- Tuzo zinapigiwa hesabu ndefu kwelikweli ndani ya Ligi Kuu Bara 2023/24
- Yanga na Azam FC vita ni kali kwenye tuzo ya ufungaji bora ndani ya ligi na ubingwa
- Simba wanajitafuta mdogomdogo huko walipo kupindua meza kibabe
NGOMA ni nzito ndani ya Ligi Kuu Bara kutokana na kila timu kupambana kufanya vizuri msimu wa 2023/24 ambapo kila idara zinafanya kazi kubwa kusaka matokeo uwanjani kwenye dakika 90 za ushindani. Wakati hayo yakiendelea pia kwa upande wa tuzo vita ni kali kwelikweli kwa wachezaji binafsi pamoja na timu.
Ipo wazi kwamba mwisho wa msimu huwa kunakuwa na tuzo ambazo hutolewa kwa wachezaji pamoja na timu hivyo mapambano yanaendelea kwa kila mmoja kupambania upande wake na mwisho kila kitu kitakuwa wazi.
Kwenye upande wa kiatu cha ufungaji bora timu ambazo zipo ndani ya tatu bora kila mchezaji anapambania kombe kuona kipi atakipata ambapo kwa sasa ni mzunguko wa pili ligi inakaribia kufika ukingoni. Timu nyingi zimebakiwa na mechi 12 na zipo zilizobakiwa na mechi 10 na 9 hivyo bado kidogo itafahamika.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa wachezaji wake wengi wamekuwa kwenye rekodi zinazopendeza huku wao wakiweka wazi kuwa malengo makubwa sio kutwaa tuzo bali kuona wanatetea taji la ubingwa ambalo lipo kwenye mikono yao.
FEISAL WAMOTO

Kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Machi 17 kiungo Fei Toto alikuwa wa moto kutokana na kufanya kazi kubwa ndani ya dakika 90 ambazo alipewa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo.
Ni miguso 28 ilikuwa kwenye mguu wake huku ule wa kulia ukiwa na nguvu zaidi na alipiga mashuti mawili yaliyolenga lango la wapinzani wao Yanga katika msako wa pointi tatu.
Shuti moja kipa Diarra aliokoa na kulifanya lango la Yanga kuwa salama huku Azam FC wakikosa kupata bao kupitia jaribio hilo ambalo lilikuwa na hatari kubwa kama lisingeokolewa na kipa wa Yanga.
Jaribio lake la pili kuelekea lango la Yanga lilikuwa ni hatari kwa wapinzani wao Yanga kwa kuwa lilizama mazima nyavuni kwa kipa kukwama kuokoa hatari hiyo.
Ikumbukwe kwamba hatari hiyo ya pili ilikuwa dakika ya 51 likiwa ni bao lake la kwanza kuwafunga mabosi wake wa zamani Yanga kwenye mechi za ushindani kwa kuwa jitihada zake kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza hazikuwa na faida zaidi waliishia kupoteza mchezo ule.
Ni mara nne alikuwa ndani ya 18 akiwa na miguso ya mpira huku hata bao lile la kwanza lililofungwa na Gibril Silla mguu wake wa kulia ulihusika kwenye kutoa pasi iliyokwenda kuleta bao la kusawazisha kwa Azam FC.
KAMBANI NI 13 FEI TOTO
Mzawa Feisal anakuwa ni namba moja kwa nyota wenye mabao mengi ndani ya kikosi cha Azam FC akiwa kafikisha jumla ya mabao 13 ambayo ni mengi kwake ndani ya msimu wake wa kwanza akiwa Azam FC.
Kwenye ligi wapo sawa na kiungo wa Yanga, Aziz KI ambaye naye katupia jumla ya mabao 13 msimu wa 2023/24 ikiwa kila mmoja yupo kwenye ubora wake katika kutimiza majukumu yake.
Safu ya Azam FC kwenye upande wa ushambuliaji ni namba mbili ndani ya timu ambazo zipo tatu bora ikiwa imefunga jumla ya mabao 47 baada ya kucheza jumla ya mechi 21.
Mbali na kuwa na mabao 47 pia timu hiyo imekusanya pointi 47 kwenye msimamo ikiwa namba mbili msimu wa 2023/24 ambao ushindani ni mkubwa tofauti yake na vinara wa ligi ambao ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ni pointi tano pekee.
Wakati Azam FC ikiwa nafasi ya pili na mabao yake 47 Yanga wao wapo nafasi ya kwanza wakiwa wamecheza jumla ya mechi 20 pekee kete 10 zimebaki kukamilisha mzunguko wa pili.
AZIZ KI HAYUPO MBALI NA MWENDO WA NGOMA

Ndani ya Yanga namba moja kwa utupiaji ni Aziz KI akiwa na mabao 13 kwenye ligi.Nyota huyu ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu Miguel Gamondi hayupo mbali kwenye suala la kufunga mabao.
Ikumbukwe kwamba katika mabao hayo 13 aliyonayo aliwafunga mzunguko wa kwanza mabao matatu ikiwa ni hat trik na akasepa na mpira wake baada ya dakika 90 kukamilika.
Kwenye Mzizima Dabi Machi 17 wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Azam FC 2-1 Yanga alianza kikosi cha kwanza lakini alikwama kufunga zaidi ya kutoa pasi ya bao kwa Clement Mzize ambaye alifunga bao la mapema dakika ya 10 katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Yanga ni namba moja kwa safu ya ushambuliaji yenye mabao mengi ikiwa na jumla ya mabao 49 baada ya kucheza mechi 20 huku Aziz raia wa Burkina Faso akiwa ametupia jumla ya mabao 13.
SIMBA WANAPAMBANA KUIPIGA NGOMA

Ndani ya kikosi cha Simba kinara wa utupiaji ni Jean Baleke ambaye kwa sasa hayupo na timu baada ya kupewa mkono wa asante hivyo ngoma ni nzito kwa kuwa hataweza kuongeza mabao mengine zaidi yatabaki hayo daima mpaka apatikane nyota mwingine wa Simba.
Saido Ntibanzokiza ni yeye amebaki kuwa namba moja kwenye upande wa safu ya ushambuliaji akiwa na mabao 7 anafuatiwa na Clatous Chama mwenye mabao sita ndani ya ligi hawa wote ni viungo washambuliaji.
Simba kwenye msimamo ni namba tatu ikiwa na pointi 45 baada ya kucheza jumla ya mechi 19 safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao 39 ikiwa ni namba tatu kwa timu zilizofunga mabao mengi ndani ya tatu bora.
