YANGA na Simba wanakazi kubwa kwenye anga la kimataifa Januari 2025 kwenye kusaka pointi tatu muhimu katika mechi za kazi ambazo zitawapa tiketi ya kutinga hatua yar obo fainali kwenye mashindano hayo makubwa.
Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa kwenye mechi zake za hivi karibuni katika Ligi Kuu Bara ambayo ni namba 6 kwa ubora barani Afrika wamerejea kwenye reli kwa kupata matokeo chanya hivyo mwendelezo huo unatarajiwa kwenye anga la kimataifa.

Yanga inapeperusha bendera kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku Simba ikiwa ni kwenye hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika ni mwendo wa kusaka pointi tatu kwa mechi zijazo.
SEMAJI LA YANGA
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa maandalizi yameanza kuelekea mechi zao zote za kimataifa na wakianza mchezo wa nyumbani dhidi ya TP Mazembe mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
“Tutakuwa nyumbani kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya TP Mazembe kikubwa ni kuona tunapata pointi tatu kwani tutakuwa nyumbani na wachezaji wanatambua kwamba huu ni mchezo muhimu nasi tutapambana kwa ajili ya kuona kwamba tunapata matokeo mashabik wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwapa nguvu wachezaji.
“Maandalizi yetu yameanza mapema ambapo safari hii tunaanza kwa shabiki mmoja kwenye maandalizi kisha wachezaji na benchi la ufundi, yaani hii mechi kila mmoja anahusika na kikubwa ni kuona kwamba tunapata matokeo mazuri kwa kupata pointi tatu.
“Wapinzani wetu tunawaheshimu unaona kwenye mechi ambazo zimepita Desemba tumekuwa na mwendelezo mzuri na malengo ni kuona hii kasi inaendelea bila kupoa, mashabiki tuendelee kuwa pamoja na tushikamane kwenye mechi hii muhimu.”
RATIBA YA MECHI ZA YANGA KIMATAIFA

Ni Januari 4 2025 dhidi ya TP Mazembe, Uwanja wa Mkapa saa 10:00 jioni walipokutana mchezo uliopita walitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1, Yanga ilipata bao la jioni kupitia kwa Prince Dube.
Januari 15 2025 itakuwa dhidi ya Al Hilal ambapo Yanga watakuwa ugenini nchini Mauritania ngoma inatarajiwa kupigwa saa 4:00 usiku walipokutana mchezo uliopita Yanga ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 Uwanja wa Mkapa.
Yanga v MC Alger hii itapigwa Uwanja wa Mkapa Januari 18 2025 saa 10:00 jioni ugenini Yanga ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 mechi mbili za Yanga itakuwa nyumbani na mchezo mmoja itakuwa ugenini.
SIMBA KAZINI KIMATAIFA

Simba itakuwa na kazi kwenye mechi tatu za kimataifa ambazo ni dakika 270. Januari 5 itakuwa SC Sfaxine v Simba, ngoma itapigwa saa 1:00 usiku itakuwa 2025, Tunisia. Walipokutana Uwanja wa Mkapa ilikuwa Simba 2-1, mabao ya Kibu Dennis.
Bravos v Simba, Januari 12 2025 itakuwa Angola saa 1:00 usiku walipokutana Uwanja wa Mkapa ilikuwa Simba 1-0 Bravos kwa bao la Jean Ahoua kwa pigo la penalti.
Simba v Constantine Januari 19 2025 Uwanja wa Mkapa muda utapangwa ambapo ugenini Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 bao la Simba lilifungwa na Mohamed Hussen.
Katika mechi tatu Simba itakuwa mbili ugenini na moja nyumbani hivyo kazi kubwa kwenye mechi za ugenini kusaka pointi tatu itakuwa katika msako wa ushindi ugenini.
HUYU HAPA MKANDAJI KIBU

Mkandandaji Kibu Dennis amebainisha kuwa furaha kubwa ni kuona wanapata matokeo kwenye mech izote ambazo watacheza hivyo watapambana kupata matokeo kwenye mechi zao zijazo.
Kibu ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ambapo kwenye mechi 15 za ligi ni 11 alipata nafasi ya kucheza akikosekana kwenye mechi 4 pekee.
“Ushindani ni mkubwa ndani ya uwanja kutokana na kila timu kuwa tayari kutafuta ushindi ipo hivyo kama ambavyo ilikuwa kwenye mchezo dhidi yaSingida Black Stars na mechi nyingine lakini malengo yetu ni kuona kwamba tunapata matokeo mazuri.”
Simba kete yao ijayo kimataifa inatarajiwa kuchezwa nchini Tunisia itakuwa ni Januari 5 dhidi ya SC Sfaxine ambapo kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Simba ilishinda mabao 2-1 mabao yote ya Simba yakifungwa na Kibu Dennis.

