Nyie Hamuogopi VibeNyie Hamuogopi Vibe
Yanga kamili
Yanga kamili Nyie Hamuogopi? Uwanja wa Mkapa Agosti 4 2024. Source: Yanga.

MCHORA ramani za ushindi ndani ya kikosi cha Yanga, Miguel Gamond ambaye ni Kocha Mkuu wa timu hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa amebainisha kuwa kwa msimu wa 2024/25 watapambana kufanya vizuri kwenye mechi za ushindani kitaifa na kimataifa baada ya kilele cha Wiki ya Wananchi iliyokuwa inakwenda na kauli mbio ya Nyie Hamuogopi?.

Ipo wazi kwamba Yanga ni mabingwa watetezi wa ligi baada ya kutwaa ubingwa msimu wa 2023/24 na walimaliza wakiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo, pointi 80 kibindoni baada ya mechi 30 watapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Agosti 4 2024 ilikuwa ni kilele cha SportPesa Wiki ya Wananchi ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 2-1 Red Arrows kwa mabao ya Mudathir Yahya dakika ya 64 na Aziz Ki dakika ya 90 kwa pigo la penalti na bao la Red Arrows lilifungwa na Ricky Banda dakika ya 6.

Gamondi amesema; “Nimefurahishwa na namna ambavyo wachezaji wanacheza mchezo wetu dhidi ya Red Arows ulikuwa ni mkubwa na wenye ushindani mkubwa tumefurahi kupata ushindi katika mchezo wetu ikiwa ni kuelekea kwenye mechi zinazofuata.

“Mwanzo mzuri kwa kila mchezaji kuna kitu ambacho kinazidi kuendelea hasa katika kuimarika na kuwa bora kwa ajili ya mechi za ushindani ambazo zipo. Ninawapongeza wachezaji na mashabiki kujitokeza kwa wingi jambo hili ni kubwa.”

MUDA KAANZA NA BALAA HUKO

Mudathir
Mudathir Yahya kwenye Nyie Hamuogopi? kiungo mshambuliaji wa Yanga 2024/25. Source:Yanga

Kiungo wa kazi ndani ya Yanga, Mudathir Yahya ameanza na balaa kwa kufunga moja ya bao katika mchezo wa kimataifa kwa utulivu mkubwa akiwa nje ya 18 akitumia pasi ya MVP, Aziz Ki mwenye jezi namba 10 mgongoni kwenye tamasha la Nyie Hamuogopi? Namba hiyo ni utambulisho wake msimu wa 2024/25.

Yanga katika kilele cha Wiki ya Mwananchi walianza kushuhudia wakifungwa ndani ya dakika 45 za mwanzo bao ambalo lilidumu kwa dakika 45 na kipindi cha pili waliweka usawa Yanga na jioni walifunga bao la ushindi.

Ni mwendelezo wa kile ambacho alikifanya msimu wa 2023/24 akiwa uwanjani na kila alipokuwa akifunga alikuwa anashangilia kwa mtindo wa kupiga simu jambo linalomaanisha kwamba msimu wa 2024/25 simu zitaita sana.

Ipo wazi kwamba jina la Muda lipo kwenye orodha ya kikosi bora msimu wa 2023/24 kutokana na kazi ambayo alifanya uwanjani chini ya Gamondi kwenye mechi alizopewa nafasi ndani ya ligi alifanya kweli kila alipopata nafasi.

AZIZ KI MASHOTO KAZINI

Aziz KI Yanga
Aziz KI kiungo mshambuliaji wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Mkali wa mguu wa kushoto Aziz Ki ambaye ana tuzo nne msimu wa 2023/24 ikiwa ni ile ya ufungaji bora baada ya kufunga mabao 21, kiungo bora wa msimu, MVP na kuwa ndani ya kikosi bora aliendeleza makali yake ya mguu wa kushoto kwa kutoa pasi na kufunga.

Aziz alitoa pasi kwa Muda akitumia mguu wa kushoto kupitia kona aliyopiga na alifunga bao la ushindi dakika ya 90 kwa pigo la penalti kwa mguu wake uleule wa kushoto na kuwanyanyua mashabiki wa Yanga jioni kabisa.

REKODI YA FULL HOUSE

Msemaji wa Yanga, Haji Manara ambaye aliwatambulisha wachezaji wa Yanga kuelekea msimu wa 2024/25 aliweka wazi kuwa imeandikwa rekodi ya kujaza viwanja viwili kwa mara moja katika tamasha moja, Agosti 4 2024.

Ni Uwanja wa Uhuru ambao hapo walikuwepo mashabiki wa Yanga wakutosha pamoja na Uwanja wa Mkapa ambapo napo mashabiki walijitokeza kwa wingi kushuhudia burudani zikitolewa.

Katika utambulisho wake Manara alimtambulisha pia Aziz Ki kwa kumpa majukumu ya nyota huyo kumvalisha uzi wa Yanga Hamisa Mobeto jambo ambalo lilizua shangwe uwanjani. Wengine ni Clatous Chama, Djigui Diarra, Nickson Kibabage, Aziz Andambwile, Dickson Job.

“Anaitwa Aziz Ki huyu MVP yeye, kiungo bora yeye na tuzo ya ufungaji bora yeye, mpaka Mobeto. Aziz upo vizuri tumuite Mobeto umvishe jezi? Alihoji Manara ambapo Ki aliitikia ndio. Tukio hilo lilishuhudiwa na mashabiki wengi lilizua shangwe kila kona kwa kiungo huyo kumvisha jezi ya Yanga Mobeto ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga inayonolewa na Gamondi.

SIMU KUTOKA KWA MAMA

Mpango
Mgeni rasmi wa Wiki ya Wananchi, Makamu wa Rais, Philip Mpango. Source: Yanga.

Mgeni Rasmi Wiki Ya Mwananchi 2024 alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ambaye kwenye tamasha hilo alikabidhiwa kadi ya uanachama wa Yanga na Rais wa Yanga Injinia Hersi Said mbele ya Wananchi ambao walikuwa kwenye kilele cha furaha.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu alizungumza na mashabiki wa Yanga kupitia simu ya mkononi ambapo aliweka wazi kuwa anawafuatilia moja kwa moja kwenye TV na alisema : “Nimeona kwamba mmejaza viwanja viwili, ninyi kweli ni taifa kubwa. Nimefuatilia usajili wenu mmesajili vizuri pongezi mnastahili.”

Share this: