- Simba SC ina rekodi mbaya dhidi ya RS Berkane kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza ugenini.
- RS Berkane wapo tayari ndani ya ardhi ya Tanzania kupambana kwenye dakika 90 za jasho uwanjani.
- Ahmed Ally Meneja wa idara ya Habari Simba SC ametoa onyo kali kwa wataowavurugia mipango yao ya kutwaa ubingwa wa Afrika.
Simba SC vs RS Berkane vita ya wababe wawili Uwanja wa Amaan Complex Mei 25 2025 kusaka bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kazi joto linazidi kupanda huku mzigo ukiwa ni kwa Simba SC kupata mabao 3-0 ili kutwaa taji hilo ikiwa tofauti wapinzani wao watatwaa taji hilo kwa kuwa kwenye mchezo wa kwanza walipata ushindi RS Berkane.

Ikumbukwe kwamba katika mchezo wa fainali ya kwanza iliyochezwa Mei 17 2025 baada ya dakika 90 nchini Morocco, ubao ulisoma RS Berkane 2-0 Simba SC. RS Berkane wana faida ya mabao mawili waliyopata kwenye mchezo wa kwanza hivyo katika mchezo wa pili wanahitaji sare ikiwa itakuwa hivyo basi watabeba taji hilo.
Tayari wachezaji wa Simba SC chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids wapo Zanzibar kwa maandalizi ya mwisho kwenye mchezo huo ambao mgeni maalum atakuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.
Inahusiana na hii:Hamza arejesha mzuka Simba SC vs RS Berkane 25/05/2025
Simba SC yapania kufanya maajabu
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa wanatambua mchezo wao utakuwa ni mgumu lakini wapo tayari kufanya maajabu ili kutwaa ubingwa wa Afrika.

“Simba tumeshafanya maajabu mengi sana acha ya zamani. Msimu huu kila aliyetufunga na sisi tulimfunga. RS Berkane ameshamaliza zamu yake sasa ni zamu yetu. Hatuzungumzi haya sababu ya historia bali ubora ambao tupo nao.
“Tunakubali Benjamin Mkapa ndio ngome yetu lakini hatushindi sababu ya uwanja, tunashinda sababu ya ubora wetu. Uwanja wa Amaan ndio ulitupeleka fainali na sasa ndio utatupa ubingwa. Hatumaliza deni na hayati Rais Mwinyi na sasa tunakwenda kulipa deni mbele ya mtoto wake, Rais Dkt. Hussein Mwinyi. Tunataka kulipa hili deni.
“Tunafahamu kuna watu wanafanya kila hila Mnyama asichukue ubingwa lakini ifanye kwa kificho, tukikuona hatutakuacha salama. Hapa tulipo tumevua kabisa vazi la utu, tumevua vazi la ustaarabu. Hapa tulipo tumevaa unyama kwelikweli, tusitafutiane lawama. Hatutamuonea mtu aibu, tutakuharibia mazima.
“Sisi tulishatabiriwa na hayati Rais Dkt. Magufuli kwamba sisi ndio tutakuwa wa kwanza kuleta ubingwa wa Afrika twendeni tukakamilishe ndoto hiyo, twendeni tukachukue ubingwa wa Afrika. Makombe ya ndani tumeshashinda sana lakini sasa tunalitaka hili kwa mara ya kwanza.
“Tuko tayari kumfurahisha mama yetu Rais Dkt. Samia kwa mchango mkubwa ambao anatupatia, ametoa ndege bure kutupeleka Morocco na amekuwa akitoa motisha kwa kila mechi. Kilichobaki ni kumheshimisha mama yetu kwa kumpa kombe la Afrika na kuwa Rais wa kwanza Tanzania kubeba kombe la Afrika na tutapeleka kombe Ikulu. Wachezaji wetu waende wakapambane wanavyoweza Simba tuchukue ubingwa, watoe maarifa yao yote, watoe nguvu zao zote Simba tuchukue ubingwa siku ya Jumapili.
Hapa ndipo vita ya Simba SC ilipo

“Tuko hapa Zanzibar kwa kazi moja tu kuchukua ubingwa, hata sio kucheza mechi. Tunaposema kuchukua ubingwa tunamaanisha kupambana vita zote kuchukua ubingwa. Kwanza niwatoe hofu, vita inaendelea. Hawa mnaowaona hapa ni wachache. Kila mtu ametoka alikotoka kuja Unguja kwa kazi moja kuhakikisha Simba anachukua ubingwa. Vita ya nje imeshaanza na tupo vizuri kwelikweli.
“Heshima ambayo tutaiweka Jumapili sio ya mtu mmoja, wewe ndio utapita mtaani ukitamba. Tunatafuta heshima ya pamoja na hivyo lazima tushirikiane. Ndugu zangu tunautaka huu ubingwa na kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu huu ubingwa utabaki Simba Sports Club. Hatutaki ibaki historia kama 1993, hili tutalibakisha.
“Asitokee Mwanasimba yeyote akawa na mashaka. Niwahakikishie kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu mbili zinarudi pale Uwanja wa Amaan na moja lingine litatupa ubingwa.”
Rais Mwinyi alipia gharama za Uwanja wa New Amaan
Taarifa iliyotolewa na Simba SC Mei 22 2025 na Zubeda Sakuru, Ofisa Mtendaji Mkuu Simba SC ilieleza kuwa gharama za Uwanja wa New Amaan kwa ajili ya mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane imelipiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.

“Uongozi wa Klabu ya Simba SC tunamshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kulipia gharama za Uwanja wa New Amaan kwa ajili ya mchezo wetu wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane.
“Uamuzi wa Rais Mwinyi ni msaada mkubwa kwa klabu yetu kwani imesaidia kupunguza gharama za maandalizi ambazo ni kubwa sana kulingana na hadhi ya mchezo husika. Aidha Klabu ya Simba SC inamshukuru Rais Mwinyi kwa kukubali mwaliko wetu wa kuhudhuria fainali akiwa mgeni maalum kwenye mchezo huo utakaopigwa siku ya Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni Uwanja wa New Amaan.”
Inahusiana na hii: Simba SC vs RS Berkane CAF waipeleka Uwanja wa Amaan
Wapinzani wa Simba SC ambao ni RS Berkane tayari wameshawasili Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo utakaoamua bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika. Mei 17 RS Berkane walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba SC.

