Ahmed AllyAhmed Ally

BAADA ya kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya CS Constantine, uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa hasira zao ni dakika 90 wakiwa nyumbani kwenye mchezo wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikumbukwe kwamba nit imu mbili zinapeperusha bendera ya Tanzania kimataifa, Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika nayo ipo hatua ya makundi huku Simba ikiwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Zimbwe Jr
Zimbwe Jr nahodha wa Simba mfugaji wa bao kimataifa ugenini dakika ya 24. Source: Simba.

Kwenye mchezo dhidi ya Constantine, Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 na wao walianza kufunga bao kupitia kwa nahodha Mohamed Hussen ambaye alipachika bao hilo dakika ya 24.

KUHUSU WACHEZAJI AMBAO HAWAPO FITI

Kipa wa Simba, Aishi Manula alipata changamoto ya kiafya muda mfupi kabla ya kikosi kuelekea Algeria huku beki Hamza akipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Constantine. Kuhusu taarifa yao Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba Ahmed Ally amesema kuwa wote wanapatiwa matibabu.

Hamza
Hamza beki wa Simba ambaye alipata maumivu mchezo uliopita kwa sasa anaendelea vema. Source: Simba.

“Wapo wachezaji walikuwa na changamoto za kiafya, wa kwanza Aishi Manula ambaye aliumwa siku ya kwenda Algeria, kwasasa anaendelea na matibabu na tutawajulisha hali yake. Mchezaji wetu Abdurazak Hamza aliumia kwenye mchezo dhidi ya CS Constantine kwa mujibu wa madaktari atapatiwa matibabu na Alhamisi ataanza mazoezi. Jeraha lake sio kubwa sana.

MWAMBA KAGOMA ISHU YAKE

Yusuph Kagoma
Yusuph Kagoma kiungo wa Simba anayevaa uzi namba 21 ameanza kurejea kwenye ubora. Source: Simba.

“Ipo taarifa njema kuhusu mchezaji wetu Yusufu Kagoma. Kijana ameshapona na sasa yuko tayari kuitumikia Simba. Kabla ya timu kwenda Algeria alikuwa ameshapona lakini mwalimu akaamua kumpa muda ajiandae zaidi. Ataingia kambini na wenzake kujiandaa na mchezo wa Jumapili. Changamoto aliyoipata imekwisha.

“Kwa upande wa majeruhi kwenye kikosi chetu niseme tu tuko salama sana kuelekea mchezo wa Jumapili. Wanasimba wajitokeze kwa wingi kwenye mchezo wetu huu ambao ni muhimu na tunahitaji ushindi.

“Baada ya kupoteza mchezo kuna wenzetu wakaanza kukata tamaa lakini niwambie tu tuko salama sana, hakuna kilichobadilika, nafasi yetu ya kwenda robo fainali iko palepale. Niwakumbushe msimu juzi mpaka mchezo wa pili hatukuwa na alama yoyote na tukaibukia kwa Vipers na kila mmoja anakumbuka Mnyama akavuka kwenda robo fainali.

“Kupoteza na CS Constantine kusitutoe kwenye reli, nafasi yetu ya kwenda robo fainali bado nyeupe kabisa. Nafasi yetu bado iko wazi tukifanya vizuri mechi inayofata. Maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wapo tayari.

KUHUSU KIKOSI BORA

AHMED Ally
AHMED Ally, Meneje awa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba. Source: Simba.

“Timu yetu ni bora kuliko timu nyingine yoyote kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, timu yetu imeimarika sana. Mwanasimba inabidi ujivunie timu yako maana ubora wa kikosi unaongezeka siku hadi siku.

“Mchezo wa Jumapili lazima kila Mwanasimba ajue umuhimu wake maana mpinzani tunayekutana nae anataka kufufukia kwetu na sisi hatuko tayari kuona CS Sfaxien anafufukia kwetu. Hakuna ambaye amewahi kupata uhai ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Tarehe 15 siku ya Jumapili saa 10:00 jioni Uwanja wa Mkapa ni siku ya kumuangamiza CS Sfaxien. Na hili halitawezekana kwa Fadlu, (Davids)  peke yake, kwa Camara, (Moussa) peke yake bali kwa Wanasimba wote kuja uwanjani, hakuna Mwanasimba anayetakiwa kubaki nyumbani. Kama kweli tuna nia ya kumuangamiza mpinzani wetu basi hatuna budi aache nyumba yake aje Benjamin Mkapa.

VIINGILIO KUWA RAFIKI KABISA
“Kwa kuwa mechi hii tunataka tuwe na mashabiki wengi Benjamin Mkapa, tunataka kujaza Benjamin Mkapa. Mara ya mwisho kujaza Uwanja wa Mkapa ilikuwa ni Simba Day. Tumeamua kuweka viingilio ambavyo havitampa mtu sababu ya kutokuja uwanjani lakini pia tupo karibu na sikukuu za mwaka. Na sisi tumeamua kupunguza viingilio ili kila Mwanasimba aje uwanjani.

“Viingilio itakuwa namna hii:-Tanzanite – Tsh. 250,000. Platinum – Tsh. 150,000. VIP A – Tsh. 30,000 (tumeshusha kutoka Tsh. 50,000). VIP B – Tsh. 20,000 (tumeshusha kutoka Tsh. 30,000).
VIP C – Tsh. 10,000 (tumeshusha kutoka Tsh. 15,000).

“Machungwa – Tsh. 5,000 (tumeshusha kutoka Tsh. 10,000). Mzunguko – Tsh. 3,000 (tumeshusha kutoka Tsh. 5,000). Mwanasimba upewe nini tena? Tunaamini hakuna Mwanasimba ambaye atabaki nyumbani.”

“Tuko mwisho wa mwaka na kuna watu tangu wameoana hajamtoka out, huwezi kumpeleka Dubai, huwezi kumpeleka Serengeti, huwezi kumpeleka hata Zanzibar basi ushindwe hata kumleta Uwanja wa Mkapa kwa Tsh. 3,000?

“Na sisi tunakuhakikishia ukija Jumapili na familia yako mtaondoka na furaha.” Amesema Ahmed Ally.

Share this: