JobJob

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic amesema baada ya kumaliza kazi kwenye mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo ni dakika 270 nguvu inaelekezwa kwenye mechi za ligi zinazofuata mbele yao.

Kituo kinachofuata kwa Yanga kwenye ligi itakuwa dhidi ya Mashujaa ya Kigoma inayotumia Uwanja wa Lake Tanganyika kwenye mechi zake za nyumbani kwenye ushindani. Watani zao wa jadi Simba, kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Ken Gold uliochezwa KMC walishinda mabao 2-0.

Duke Abuya
Duke Abuya kiungo wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Yanga inayodhaminiwa na SportPesa mchezo wake wa ligi uliopita kabla ya kuingia kwenye anga la kimataifa ilikomba pointi tatu mazima dhidi ya Namungo kwa ushindi wa mabao 2-0 watupiaji walikuwa ni Kennedy Musonda na Pacome.

Mchezo dhidi ya Mashujaa unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC Complex utakuwa ni wakwanza kwa Yanga kucheza ndani ya uwanja huo mpya kwa msimu wa 2024/25 katika mechi za ushindani kwa kuwa awali walikuwa wanatumia Uwanja wa Azam Complex.

Kwenye msimamo Yanga ambayo imemtambulisha Israel Mwenda kuwa ingizo jipya ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 11 ndani ya ligi vinara ni Azam FC wenye pointi 33 baada ya kucheza mechi 15 ndani ya ligi. Mashujaa kwenye msimamo ni nafasi ya 7 ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi 14.

HUYU HAPA MASHINE YA KIJERUMANI

Ramovic Sead
Ramovic Sead Kocha Mkuu wa Yanga 2024. Source: Yanga.

Ramovic kocha wa Yanga mashine ya kijerumani imesema kuwa wanatambua mchezo dhidi ya Mashujaa utakuwa mgumu hivyo wapo tayari kwa ajili ya kupambana kupata pointi tatu muhimu katika mchezo ambao utakuwa na ushindani mkubwa.

“Baada ya kumaliza mechi 3 za kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika sasa akili yetu ni kwenye ligi, tunataka kupambana na kupata pointi hilo linawezekana kwa kuwa tupo tayari.

“Kuna wachezaji walikuwa na majeraha wamerejea kwenye timu na wako baadhi tutawakosa, kila mchezaji ana nafasi sawa kwenye kikosi changu, jitihada kwenye uwanja wa mazoezi ndio kitu kitakachomuhakikishia mchezaji kwenye kikosi cha kwanza.

“Tumeshamaliza mechi 3 za Ligi ya Mabingwa na sasa akili yetu inaelekea kwenye Ligi Kuu. Tunataka kupambana kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu, nimezungumza na wachezaji umuhimu wa pointi 3 za mchezo na wako tayari.

“Tunapewa nafasi ya kufanya vizuri lakini hilo halitufanyi tuwadharau wapinzani wetu, tunajiandaa vizuri kuhakikisha wachezaji wanakwenda kufanyia kazi tunayowaelekeza mazoezini. Tunaamini utakuwa mchezaji mzuri wenye ushindani.”

 

HUYU HAPA KOCHA MASHUJAA

Abdallah Bares, Kocha Mkuu wa Mashujaa amesema kuwa wanatambua wana kazi kubwa kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga lakini ni muhimu kupata matokeo mazuri kutokana na maandalizi ambayo wamefanya.

“Tunatambua kwamba mchezo wetu utakuwa mgumu lakini huu ni mchezo muhimu kwa upande wetu na tumejiandaa ili tupate alama tatu muhimu ili tukae sehemu nzuri kuelekea kwenye kumaliza mzunguko wa kwanza.”

Mchezo uliopita kwa Mashujaa ilikuwa ni Desemba 15 walikuwa ugenini dhidi ya JKT Tanzania, baada ya dakika 90 ubao wa Gen Isamuhyo ulisoma JKT Tanzania 0-0 Mashujaa, hivyo waligawana pointi mojamoja.

HAWA HAPA WACHEZAJI

Nkane
Nkane Dennis, kiungo mshambuliaji wa Yanga 2024. Source: Yanga.

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Dennis Nkane ameweka wazi kuwa wanatambua kwamba timu wanayokutana nayo ni imara hivyo watapambana kupata matokeo mazuri.

“Sisi wenyewe tunafahamu kwamba, Mashujaa ni aina ya timu ambayo imekuwa na matokeo mazuri katika uwanja wao wa nyumbani na ugenini. Hivyo tuna fahamu tunakwenda kukutana na mchezo mgumu.

“Lakini licha ya ugumu ambacho tunahitaji ni alama tatu muhimu. Tumeshajiandaa kwa namna yoyote watakavyokuja. Tunawasihihi mashabiki waje tupiganie nembo ya Yanga.”

Ibrahim Ame, beki wa kupanda na kushuka ndani ya kikosi cha Mashujaa amebainisha kuwa wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa na malengo ikiwa ni kupata pointi tatu muhimu.

“Tunatambua mchezo utakuwa mgumu na tutaingia kwa tahadhari kubwa ili kupata pointi tatu muhimu. Tutafuata maelekezo ya benchi la ufundi tukiwa uwanjani kwa kuwa mpinzani wetu tunamheshimu.”

 

UIMARA WA TIMU HIZI

Bacca
Bacca beki wa Yanga ambaye ni chaguo la kwanza msimu wa 2024/25. Source: Yanga.

Yanga amba oni wenyeji ni imara kwenye safu ya ushambuliaji ikiwa imefunga jumla ya mabao 16 baada ya kucheza mechi 11 ambazo ni dakika 990 imekuwa na wastani wakufuga bao moja kila baada ya dakika 61.

Kwenye upande wa safu ya ulinzi Yanga ni mabao  manne imefungwa ikiwa na wastani wa kuruhusu bao moja kila baada ya dakika 247.

Wapinzani wao Mashujaa kwenye mechi 14 safu ya ushambuliaji imefunga mabao 11 na ukuta umeruhusu mabao 8. Ni wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 114 baada ya kucheza dakika 1,260 na inaokota bao nyavuni kwa wastani kila baada ya dakika 157.

Share this: