WIKIENDI ilikuwa na mambo mengi huku kila shabiki akianza mwanzo wa wiki na matokeo yake kwenye mtima wake kutokana na timu aliyokuwa akiamini itapata matokeo ndani ya dakika 90 kuvuja jasho kusaka ushindi huku mwamba Eric ten Hag wa Kocha Mkuu wa Manchester United akikalia kuti kavu kutokana na mwendo wa timu hiyo.
Kuna wanaoanza wiki wakiwa na furaha na wapo wenye huzuni hivyo maisha lazima yaendelee na soka linapigwa la maana ndani ya uwanja huku mikwanja ikitolewa kupitia SportPesa kwa uhakika kila wakati.

Ikiwa ni wiki ya 11 ya La Liga ni kicheko kwa Barcelona huku Real Madrid ikiwa ni huzuni kwao baada ya kupoteza katika mchezo wa El Classico Uwanja wa Santiago Bernaneu kwa kushuhudia ubao ukisoma Real Madrid 0- 4 Barcelona.
Walikuwa nyumbani kwenye mchezo huo wa La Liga kusaka pointi tatu waliyeyusha zote mazima na kukwama kupata hata bao la kufutia machozi kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ilikuwa ni Oktoba 26 2024.
Kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa watupiaji walikuwa ni Robert Lewandowski huyu alirejea kambani mara mbili ilikuwa dakika ya 54, 56 mwamba Lamine Yamal Nasraqui Ebana yeye alitupia bao moja ilikuwa dakika ya 77 na kamba ya nne kukamilisha 4G ilijazwa kimiani na Raphina dakika ya 84.

Katika mchezo huo kuna kadi za njano zilitolewa ilikuwa dakika ya 87 kwa Eder Militao, Vinicius Jr dakika ya 80 kwa upande wa Real Madrid na Marco Casado Torras dakika ya 44, Jules Kounde dakika ya 69, Indigo Martinez dakika ya 75, Inari Pena dakika ya 82, Gavi dakika ya 90 kwa Barcelona.
Ushindi huo unaifanya Barcelona kuongoza La Liga wakiwa na pointi 39 nafasi ya pili ni Real Madrid wakiwa na pointi 24 kibindoni msimu wa 2024/25 ambao una ushindani mkubwa mwanzo mwisho ndani ya uwanja.
KOCHA MANCHESTER UNITED AKALIA KUTI KAVU

Dakika 90 chungu zilikuwa kwa Manchester United baada ya ubao wa Uwanja wa London kusoma West Ham 2-1 Manchester United, Gary Neville ameweka wazi kuwa anafikiria Eric ten Hag atafukuzwa ndani ya timu hiyo hivyo ni kama amekalia kuti kavu hivi.
Manchester Legend, Gary Neville amesema kuwa anaamini bosi wa Manchester United, Eric ten Hag ataondolewa katika majukumu yake ndani ya Manchester United, inayotumia Uwanja wa Old Traford kwa mechi za nyumbani.
Jumapili ya Oktoba 27 Manchester United walipoteza ugenini shukrani kwa bao la jioni la penalti iliyofungwa na Jarrod Bowen dakika ya 90 ambapo penalti hiyo ilibidi itazamwe kwenye VAR kutokana na utata kutokea baada ya tukio hilo ndani ya 18.
Bao pekee la Manchester United lilifungwa na Casemiro dakika ya 81 kabla ya Bowen kuvunjavunja mioyo ya United na bao la utangulizi kwa West Ham lilifungwa na Crysencio Summerville dakika ya 74.

Nyota huyo amesema:” Eric ten Hag anatafuta matatizo. Yupo nafasi ya 14 katika msimamo baada ya mechi 8 na mechi hizo ni kama asilimia 25 hivi ya msimu. Inakuwa ni mbaya kila wakati kutokana na viwango, United inapaswa kuwa juu lakini wamepoteza.”
WASHIKA BUNDUKI ARSENAL WATOSHANA NGUVU

Washika bunduki Arsenal ngoma ilikuwa nzito kwenye mchezo wao wakiwa nyumbani baada ya kushuhudia ubao wa Uwanja wa Emirates ukisoma Arsenal 2-2 Liverpool wakigawana pointi mojamoja kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.
Mabao ya Arsenal yalifungwa ba Bukayo Saka dakika ya 9 akifikisha jumla ya mabao 50 ndani ya Ligi Kuu England huku lile la pili likifungwa na Mikel Merino dakika ya 43 akimalizia pigo la faulo iliyopigwa kwenye mchezo huo ambayo ilileta utata kidogo kwa wachezaji wa Liverpool kudai kuwa mfungaji alikuwa ameotea.
Iliyeyuka dakika moja nyingine wakitazama VAR mwisho ikawa ni kamba kwa Arsenal katika mchezo huo waliposhuhudia mwamba Virgil Van Djik akiweka usawa dakika ya 18 na lile la pili ni Mohamed Salah dakika ya 81.
Kuna mastaa ambao walionyeshwa kadi za njano kwenye mchezo huo ni pamoja na David Raya dakika ya 66, Gabriel Jesus dakika ya 90 kwa Arsenal na Darwin Nunez dakika ya 90, Alexis Mac Allister dakika ya 33 kwa Liverpool.
Mrithi wa mikoba ya Jurgen Klopp, Arne Slot anaendeleza rekodi yake ya kutofungwa ugenini baada ya kuanza kazi ndani ya timu hiyo kwa msimu wa 2024/25.

