- JEAN Ahoua kiungo wa Simba amefunga bao la ushindi mbele ya Stellenbosch FC kwa pigo la faulo akikosa nafasi ya dhahabu dakika za jioni.
- Kete ya mwisho ugenini nchini Afrika Kusini, Aprili 27 2025 kutoa maamuzi nani kutinga fainaili Kombe la Shirikisho Afrika.
- Simba SC mashuti 22 wapiga kueleka kwa wapinzani wao, moja pekee limeleta bao lililokumbwa na joto ya VAR
SIMBA SC ya Tanzania inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids imepata ushindi wa bao1-0 dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya fainali ambapo ni nusu fainali ya kwanza.

Wapinzani wao Stellenbosch FC mbinu kubwa ambayo wanaitumia kwenye mech izote kimataifa nikuwapa nafasi wapinzani kumiliki mpira kisha wao wanafanya mashambulizi yakushtukiza.
Ilikuwa hivyo mpaka dakika 45 zinakamilika, walipiga mashuti manne pekee kuelekea lango la Simba SC ambao wao walipiga mashuti 16 na katika mashuti hayo ni shuti moja pekee lililenga lango.
MTUPIAJI WA BAO LA USHINDI KWA SIMBA SC
Bao la ushindi kwa Simba SC ambayo ina mtihani kwenye kete ya pili ugenini nchini Afrika Kusini ni pigo la faulo kupitia kwa Jean Ahoua ambaye alifunga akiwa nje ya 18 dakika ya 45.
Ahoua baada ya kufunga bao hilo lilileta utata baada ya mwamuzi kwenda kucheki VAR kudhibitisha bao hilo kama kulikuwa na mtego wa kuotea na mwisho likakubalika hivyo mpira ukapelekwa kati ya uwanja..
Ushindi huo kwenye nusu fainali ya kwanza unafungua ukurasa kwa Simba SC kutanguliza mguu mmoja kutinga hatua ya fainali imepigwa na kuna kazi kubwa kwenye dakika 90 za ugenini Afrika Kusini kulinda ushindi na kusaka ushindi kujihakikishia nafasi kutinga hatua ya fainali.
KADI ZA NJANO
Kwenye mchezo wa Aprili 20 2025 kadi za njano zilionyeshwa kwa wachezaji ambapo Stellenbosch FC waliianza kuingia kwenye orodha hiyo kupitia kwa Enninya dakika ya 35 baada ya kumchezea faulo nyota wa Simba, Ellie Mpanzu.
Mchezaji huyo hakukomba dakika 90 za mchezo ambapo aligotea dakika ya 57 nafasi yake ikachukuliwa na Mcaba ambaye alikamilisha dakika zilizobaki kwenye mchezo huo.
Nyota mwingine ni Ibrahim Jabaar ambaye alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 37 ya mchezo huku kwa upande wa Simba SC nyota aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Mohamed Hussen Zimbwe Jr, Chamou alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 90.
AHOUA KAZI YAKE
Kiungo Ahoua alikosa utulivu mwanzo mwisho wa mchezo akikosa nafasi mbili ndani ya 18 ilikuwa dakika ya 49 kwa pigo la kichwa na dakika ya 90 baada ya shuti lake kwenda nje ya lango akiwa amebaki yeye mwenyewe na nyavu.
Licha yakukwama kufunga bao hilo rekodi zinaonyesha kwamba alipata maumivu dakika ya 89 na alionekana kuonyesha ishara yakutaka kufanyiwa mabadiliko jambo ambalo halikufanyika.
MPANZU KAKOMBA ZOTE 90
Ellie Mpanzu kiungo wa Simba alikomba dakika zote 90 kama ilivyokuwa kwa Fabrince Ngoma, Hamza Jr ambaye alifanya kazi kubwa kwenye ukuta wa Simba kuimarisha ulinzi.
Mpanzu alifanya majaribio ya hatari ambayo yalikwama kuzama nyavuni kwa kipa Masuluke Oscar ambaye aliokoa hatari dakika ya 30 na 78 kutoka kwenye miguu ya Mpanzu.
CAMARAA LANGONI
Moussa Camara alikuwa langoni kwa Simba na aliokoa hatari dakika ya 27, 48, 52, 65, 66, 83 ambapo wapinzani wao walikuwa wakifanya mashambulizi yakushtukiza kuelekea katika lango la Simba SC.
KIKOSI CHA SIMBA KILICHOANZA
Kikosi kazi cha Simba kilichoanza Aprili 20 dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kilikuwa namna hii: -Moussa Camara, Chamou, Hamza Jr, Mohamed Hussen, Shomari Kapombe, Fabrice Ngoma. Jean Ahoua, Steven Mukwala, Ellie Mpanzu, Yusuph Kagoma, Kibu Dennis. Akiba ni Ally Salim, Duchu, Nouma, Edwin Balua, Okejepha, Mavambo, Awesu, Mutale, Leonel Ateba.
Mutale aliingia kipindi cha pili ilikuwa dakika ya 70 akichukua nafasi ya kiungo mshambuliaji Kibu Dennis ambaye hakukomba dakika 90 kwenye mchezo wa kimataifa.
KITUO KINACHOFUATA
Kituo kinachofuata ni Afrika Kusini kwenye kete ya mwisho itakayoamua nani atatinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Aprili 27.
REKODI ZA DAKIKA 90
Rekodi zinaonyesha kuwa Simba ilikuwa na umiliki wa mpira kwa asilimia 57 na wapinzani wao ni asilimia 42 huku mashuti ambayo yalipigwa kuelekea langoni ni 22 kwa Simba SC na wapinzani wao mashuti matano pekee.


