Simba Vs Al MasrySimba Vs Al Masry

UONGOZI wa Simba umetamba kuwa rasmi unaanza maandalizi ya kuielekea michezo miwili ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara baada ya kuwafahamu wapinzani wao.

Simba Vs Al Masry
Simba Vs Al Masry

Ikumbukwe kuwa droo ya mashindano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu hatua ya Robo Fainali yaani, droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika zilifanyika rasmi jana Alhamisi na kushuhudia wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano hayo Simba wakipangwa na Al Masry ya Misri.

Droo hiyo ya hatua ya robo fainali ilifanyika Doha, Qatar ambapo kwa upande wa Simba ni Kaimu Ofisa Mtendaji wao mkuu, Zubeda Sakuru na Meneja wao wa Idara ya Habari na mawasiliano, Ahmed Ally walikuwa sehemu ya viongozi mashuhuda ambao walihudhuria upangwaji wa droo hiyo.

SIMBA KUANZIA UGENINI MAPEMA APRILI

Kama ilivyotarajiwa mara baada ya Simba kuongoza msimamo wa kundi A, wanatarajia kuanzia ugenini ambapo mchezo wa kwanza utapigwa kati ya Aprili 1-2 huku mechi ya marudiano ikitarajiwa kupigwa kati ya Aprili 8-9 kwenye Uwanja wa Benjamin Makapa, Dar es Salaam.

NI MECHI YA KUSAKA MBABE

Katika historia ya ushindani timu hizi zimewahi kukutana mwaka 2018 katika mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho ambapo baada ya dakika 180, hakukuwa na mbabe kwani mechi ya kwanza Simba wakiwa nyumbani uliisha kwa sare ya mabao 2-2 na mechi ya marudiano nchini Misri ikamalizika kwa matokeo ya suluhu.

SIMBA WATAMBA HAWANA HOFU, WANAANZA MAANDALIZI

n
Ahmed Ally na Kaimu CEO wa Simba Zubeda

Mara baada ya kupangwa kwa droo hiyo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally amesema kwa ukubwa wa kikosi chao tangu awali walikuwa hawana shaka ya kupangwa na timu yoyote katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Ahmed amesema Simba ni timu kubwa na walikuwa tayari kupangwa na timu yoyote kati ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Al Masry ya Misri ambazo walikuwa na nafasi kubwa ya kupangwa nazo.

“Sisi tulikuwa tayari kupangwa na yoyote, ukiangalia timu zote tatu ambazo tulitarajia kupangwa nazo tumezizidi uzoefu wa mashindano pamoja na ukubwa, Lakini kwa kuangalia jografia ya nchi yetu kama tungepewa nafasi ya kuchagua mpinzani, tungemchangua Stellenbosch kwakuwa Afrika Kusini ni karibu na tunaweza kusafiri na mashabiki wetu na pia kule kule tuna Matawi hivyo tusingekuwa na ugeni.

“Sasa tunaanza rasmi maandalizi yah atua hiyo ya Robo Fainali yukiamini tunakutana na wapinzani wagumu lakini tupo tayari kwa ajili ya kuliwakilisha vyema taifa letu,” amesema Ahmed.

WACHAMBUZI WAIONYA SIMBA

n

Kufuatia kupangwa kwa droo hiyo wachambuzi mbalimbali wa soka wameitahadharisha Simba juu ya ubora wa wapinzani ambao wanatarajia kukutana nao ambao wanarekodi nzuri katika mashindano hayo.

Akizungumzia hilo mchambuzi wa masuala ya michezo, Hans Raphael amesema: “Ni Droo ngumu kwa Simba, wanakutana na timu shindani haswaa, Al Masry wamewahi kucheza nusu fainali ya CAF, pia wanatoka kwenye ligi bora Africa, wakifanya uzembe watabaki hapa hapa Robo Fainali. Nyota hatari wa kuchungwa ni Karim Bambo ambaye anatumia zaidi mguu wa kushoto.”

KIKOSI SIMBA CHATUA DAR BAADA YA KUICHAPA NAMUNGO

Ahoua Namungo
Ahoua Namungo

Hatimaye kikosi cha Simba kimerejea Dar es Salaam wakitokea katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo ambapo walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC huku wakifanikiwa kuvunja mwiko katika Uwanja wa Majaliwa kutokana na kutopata alama tatu katika miaka miwili mfululizo iliyopita.

LKatika mchezo huo mlinzi wa kati wa Namungo Derick Mukombozi alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 35 baada ya kucheza mchezo usio wa kiungwana. Jean Charles Ahoua aliipatia bao la kwanza dakika ya 49 kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi Shomari Kapombe kufanyiwa madhambi ndani ya 18.

Leonel Ateba alikosa mkwaju wa penati uliookolewa na mlinda mlango, Jonathan Nahimana dakika ya 51 baada ya Elie Mpanzu kufanyiwa madhambi ndani ya 18 na Hassan Kibailo.

Ahoua aliipatia Simba bao la pili dakika ya 72 kwa mkwaju wa penati baada ya Kapombe kufanyiwa madhambi ndani ya 18 na Anthony Mlingo. Steven Mukwala aliipatia bao la tatu dakika ya 92 baada ya shuti kali lililopigwa na Valentine Nouma kumgonga mlinzi wa Namungo kabla ya kumkuta mfungaji.

Ushindi huu umeifanya Simba kufikisha pointi 50 na wanaendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 19 huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.