
PATACHIMBIKA leo Uwanja wa Mkapa kwenye kilele cha tamasha la Simba Day Agosti 3 2024 ambalo ni maalumu kwa ajili ya utambulisho wa wachezaji wapya, benchi la ufundi, uzi mpya utakaotumika msimu wa 2024/25 unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ikumbukwe kwamba mabingwa wa msimu wa 2023/24 ni Yanga wao wanakuja na tamasha la Mwananchi Day Agosti 4 2024 ambapo Agosti 3 2024 ilikuwa ni SportPesa Supu Day ikiwa ni hamasa kueleka kilele Uwanja wa Mkapa.
Simba inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya APR ya Rwanda mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa pamoja na burudani kutoka kwa wasanii wakubwa Bongo.
PATACHIMBIKA KWENYE BURUDANI

Kwa upande wa burudani kwenye Simba Day inayokwenda na slogan ya Ubaya Ubwela kuna mastaa wakubwa watakaotoa burudani.
- Ali Kiba, Legend wa Bongo Fleva ambaye ana ngoma kali ikiwa zinazobamba Afrika Mashariki na kati na dunia kiujumla. Ni yeye atakuwa kiongozi kwa upande huu unaikumbua ile Unyama ni Mwingi? Kazi yake King Kiba.
- Joh Makini, mwamba wa Kaskazini kutoka Weusi tangu ngoma kali ikiwa ni pamoja na Popote nyota huyu anatarajiwa kutoa burudani.
- Chino Kidd atakuwepo Uwanja wa Mkapa
SAKATA LA MAKABILA
Awali ilikuwa inatajwa kuwa msanii Dulla Makabila ataimba kwenye tamasha la Simba Day lakini mashabiki waligomea hilo. Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa Makabila hakuwepo kwenye mpango wa watakaotoa burudani.
“Makabila hakuwa kwenye mpango wa wale watakaotoa burudani. Lakini kabla hatujawataja wasanii tumeona wahusika wenyewe ambao ni mashabiki wamemkataa unadhani tungefanya nini kama wahusika wa burudani hawamhitaji? Basi hatakuwepo pia.”
BENCHI LA UFUNDI

Julai 5 2024 Simba ilimtambulisha kocha mpya ambaye ni Fadlu Davids ambaye alikuwa na kikosi kambini nchini Misri. Msaidizi mzawa ndani ya Simba ni Seleman Matola ambaye ameweka wazi kuwa wanatarajia kuwa na msimu wenye ushindani mkubwa na wapo tayari kufanya vizuri.
Fadlu ameweka wazi kuwa kuelekea mchezo dhidi ya APR kikubwa wanachohitaji ni ushindi kwa kuwa ni mchezo muhimu kwao mbele ya mashabiki ambao wamenunua tiketi zote siku tatu kabla ya kilele cha Simba Day.
WATAMBUE NYOTA WAPYA SIMBA
MASHAKA
Valentino Mashaka ni kiungo mshambuliaji alikuwa akikipiga Geita Gold. Ilikuwa ni Julai 5 2024 Valentino alitambulishwa ndani ya kikosi cha Simba. Huyu ni kiungo mshambuliaji ambapo alipokuwa ndani ya Geita Gold alikuwa ni chaguo la kwanza.
OKEJAPHA
Anaitwa Augustine Okejapha ametambulishwa ndani ya kikosi cha Simba kwa ajili ya kupata changamoto mpya. Nyota huyo ni raia wa Nigeria.
MUTALE
Joshua Mutale alitambulishwa ndani ya kikosi cha Simba Julai Mosi 2024. Kwenye kambi ya Misri alikuwa gumzo kutokana na spidi, nguvu katika mazoezi.
MUKWALA
Steven Mukwala ni nyota mpya ndani ya kikosi cha Simba alitambulishwa Julai 2 2024 kuwa ndani ya kikosi hicho ambacho kitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
CAMARA
Moussa Camara yeye ni kipa alitambulishwa rasmi ndani ya Simba Agosti 2 2024. Inatajwa ni kandarasi ya miaka miwili amesaini.

JEAN
Ingizo jingine jipya ndani ya Simba ni Ahoua Jean Charles ambaye alitambulishwa Julai 3 2024.
HAMZA
Nyota mwingine mpya ndani ya kikosi cha Simba ni Abdulrazack Mohamed Hamza alitambulishwa rasmi Julai 4 2024 kuwa ni nyekundu na nyeupe.
KAGOMA
Yusuph Kagoma kiungo aliyekuwa ndani ya Singida Fountain Gate alitambulishwa ndani ya Simba kuwa ingizo jipya ilikuwa ni Julai 8 2024.
CHAMOU
Huyu ni beki anaitwa Karaboue Chamou alitambulishwa ndani ya kikosi Julai 7 2024
NOUMA
Beki mwingine ni raia wa Burkina Faso anaitwa Valentin Nouma alitambulishwa ndani ya Simba Julai 7 2024 kwa ajili ya changamoto mpya kwenye kikosi hicho
FERNANDES
Kiungo Debora Fernandes Mavambo mwenye uwezo wa kuchezesha timu akiwa na mpira ni ingizo jipya ndani ya Simba kuelekea msimu mpya wa 2024/25.
OMARY
Omary Abdalha huyu ni kiraka alitambulishwa ndani ya kikosi cha Simba Julai 6 akitokea Mashujaa FC.
KIJILI
Kelvin Kijili alitambulishwa rasmi ndani ya Simba Julai 12 2024 yeye ni beki.
AWESU
Julai 17 2024 ni kiungo mshambuliaji Awesu Awesu aliyekuwa KMC alitambulishwa ndani ya Simba kwa dili la miaka miwili.
PATACHIMBIKA ISHU YA KIBU

Kibu Dennis kiungo mshambuliaji wa Simba amerejea ndani ya kikosi na Agosti 2 alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa kwenye mazoezi ya mwisho kuikabili APR ya Rwanda. Ally amesema kuwa kiungo huyo amerejea na kutakuwa na adhabu juu yake kwa kuwa hakufuata taratibu.
“Kurejea mazoezini kwa Simba hakuondoi ukweli kwamba yeye bado ni mtoro hivyo Kibu Dennis lazima tumchukulie hatua za ndani ili kumkumbusha kwamba hii ni taasisi, kuwakumbusha wachezaji kuwa lazima waheshimu mikataba.
“Sisi tunamtambua kwamba yeye ni mtoro kwa kuwa aliondoka bila kufuata utaratibu. Utawala bado tunatambua kwamba Kibu ni mtovu wa nidhamu.”

