YangaYangaRivers

Huenda timu ya Wananchi Yanga, siku ya kesho ikaandika rekodi ya kufuzu hatua ya nusu fainali katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, iwapo itakamilisha kazi waliyoianza wiki iliyopita nchini Nigeria.

Mechi hiyo ya mzunguko wa pili, yaani marudiano inachezwa jijini Dar-Es-Salaam, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya mechi ya kwanza ya robo fainali ya kombe la shirikisho iliyopigwa katika dimba la Godwill Akpabio Jijini Uyo nchini Nigeria, ambapo yanga walishinda kwa magoli 2-0.

Ushindi huo umewafanya Wananchi watangulize mguu mmoja ndani kucheza nusu fainali na sasa wanahitaji sare ya aina yoyote au kama ni kupoteza basi iwe ni kwa tofauti ya bao moja na hapo watakuwa wameandikisha historia hiyo kwenye soka la Tanzania kwakuwa timu ya kwanza kufikia hatua hiyo tangu tuanze Karne ya 21.

Ikumbukwe rekodi za hivi karibuni kwa timu za Tanzania katika hatua kama hii inashikiliwa na wekundu wa Msimbazi Simba, ambao walitinga robo fainali ya michuano ya CAF mara 4, huku mara tatu zote zikiwa ni za Klabu bingwa lakini Simba hawajawahi kufika nusu fainali, hivyo Yanga wanataka kuweka rekodi hiyo tena ndani ya kipindi kifupi cha ujenzi wa timu yao.

Siri kubwa ya matokeo ya mchezo wa mkondo wa kwanza ni kucheza kwa nidhamu ambapo Kocha Nasreddine Nabi aliamua kuanza na mabeki watano ambao ni Bakari Mwamnyeto,Dickson Job, Ibrahim Bacca,Djuma Shaban na Joyce Lomalisa ambao walitengeneza ukuta mgumu uliowafanya Rivers United kukosa hata nafasi ya kupiga shuti lililolenga lango la Yanga.

Nabi alianza na mfumo wa 3-5-2 ikimaanisha walikuwa na idadi kubwa ya wachezaji wakati wa kujilinda.

Lakini kama haitoshi baada ya zoezi la kuwadhibiti washambuliaji wa Rivers akiwemo aliyekuwa kinara wa kucheka na nyavu wao Paul Acqua, mwenye mabao (4) kukamilika, Kocha Nabi alibadili mpango wake wa awali, kwa kuwaondoa mabeki Djuma Shaban, Joyce Lomalisa na Farid Mussa na kuwaingiza Kibwana Shomari, Jesus Moloko na Tuisila Kisinda.

Nabi alitambulisha mfumo wa 4-4-2 ambao ulidhihirisha kwamba Yanga walitaka kupata mabao, kwani waliongeza idadi ya wachezaji mbele wakiwa wanashambulia na kuwa watu 8 tofauti na mwanzo.

Matunda ya mabadiliko hayo ya wachezaji na kimfumo yalizaa matunda ambapo, mshambuliaji Fiston Mayele akacheka na nyavu mara 2 dakika za 73 na 81, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Bakari Mwamnyeto na Jesus Moloko katika nyakati mbili tofauti, ambazo hazikupishana muda sana.

Rivers wakapoteza mchezo kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya CAF msimu huu kwenye dimba lao la nyumbani, huku Yanga wakipata ushindi wa pili ugenini baada ya awali kuifunga TP Mazembe hatua ya makundi.

.Ulikuwa ushindi ambao una sababu za ubora maana takwimu zinaonyesha licha ya Rivers United kumiliki mchezo kwa asilimia 56 dhidi ya 44 za Yanga lakini wenyeji walizidiwa katika maeneo mengi,mfano Yanga ilipiga mashuti 9 yaliyolenga lango wakati wenyeji hawakupiga hata moja.

Vijana wa Jangwani walipiga mashuti matatu ambayo hayakulenga lango wakati The Pride of Rivers walipiga 6, unapata taswira wenyeji hawakuwa na shabaha.

Rivers ndio waliozuia mashuti mengi kutoka kwa Yanga waliopiga mara 6 wakati Yanga walizuia matatu tu ya Rivers.

Kipa wa Yanga ,Djiguir Diarra hakuokoa hatari yoyote kutoka kwa Rivers wakati kipa wa Rivers United aliokoa mashuti 7 kutoka kwa Wananchi,tafsiri yake Yanga walikuwa hatari zaidi kwenye eneo la kushambulia na walihitaji mabao.

Eneo pekee ambalo Yanga walizidiwa kwa takwimu ni kona ambao wao walipata 2 tu wakati Rivers walimaliza mchezo wakiwa na kona 7.

Hizi takwimu zinasaidia kufanya tathmini kuelekea mchezo wa marudiano ambazo Makocha wote watazitumia kurekebisha makosa ya mchezo uliopita.

Kocha wa Rivers United Stanley Eguna alisema wao watajaribu kurekebisha makosa ambayo wameyafanya na kuwagharimu kufungwa nyumbani na Yanga katika mchezo wa kwanza.

“Tutacheza mechi ya marudiano na mkakati mwingine, japo sitauweka hadharani kwa sasa. Nimeiona Yanga imeimarika tofauti na tulivyocheza nao mara ya mwisho tulipokutana.

Yanga vs RiversNimejaribu kuwafuatilia na najua kwamba mpaka kufika hatua hii ya kukutana na sisi waliongoza kwenye makundi, wanaongoza Ligi yao ya Tanzania,na wametufunga.

Kwa sasa nina kazi kubwa ya kurekebisha timu kimbinu kwakuwa tunahitaji kufuzu na hilo linawezekana”. Alisema Eguna.

Naye Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi alisema baada ya mechi ya kwanza na Rivers kwamba hawakutegemea kuifunga bao mbili ingawaje kwenye mpira lolote linaweza kutokea.

“Imekuwa kama mshtuko kuona tunaifunga Rivers nyumbani kwao kwakuwa haikuwa rahisi, ingawa nilisema sisi hatukwenda Nigeria kulipa kisasi bali kusaka nafasi ya kufuzu.

Bado mechi haijaisha ninawajua wachezaji wa Nigeria ni wapambanaji sana, tutajipanga zaidi kwa ajili ya mechi ya marudiano kwakuwa kazi bado haijaisha”

Yanga walitupwa nje na Rivers kwenye hatua ya mtoano kufuzu makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika msimu wa 2020/21 tena kwa kipigo cha michezo miwili ya nyumbani na ugenini hivyo iwapo wataifunga tena kwa Mkapa Jumapili hii watakuwa wamelipa kisasi.

Eneo pekee la kuzingatia ni kwamba ushindi wa 2-0 ni mkubwa lakini ni mdogo kutokana na tabia za mpira wa miguu iwapo hautoheshimiwa kwa maandalizi.

Inakumbukwa namna watani wa Yanga, nazungumzia Simba ambao msimu wa 2020/21 walivyotupwa nje na Jwaneng Galaxy ya Botswa kwenye hatua ya mwisho kufuzu makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Oktoba 17,201, Simba ilishinda bao 2-0 nchini Botswana na mnamo Oktoba 21,2021, licha ya Simba kutangulia kwa bao la Bernard Morrison,lakini Galaxy walisawazisha kipindi cha pili na kufunga mabao mengine mawili kisha wakafuzu kwa kanuni ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla ilikuwa sare ya 3-3.

Wananchi wana faida kwani katika msimu huu haijapoteza mchezo kwenye dimba la Mkapa lakini ilitoka sare michezo miwili dhidi ya Al Hilal ya Sudan na Club Africain ya Tunisia.

Mechi nyingine zote wameshinda tena kwa idadi ya mabao kuanzia mawili na kuendelea swali linasalia je Wananchi wataweza kuikamilisha safari waliyoianza kwa natumaini?

Share this: