ANGA la kimataifa, Simba wamekomba pointi tatu kwenye dakika 90 za Uwanja wa Mkapa kwa ushindi mbele ya wapinzani wao Bravos ya Angola ikiwa ni mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa kwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Ikumbukwe kwamba watani zao wa jadi Yanga, kete yao ya kwanza dakika 90 Uwanja wa Mkapa iliyopewa jina la Dube Day ngoma ilikuwa nzito kwa mabingwa hao watetezi wanaodhaminiwa na SportPesa kwenye ligi baada ya kupoteza mbele ya Al Hilal ya Sudan.
CAMARA KAZINI KIMATAIFA

Mousa Camara, kipa wa Simba alikuwa kazini kwenye dakika 90 za nguvu ambapo aliokoa hatari zaidi ya nne ikiwa ni pamoja na penalty iliyopigwa dakika ya 48 akaiweka kwenye mikono yake na kulifanya lango kuwa salama.
Kwenye mchezo dhidi ya Bravos bao la Simba lilipatikana kwa penalti dakika ya 26 kupitia kwa Jean Ahoua ambaye alipachika bao hilo kwa mguu wake wa kulia na Steven Mukwala dakika ya 42 jaribio lake lilikwenda nje kidogo ya lango.
Ilikuwa kazi kubwa kimataifa kwa Camara kuwatuliza wachezaji wa Simba hasa kipindi cha pili ambapo Bravos walionekana kuchangamka mwanzo mwisho kwa kufanya mashambulizi makali ikiwa ni dakika ya 56, 57 yote yakiokolewa na Camara.
KIKOSI KAZI CHA SIMBA

Mousa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussen, Hamza, Che Malone, Fabrince Ngoma,Ladack Chasambi, Okejapha, Steven Mukwala, Jean Ahoua na Kibu Dennis hawa walianza kikosi cha kwanza.
Akiba ilikuwa ni Aishi Manula, Nouma, Chamou, Mavambo, Mzamiru Yassin, Awesu Awesu, Leonel Ateba, Mutale, Edwin Balua.
SEMAJI HESABU KIMATAIFA

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa hesabu kubwa kwenye mechi za kimataifa ni kutinga hatua ya robo fainali kisha robo fainali kwa kuwa hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi walichonacho.
“Tunatambua tuna kazi ngumu kwenye mechi zetu zote kimakataifa nyumbani na ugenini na malengo yetu ni kuona kwamba tunatoka kwenye hatua ya makundi na kutinga hatua ya robo fainali kisha nusu fainali kwa kuwa kila kitu kipo kwenye mpango.
“Mechi za nyumbani ni muhimu kufanya vizuri na kupata pointi, mashabiki na Wanasimba ni muhimu kujitokeza kwenye mechi zetu zote kuwapa nguvu wachezaji kucheza kwa kujituma kutafuta matokeo mazuri kwa kushangilia vibayavibaya.
“Benchi la ufundi linafanya kazi kubwa kuona kwamba matokeo mazuri yanapatikana kwenye mechi zetu zote za kimataifa hivyo kazi inaendelea kufanyika kwa kuwa wachezaji wanajua kwamba mashabiki wanahitaji matokeo mazuri uwanjani ambayo ni ushindi.”
KAZI YA KWANZA MRITHI WA GAMONDI

Kwa Yangakwenye anga la kimataifa Kocha Mkuu, Saed Ramovic mchezo wake wa kwanza Novemba 26 2024 alianza na kikosi kazi cha namna hii:-
Djigui Diarra, Yao, Nickson Kibabage, Dickson Job, Bacca, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Aziz Ki, Pacome.
Kwa upande wa wachezaji wa akiba ni Aboutwalib Mshery, Bakari Nondo, Kibwana Shomari, Dennis Nkane, Sure Boy, Jonas Mkude, Shekhan Khamis, Clatous Chama, Kennedy Musonda.
Baada ya dakika 90, Yanga Novemba 26 2024 ilishuhudia ubao ukisoma Yanga 0-2 Al Hilal ukiwa ni mchezo wa tatu kwa Yanga kupoteza mfululizo kwenye mechi za mashindano ambazo ni dakika 270.
Ipo wazi kwamba mechi mbili zilikuwa ni za ligi ilikuwa Yanga 0-1 Azam FC na Yanga 1-3 Tabora United zama za Miguel Gamondi ambaye kwa sasa amepewa Thank You mbinu zake hazitatumika tena mikoba yake ipo mikononi mwa Ramovic.
Mchezo wa kwanza kwa Ramovi ilikuwa wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 0-2 Al Hilal. Mech izote tatu Yanga ilikuwa nyumbani hivyo kwenye anga la kimataifa ina kazi ya kufanya katika mechi zijazo kupata pointi tatu kufika hatua yar obo fainali.
HUYU HAPA KOCHA MJERUMANI
Kocha Mkuu wa Yanga, Mjerumani Ramovic ameweka wazi kuwa bado wana kazi kubwa ya kufanyia kazi makosa ambayo yalitokea kwenye mchezo uliopita licha ya kwamba wachezaji hawajawa fiti kwa asilimia kubwa.
Siku moja kabla ya mchezo kocha huyo alibainisha kuwa haitakuwa kazi rahisi kupata muunganiko mzuri na mbinu zake kuelekeweka mapema kwa kuwa ni mwanzo akiwa hajatumia hata siku 10 kwenye mazoezi.
“Ni ngumu kusema kuwa kutakuwa na mwendelezo mzuri na kiwango bora kwa kuwa bado tunaanza kutengeneza kikosi. Muda ambao nimekuwa na wachezaji haujawa mkubwa lakini tuna amini kwamba tutashirikiana ili kupata matokeo mazuri.
“Wapinzani wetu tunawaheshimu na kikubwa kwenye mechi zetu kila mchezaji ana nafasi ya kupata matokeo kikubwa ni juhudi uwanjani pamoja na nidhamu kwa kuwa mchezo wa mpira ni kitu ambacho hauwezi kuficha.”

