YANGA Novemba 5 2024 wanatimiza mwaka mmoja baada ya kupata ushindi mkubwa kwenye Kariakoo Dabi katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa Novemba 5 2023 baada ya dakika 90 wakasepa na pointi tatu mazima.
Huo ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa Yanga mbele ya Simba msimu wa 2023/24 walipotwaa taji la ligi wakimaliza ligi na pointi 80 baada ya kucheza jumla ya mechi 30 ndani ya uwanja ambazo dakika 2,700.
Ipo wazi kwamba Yanga inadhaminiwa na SportPesa ina kazi ya kutetea taji la ligi kwa msimu wa 2024/25 na imecheza jumla ya mechi 9 ikipoteza mchezo mmoja kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Yanga 0-1 Azam FC.
HAWA HAPA WATUPIAJI KARIAKOO DABI

Katika mchezo wa Kariakoo Dabi uliochezwa Uwanja wa Mkapa, ilikuwa kazi kubwa kwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kusaka pointi tatu mbele ya Simba ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo.
Mapema dakika ya 3 Kennedy Musonda alitupia bao la kwanza kwa Yanga ambalo hilo halikudumu sana iligotea dakika ya 9 kwa Simba kuweka mzani sawa kwa kupachika bao kupitia kwa Kibu Dennis ambaye alitumia pasi ya kiungo mshambuliaji Saido Ntibanzokiza.

Maxi Nzengeli kiungo huyu mshambuliaji alitupia mabao mawili kwenye mchezo huo, Aziz Ki alitupia bao moja na msumari wa tano ulipachikwa kupitia mkwaju wa penalty mtupiaji akiwa ni Pacome.
Ikumbukwe kwamba langoni ni Aishi Manula alianza baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kwa kuwa hakuwa fiti na mchezo wake wa kwanza kurejea ilikuwa Kariakoo Dabi huku Ally Salim ambaye alikuwa kipa kwenye mechi zilizopita akiwekwa benchi kutokana na ukubwa wa mchezo huo.

Maxi alibainisha kuwa kikubwa ambacho walikuwa wanakifanya kwenye mechi ni kutafuta ushindi jambo ambalo lilifanikiwa na furaha ya mashabiki ikiwa kuona wao wanapata pointi tatu muhimu Pamoja na ushindi kwa kufunga mabao.
“Kwenye mechi ambacho tunahitaji ni kupata ushindi na matokeo mazuri, muhimu pointi tatu na ilikuwa hivyo kwetu hivyo tunaamini kwamba furaha yetu imekamilika na mashabiki wamepata kile ambacho walikuwa wanahitaji.
“Mchezo wa dabi sio mwepesi hasa ukizingatia kwamba kila mchezaji anahitaji kuona matokeo yanapatikana na timu zote zinahitaji kupata ushindi hivyo ambacho kinatokea ni matumizi mazuri ya nafasi ndani ya uwanja.”
MASTA GAMONDI AWAPA TANO WACHEZAJI
Miguel Gamondi, masta baada ya ushindi huo aliwapa tano wachezaji wake kwa kubainisha kuwa walifanya kazi kubwa kutafuta matokeo na mwisho ilikuwa hivyo licha ya kupata ushindi mkubwa malengo yao ilikuwa ni pointi tatu muhimu.
“Kupata ushindi mkubwa haikuwa matarajio yetu kikubwa ilikuwa kuona kwamba tunapata pointi tatu muhimu halafu mengine yanafuata. Wachezaji walijituma mwanzo mwisho kuhakikisha matokeo yanapatikana na ilikuwa hivyo pongezi wanastahili kwa kuwa sio kazi rahisi.
“Mchezo mkubwa unakuwa na hisia kubwa, na Simba sio timu ndogo unaona namna ambavyo wanacheza, wachezaji wake wengi wana uzoefu mkubwa hivyo kushinda ushindi mkubwa ni furaha kwetu na mashabiki tuna amini wamefurahi kuona hali inakuwa hivi.”
KIBU DENNIS MAJANGA MATUPU

Kibu Dennis kiungo mshambuliaji wa Simba unaweza kusema ni majanga matupu kwake ndani ya kikosi hicho kwa kuwa hajafunga bao tena kwenye mechi za ligi licha ya kupata nafasi kwenye mechi za ushindani ambazo timu hiyo inacheza.
Mara ya mwisho kufunga bao kwenye mchezo wa ligi ilikuwa kwenye Kariakoo Dabi, Novemba 5 2024 alipotumia pasi ya Ntibanzokiza baada yah apo hajapata bahati ya kufunga tena ndani ya uwanja katika mechi za ushindani kwenye ligi pekee.
Msimu wa 2024/25 ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids bado hajafungua akaunti ya mabao rasta Kibu D wengi hupenda kumuita mkandaji ambaye kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa alianza kikosi cha kwanza .
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika baada ya dakika 90 ubao ulisoma Mashujaa 0-1 Simba bao la ushindi likifungwa na Steven Mukwala dakika ya 90 ya mchezo.
Simba ilisepa na pointi tatu mazima ugenini na kurejea Dar kwa ajili ya mechi za ushindani kwa msimu wa 2024/25 ambao kila timu inapambana kufikia malengo yake.

