YANGA yapiga hesabu robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kupata matokeo chanya uwanjani

Kwenye ligi kasi ya Aziz KI kwenye utupiaji yazidi kushika kasi akiwapa tabu makipa

Okra Magic kaanza kufanya kweli ndani ya uwanja ikiwa ni ingizo jipya

BENCHI la ufundi la Yanga limeweka wazi kuwa hesabu kubwa ni kufanya vizuri kwenye mechi za kitaifa na kimataifa kutokana na maandalizi ambayo wanayafanya ndani ya uwanja kila wakati msimu wa 2023/24.

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga akiwa kwenye moja ya mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya mechi. :Source Yanga
Gamod

Ikumbukwe kwamba Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi raia wa Argentina ni mabingwa watetezi wa ligi wanadhaminiwa na Kampuni ya SportPesa.

Mchezo wao uliopita dhidi ya Geita Gold walipata ushindi wa bao 1-0 lilifungwa na Aziz KI ambaye alitumia pasi ya mwamba Okra Magic kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complexx.

LIGI YA MABINGWA KUNA KAZI

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya robo fainali Yanga  ina kazi ya kusaka ushindi dhidi ya Mamelod Sundowns kutoka Afrika Kusini mchezo unaotarajiwa kuchezwa kati ya Machi 29-31 Uwanja wa Mkapa.

Ikumbukwe kwamba Mamelod ilimaliza ikiwa namba moja kundi A baada ya kukusanya pointi 13 ilipocheza mechi 6 inatarajiwa kumenyana na Yanga iliyomaliza nafasi ya pili kundi D na pointi 8.

Mchezo wa mkondo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa kati ya Machi 29-31 na ule wa marudiano itakuwa kati ya Aprili 5-7 2024 ambapo Yanga itaanzia nyumbani pale Uwanja wa Mkapa, Dar.

HUYU HAPA SKUDU

Skudu Makudubela kiungo wa Yanga akiwa kwenye moja ya maandalizi ya mchezo wa ushindani. :Source Yanga
Skudu —

Skudu Makudubela kiungo wa Yanga ameweka wazi kuwa wanatambua namna ushindani ulivyo ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini wanaamini maandalizi mazuri yatawapa matokeo chanya.

“Ushindani ni mkubwa kwa kuwa tupo hapa kwenye hatua ya robo fainali tutapambana kufanya vizuri na kupata matokeo mazuri, inawezekana kutokana na maandalizi mazuri kwenye kila mchezo.

“Kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo wetu dhidi ya Mamelod haitakuwa kazi nyepesi lakini tupo tayari na tunaamini kwamba tutapata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu,’.

GAMONDI HUYU HAPA

Gamondi amesema kuwa kazi kubwa kwenye mechi zote wanazocheza ni kutafuta ushindi na hilo linaanzia kwenye uwanja wa mazoezi kwa wachezaji kupewa mbinu na kuboresha makosa katika mechi zao.

“Kwenye mechi zetu tunatazama makosa yetu na kuyafanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi tunatambua kazi ni kubwa na malengo yetu ni kuwa kwenye mwendelezo mzuri.

“Mashabiki wanapenda burudani hilo tunatambua nasi tunafanya maandalizi kwa ajili ya mechi zetu zote na inawezekana kupata matokeo mazuri,”.

AZIZ KI KAWAKA HUKO

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga Aziz KI akishangilia moja ya bao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold uliochezwa Uwanja wa Azam Complex: Source Yanga
Aziz Geita

Aziz KI kasi yake ya kucheka na nyavu imezidi kuwa bora akiwa ni kiungo mshambuliaji namba moja kwenye chati ya wafungaji ndani ya Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo amekuwa na mwendelezo bora katika kufunga na kutoa pasi za mabao akiwa kafikisha jumla ya mabao 13 na pasi za mabao alizotoa ni sita kwenye ligi.

Ipo wazi kwamba kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Ihefu uliochezwa Uwanja wa Azam Complex wakati ubao ukisoma Yanga 5-0 Ihefu alitoa hat trick ya pasi na kufunga bao moja hivyo alihusika kwenye mabao manne kati ya matano.

Bao lake la 13 alifunga kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Geita Gold uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ilikuwa Machi 14 dakika ya 28 akitumia krosi ya Okra Magic ambaye anatoa pasi yake ya kwanza kwenye ligi msimu wa 2023/24 akiwa na uzi wa Yanga.

KI kahusika kwenye mabao 19 kati ya 48 yaliyofungwa na Yanga akiwa kafunga 13 na kutengeneza pasi za mabao 6 msimu wa 2023/24 kwenye ligi.

Kiungo huyo ameweka wazi kuwa wanatambua ushindani uliopo kwenye mechi zote wanazocheza kikubwa ni kuwa kwenye mwendelezo mzuri na kupata matokeo chanya.

“Kila mchezo kwetu tunatambua ni muhimu kupata matokeo hivyo ambacho tunakifanya ni kushirikiana na wachezaji pamoja na benchi la ufundi kuona namna gani tunapata matokeo mazuri kwenye mchezo husika.

“Mashabiki wanatuongezea nguvu kwenye mechi ambazo tunacheza na tunaamini kwamba bado tuna kazi ya kufanya katika mechi zetu zinazofuata hilo lipo wazi,”.

Baada ya kucheza jumla ya mechi 19 Yanga imekusanya pointi 52 ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo mchezo ujao ni dhidi ya Azam FC unatarajiwa kuchezwa Machi 17 Uwanja wa Mkapa.

Share this: