KUMEANZA kuchangamka ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya wikiendi Yanga na Simba kusepa na pointi tatu muhimu ndani ya uwanja 2024/25 kwa ushindi wa mabao zaidi ya mawili baada ya dakika 90. Wababe hao wawili wameendeleza kuandika rekodi za kibabe uwanjani.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa katika mchezo wake Uwanja wa KMC Desemba 22 2024 imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons. Mechi zote unaweka mkeka wako na SportPesa kisha baada ya mchezo unakunja mkwanja wako bado hujachelewa.
REKODI ZAMOTO KWA YANGA

Yanga imeandika rekodi yake Uwanja wa KMC Complex kwenye mechi mbili kusepa na pointi sita huku ikifunga mabao 7 na wao wakifungwa mabao mawili ilikuwa Yanga 3-2 Mashujaa na mchezo wa pili ni Yanga 4-0 Tanzania Prisons.
Mbali na Yanga kufunga mabao 7 kwenye mechi mbili mfululizo, Prince Dube ameandika rekodi ya kuwa mshambuliaji wa kwanza kufunga hat trick ilikuwa dhidi ya Mashujaa na mchezo wake wa pili dhidi ya Tanzania Prisons amefunga akifikisha mabao manne.
SIMBA WAMO KWENYE REKODI

Simba ni timu ambayo imefunga mabao mengi ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya kucheza jumla ya mechi 13 ndani ya NBC Premier League.
Mabao 29 imefunga huku kinara wa utupiaji akiwa nj Jean Ahoua mwenye mabao sita kibindoni kwenye ligi. Leonel Ateba na Steven Mukwala hawa wawili wametupia mabao mannemanne kila mmoja katika mabao hayo 29.
Ikumbukwe kwamba Simba ni timu ya kwanza kufunga mabao mengi katika mzunguko wa kwanza ilikuwa ni Desemba 21, Kagera Sugar 2-5 Simba. Imefungwa mabao machache uwanjani ambayo ni matano huku Camara akiwa hajafungwa kwenye mechi 10.
HILI HAPA JESHI DHIDI YA KAGERA SUGAR

Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussen ambaye ni nahodha, Chamou, Hamza, Fabrice Ngoma, Jean Ahoua, Mavambo, Steven Mukwala, Ellie Mpanzu, Awesu Awesu.
Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo wa Desemba 21 Uwanja wa Kaitaba nyota Mpanzu ulikuwa ni mchezo wake wa kwanza ndani ya ligi akifanya kazi kubwa kwa ushirikiano na wachezaji wenzake ndani ya uwanja.
HAWA HAPA WATUPIAJI
Shomari Kapombe beki wa Simba alifungua akaunti ya mabao kwa kufunga bao lake la kwanza msimu wa 2024/25 ilikuwa dakika ya 13, Jean Ahoua alipachika bao moja ilikuwa dakika ya 44.
Kiungo Fabrince Ngoma alitupia bao moja ilikuwa dakika ya 53, Mukwala alitupia mabao mawili ilikuwa dakika ya 66, 85 katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.
Ni Ahoua kiungo wa Simba mwenye mabao sita ndani ya ligi alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Kaitaba baada ya dakika 90 Simba ikisepa na pointi tatu mazima.
Ni Datius Peter alifunga bao moja dakika 79 na Cleophance Mkandala dakika 90 alifunga bao la jioni kwenye mchezo huo wakifikisha jumla ya pointi 33 ndani ya ligi.
Simba inakuwa ni timu ya kwanza kufunga mabao mengi ndani ya ligi msimu wa 2024/25 kwenye mchezo mmoja ikiwa ugenini ikifuatiwa na Yanga ambayo imepata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex.
NENO LA SEMAJI
Baada ya ubao wa Uwanja wa Kaitaba kusoma Kagera Sugar 2-5 Simba Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa malengo makubwa ilikuwa ni kupata pointi tatu hilo limewezakana kwa kuwa hawakuwa na matokeo mazuri Kaitaba.
“Tulikuwa na malengo ya kupata pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar hilo limewezekana kwani kwenye mechi za hivi karibuni hatukuwa na matokeo mazuri dhidi ya Kagera Sugar.
“Benchi la ufundi lilitazama mechi zilizopita na kuona kile ambacho tulikuwa tunakosea na kufanyia kazi mwisho matokeo yamepatikana hivyo ni mwendelezo kwenye kupata pointi ndani ya uwanja, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kazi bado inaendelea.
“Licha ya kupata ushindi unaona kwamba tumeruhusu mabao mawili, mashabiki hawajapenda walikuwa wanataka kuona kwamba haturuhusu mabao, makosa yametokea tutafanyia kazi.
USAJILI WA MPANZU UMEJIBU

“Mpanzu ni usajili wetu muhimu kwa kuwa amekuwa kwenye kikosi kwa muda mrefu yeye sio mgeni tena anatambua kuhusu hali ya hew ana namna ambavyo ligi inakwenda hivyo kuanza kwake kumekuwa na manufaa makubwa kwenye timu.
“Uwezo wake ni mkubwa anazidi kufanya kazi ikiwa ni mchezo wake wa kwanza bado kuna mengi kutoka kwake Wanasimba watulie furaha itaendelea na kila mmoja atapata kile anachokipenda kutoka kwa wachezaji wetu.”
PANGA KUSEPA NA MUTALE
Inatajwa kwamba kiungo mshambuliaji Joshua Mutale huenda akakutana na Thank You ndani ya kikosi cha Simba kutokana na kutokuwa kwenye mwendelezo wa ubora katika mechi za ushindani.
Taarifa zinaeleza kuwa Mutale ni miongoni mwa wachezaji ambao wataondolewa katika kikosi cha Simba kwa ajili ya kuleta wachezaji wengine wenye uwezo mkubwa.
Ukiweka kando Mutale kipa Ayoub Lakred ambaye hayupo kwenye uwanja kwa muda mrefu katika mechi za ushindani kutokana na kutokuwa fiti ambapo aliumia mwanzo wa msimu nchini Misri huyu anatajwa kuwa naye atakutana na Thank You.

