- Timu hizo zinakutana katika fainali itakayofuatiliwa na mamilioni ya watu duniani, mchezo ukipigwa katika dimba la Olímpico de la Cartuja, jijini Sevilla
- Hii ni mara ya 260 kwa timu hizo kukutana katika historia
- Msimu huu Barcelona wamekuwa mbabe wa Real Madrid ambapo katika michezo miwili waliyokutana wameizaba vibaya Madrid kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-2.
Barcelona Vs Real Madrid uso kwa uso leo Jumamosi watakutana kwenye mchezo wa kihistoria wa fainali ya Copa del Rey, huku ikielezwa kuwa itakuwa ni vita kubwa ya zaidi ya kombe kwa mahasimu hawa wakuu wa soka la Uhispania.
Barcelona inataka kushinda taji la kwanza kati ya mataji matatu makubwa inayoyalenga katika msimu wa kwanza wa kocha mkuu, Hansi Flick. Timu hiyo inaelekea kutwaa ubingwa wa La Liga, na siku tatu baada ya fainali ya kombe hilo inatarajiwa kuanza nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan.
ANCELOTTI HATARINI KUBWAGA MANYANGA REAL MADRID

Mchezo huu pia unaweza kuwa wa mwisho kwa kocha, Carlo Ancelotti kushinda taji na Madrid, kwani tayari wachambuzi wengi wanabashiri kuwa kuwa kocha huyo anaweza kuondoka msimu huu wa joto, ikielezwa huenda anaenda kuifundisha timu ya taifa ya Brazil.
Madrid ndio wana mambo mengi zaidi ya kupigania, kwani tayari imeondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ualaya, kombe hili ndilo fursa bora ya angalau kumaliza msimu kwa kutwaa taji. Pia bado iko kwenye mbio za La Liga, lakini inahitaji kufuta pengo la pointi nne dhidi ya Barcelona katika mechi tano zilizobaki.
BARCELONA KUENDELEZA UBABE?
Kwa Barcelona, kushinda taji kwa kuwashinda Madrid kutawapa motisha kubwa kuelekea mchezo wao dhidi ya Inter Milan siku ya Jumatano, huku klabu hiyo ya Catalonia ikisaka Kombe la Ulaya kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha muongo mmoja.
BARCELONA Vs MADRID MATOKEO YAO MSIMU HUU
Barcelona imeitawala Madrid katika mechi mbili zilizopita msimu huu, ikiwachapa 5-2 kwenye fainali ya Super Cup ya Uhispania mwezi Januari, baada ya kuishinda 4-0 ugenini kwenye ligi mwezi Oktoba.
BARCELONA Vs REAL MADRID KUSHUHUDIWA NA MASHABIKI 70,000
Mchezo huu ambao unajulikana saka kama El Clasico, ikiwa ni ya tatu ya msimu huu itachezwa mbele ya mashabiki 70,000 katika Uwanja wa La Cartuja mjini Seville, ambapo Mfalme Felipe VI atakabidhi kombe kwa washindi.
Hii ni fainali ya kwanza ya Copa del Rey kati ya vigogo hawa wawili wa Uhispania tangu mwaka 2014. Barcelona inashikilia rekodi ya vikombe 31 vya Uhispania. Madrid ina 20, ikiwa ya tatu kwa idadi ya mataji hayo.
LEWANDOWSKI, BALDE ‘OUT’ KUWAKOSA REAL MADRID
Mara baada ya kuiongoza Barcelona kurejesha uongozi wa pointi 3 dhidi ya Madrid baada ya kuishuhudia timu yake ikiifunga Mallorca 1-0 kupitia bao la Dani Olmo, straika wa wababe ha, Robert Lewandowski anatarajia kuukosa mchezo huo.
Hiki kinatarajiwa kuwa kibarua kikubwa kwa kocha, Hans Flick ambaye atalazimika kujaza nafasi ya Robert Lewandowski aliyeumia msuli wa paja la kushoto wiki iliyopita. Mshambuliaji huyo wa Poland amekuwa na msimu bora mwingine akiwa na jumla ya mabao 40 kwenye michuano yote.
Ferran Torres anatarajiwa kuanza badala yake. Mshambuliaji huyu mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali amekuwa mchezaji muhimu wa akiba msimu huu, akiwa amefunga mabao 17 licha ya kucheza muda mchache, likiwemo tano kwenye kombe hili. Chaguo jingine linaweza kuwa Dani Olmo kucheza kama “namba tisa bandia” akiwa ameambatana na Lamine Yamal na Raphinha.
Barcelona pia haitakuwa na beki wa kushoto wa kwanza, Alejandro Balde. Mchezaji kinda Gerard Martin anatarajiwa kuchukua nafasi hiyo, isipokuwa kama Flick ataamua kuweka mchezaji mwenye uzoefu zaidi.
JE NI WAKATI WA MBAPPE?

Kumaliza msimu bila taji litakuwa ni pigo kubwa kwa Madrid baada ya kumsajili nyota Kylian Mbappé majira ya kiangazi yaliyopita.
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa amefunga mabao mengi lakini ameshindwa kuonesha makali katika mechi muhimu za msimu huu. Alizomewa alipotolewa dakika za mwisho kwenye mchezo wa pili kati ya wawili waliopotezwa dhidi ya Arsenal kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Vinícius Júnior pia ameonekana kupungua makali tangu alipoonekana kupuuzwa kwenye tuzo ya Ballon d’Or mapema msimu huu. Lakini mshambuliaji huyo wa Brazil ameonesha uwezo mkubwa hapo kabla katika mechi za fainali.
CAMAVINGA, MILITAO, CARVAJAL KUWAKOSA BARCELONA
Kiungo Eduardo Camavinga ameumia kano wiki hii na atakosa sehemu iliyobaki ya msimu, akiungana na majeruhi wa muda mrefu wa Madrid ambao ni pamoja na mabeki Dani Carvajal na Eder Militao.
YAMAL ATIKISA, RAPHINHA WAITEKA EL CLASICO

Jukumu kubwa la ulinzi kwa Madrid litakuwa kuwadhibiti mastaa Lamine Yamal na Raphinha, ambao wote walikuwa hatari sana katika clásico zilizopita msimu huu.

