa kuwa nafasi walizotengeneza walikwama kuzitumia kwa umakini huku safu ya ulinzi ikiruhusu bao la mapema kwenye mchezo huo dakika ya 5.

Hapo ndipo ambapo tatizo lilianzia na kufanya kazi iwe kubwa kuelekeamchezo wa mkondo wa pili lakini wakiongeza umakini waa nafasi ya kupata matokeo licha ya kwamba wapinzani wao nao wanahitaji matokeo pia.

Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Mkapa wachezaji wa Simba walitengeneza nafasi nyingi zaidi kuliko Al Ahly katika mchezo huo.

Mashuti 20 yalipigwa kuelekea lango la Al Ahly ya Misri na 7 yalilenga lango lakini uimara wa kipa wa Al Ahly uliwapa tabu Simba kupata ushindi huku Al Ahll wao ni mashuti 7 walipiga lango la Simba mawili yalilenga lango na moja lilizama nyavuni baada ya kumshinda mlinda mlango Ayoub Lakred.

HUYU HAPA AHMED ALLY

Ahmed Ally
Ahmed Ally Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba akitoa ufafanuzi kwenye moja ya mkutano na Waandishi wa Habari na Wanasimba. Source: Simba

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa wanatambua namna ushindani ulivyo kimataifa lakini watafanya yale ambayo hayafikiriwi imani kubwa ni kupata ushindi.

Ally ameongeza kuwa nguvu ya mashabiki ni kubwa na wanatambua mchango wao hivyo wanapaswa kuendelea kila wakati bila kukata tamaa makosa yatafanyiwa kazi.

“Kweli tulikuwa na mchezo mzuri nyumbani lakini hatukupata matokeo hilo lipo wazi kabisa. Kupoteza mchezo wetu dhidi ya Al Ahly imetuumiza kwa kuwa ukweli ni kwamba tulikuwa na siku bora kwenye aina ya uchezaji na tulipata nafasi nyingi lakini hatukuzitumia lakini haina maana kwamba kazi imefika mwisho tunakwenda kufanya yale ambayo wanaamini hayawezekani.

“Sisi tunaweza na tunaamini wengi wanadhani kazi yetu imefika mwisho ila ukweli ni kwamba bado tupo imara na tunakwenda kufanya kazi kubwa kwa ajili ya kutafuta matokeo ugenini kila kitu kinawezekana.

“Yale ambayo wanaamini hayawezekani hayo tunakwenda kufanya maajabu makubwa kwenye ulimwengu wa mpira na tunaweza kwa kuwa wachezaji wapo tayari,”.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Aprili 5 Ijumaa baada ya dakika 90 itafahamika nani atasonga hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa dakika 90 za awali ni Al Ahly walikuwa wababe wakiwa wametanguliza mguu mmoja hatua ya nusu fainali mabingwa hao watetezi.

 

Share this: