
HABARI ya mjini kwa sasa ni SportPesa Supu Day ikiwa ni mpango kazi maalumu ulioandaliwa na Yanga kwa kushirikiana na wadhamini wake SportPesa kwenye Wiki ya Wananchi kuelekea kilele cha tamasha hilo kubwa linalotarajiwa kufanyika Agosti 4 2024 Uwanja wa Mkapa slogan ikiwa ni Nyie Hamuogopi?
Mpangilio mzima wa Supu Day ulianza asubuhi kwa mashabiki wengi kujitokeza kutokana na hamasa iliyopo. Ratiba ilikuwa wazi kuhusu uwepo Jogging kwa mashabiki ikiwa ni sehemu ya michezo kwa afya.
SPORTPESA SUPU DAY ILIVYOKUWA
Jogging routes ilianzia makao makuu ya Yanga, Jangwani, Kigogo,Magomeni Mikumi, Magomeni Mapipa, Fire, Jangwani ikiwa ni kituo cha mwisho kukutania na ikumbukwe kwamba hapo ndipo walianzia mapema saa 12:00 asubuhi.
YANGA V RED ARROWS

Agosti 4 2024 itakuwa ni Kilele cha Wiki ya Mwananchi ambapo Yanga itacheza mchezo wa kimataifa dhidi ya Red Arrows ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kuwatambulisha wachezaji wapya na wale waliokuwa kwenye kikosi cha Yanga kwa msimu wa 2023/24.
Haji Manara, Msemaji wa Yanga ameweka wazi kuwa watafanya utambulisho wa wachezaji kipekee na itakuwa ni darasa kwa wengine kutambua namna ya kufanya utambulisho kwa wachezaji wakubwa unavyokuwa kwa kuwa wao ni wataalamu kwenye eneo hilo.
“Tunakwenda kutoa darasa ya namna ya kufanya utambulisho mkubwa kwa kuwa hapa wataalamu tupo. Unajua ni raha kumtambulisha mchezaji mkubwa Clatous Chama, Aziz Ki, Prince Dube hawa wachezaji ni wakubwa na wanafanya kazi kubwa usisahau kwamba wale waliopo Yanga wametwaa ubingwa msimu uliopita.
“Dickson Job, Mudathir Yahya ni fahari ya Yanga na wachezaji wote wanajituma kwenye kutimiza majukumu yao. Hivyo mashabiki mjtokeze kwa wingi kushuhudia burudani na somo kwa wengine namna ya kufanya utambulisho inavyokuwa.”
IJUE SABABU YA SPORTPESA SUPU DAY

Wadhamini wakuu wa Yanga SportPesa kupitia kwa Mkurugenzi wa Mahusiano wa TZ Sportpesa, Sabrina Msuya walibainisha sababu ya kuja na SportPesa Supu Day “Sisi kama wadhamini wakuu tutakuwa pamoja kwenye supu day siku ya Jumamosi, Kampuni ya SportPesa imeandaa supu kwa wananchi wakiwa wanajiandaa kupata burudani kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi.”
MASHINE MPYA YANGA
DUBE
Usiku wa kuamkia Julai 7 2024 ilitolewa zawadi ya 7/7 kwa mashabiki wa Yanga kwa utambulisho wa mshambuliaji Prince Dube kuwa ni mali ya Yanga. Dube alikuwa na kikosi Afrika Kusini ambapo walitwaa Kombe la Toyota Cup kwenye mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs.
Katika mchezo huo wa maandalizi kuelekea2024/25 Yanga ilishinda mabao 4-0 huku Dube naye akitupia bao moja, Aziz Ki alitupia mabao mawili na Clement Mzize alitupia bao moja.
BOKA

Beki wa kushoto kutoka FC Lupopo anaitwa Boka Chadrak alitambulishwa usiku wa kuamkia Julai 8. Anakuja kuwa mbadala wa Joyce Lomalisa ambaye hatakuwa ndani ya kikosi cha Yanga kwa msimu wa 2024/25 baada ya mkataba wake kugota mwisho.
Nyota huyu alikuwa na kikosi nchini Afrika Kusini hakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs kwa kuwa alipata maumivu. Kwa mujibu wa Meneja wa Yanga, Walter Harrison aliweka wazi kuwa anazidi kutengamaa hali yake.
KHOMEINY
Mwanzo wa siku mpya mapema kabisa ilikuwa Julai 8 2024 Yanga walimtambulisha kipa Aboubhakar Khomeiny ambaye msimu wa 2023/24 alikuwa ndani ya Ihefu. Yupo ndani ya kikosi cha Yanga anaungana na Djigui Diarra, Aboutwalib Mshery kwenye eneo la walinda milango.
Mshery na Diarra bado wapo ndani ya Yanga kwa kuwa waliongeza kandarasi ndani ya timu hiyo inayonole na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ambaye aliongeza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumika Yanga.
DUKE
Kiungo Duke Abuya anatajwa kuwa miongoni mwa sajili ambazo zitakuwa na mwendo mzuri kutokana na uwezo wake kwenye umiliki wa mpira na pasi zenye uhakika ndani ya kikosi cha Yanga ambacho kitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
CHAMA

Kiungo Clatous Chama huyu ni mchezaji wa kwanza kutambulishwa ndani ya Yanga kwa wale ambao walisajiliwa kuelekea msimu mpya wa 2024/25. Msimu wa 2023/24 alikuwa Simba na alifunga mabao 7 akitoa pasi sita za mabao. Chama ameweka wazi kuwa anaanza changamoto mpya hivyo mashabiki wakutane uwanjani.

