
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wameendelea kuteka mijadala mikubwa hapa nchini, ambapo achana na sakata lao la majibizano ya hojab na maneno dhidi ya Mzee Magoma, leo Alhamisi rasmi kikosi chao kimekwea pipa kwenda Afrika Kusini kwa ajili michezo ya kirafiki.
Kikosi cha Yanga ambacho kinadhaminiwa na Kampuni ya michezo ya Kubashiri ya SportPesa kimelazimika kukatisha kambi yake ya maandalizi ya kabla ya msimu ‘Pre-season’ ambayo ilikuwa ikiendelea Avic Town, Kigamboni Dar es Salaam.
Wakiwa nchini Afrika Kusini Yanga wanatarajiwa kucheza michezo mitatu ya kirafiki ambapo miongoni mwa timu watakazovaana nazo ni Augsburg kutokea nchini Ujerumani.
Mwaliko wa Yanga ni kutoka ndani ya kikosi cha timu ya Kaizer Chiefs ambao wamekuwa na mahusiano nao ya ukaribu katika masuala ya kiuongozi na uendeshaji wa klabu.
Msimu uliopita Kaizer Chiefs walialikwa na Yanga kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kuadhimisha kilele cha wiki ya Wananchi, mchezo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
YANGA NI WENYEJI SAUZ
Unaweza kusema licha ya ugeni wao wakiwa nchini Afrika Kusini, Yanga wanatarajia maisha ya uenyeji kwani ikumbukwe msimu uliopita Yanga walifanikiwa kuanzisha Tawi jipya linalofahamika kama ‘Tawi la Yanga Afrika Kusini’.
Hii ni wakati timu hiyo ilipoenda kuvaana na Mamelodi Sundowns Ijumaa ya Aprili 5, mwaka huu katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/24 ambapo Yanga waliingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya suluhu katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
INJIA HERSI ATOA TAMKO

Kufuatia tukio hilo, Rais wa Yanga Injina Hersi Said alisema: “Niweke rekodi sawa, sisi tuna matawi lukuki nje ya mipaka ya Tanzania. Kwa Mfano kule Marekani tunalo tawi la uanachama. Tunasisitiza mashabiki wetu nje ya Tanzania kutumia fursa hii ya kufungua account ya Tanzanite ya CRDB ambapo imetufanya kuwa karibu sana Wanachama wetu wa diaspora.
“Niwapongeze sana idara ya habari na Wanachama kwa kuweka mipango mikakati madhubuti ya kampeni ya ‘Twenzetu kwa Madiba’. Ama kwa hakika idara hizi mbili zina watu wenye upeo mkubwa wa maarifa wa kuanzisha agenda zenye dhima kwa Klabu.
“Nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana mashabiki wa wetu hapa Afrika Kusini na pia niwashukuru wadhamini ambao wamedhamini safari yetu ya Afrika Kusini.
ALICHOSEMA ALI KAMWE

Akizungumzia safari yao Ofisa habari wa timu hiyo, Ali Kamwe alisema: “Ukubwa wa timu yetu ndio umeifanya leo hii tumepata mialiko mikubwa nje ya Tanzania ambapo tunakwenda kucheza michezo ya kirafiki.
“Michezo hii kwetu ni sehemu ya maandalizi ya Kampeni yetu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ambapo malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunaandika rekodi ya kufika mbali katika mashindano hayo na ikiwezekana kushinda ubingwa.
“Kikosi chote kinasafiri na timu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huu, wakiwemo wachezaji wetu wapya ambao ni sehemu ya maboresho ya kikosi chetu kuelekea msimu ujao wa 2024/25.
“Tumewaambia waliotualika waandae utaratibu mzuri kwetu kwa ajili ya kurudi na kombe letu.”
KUHUSU JEAN BALEKE KUWEPO KWENYE MSAFARA WA YANGA
“Baleke hatujamtambulisha hivyo huenda watu wakawa wanamfananisha, lakini kuna mchezaji tutamtangaza lakini sio kwa sasa hatuna la kusema kuhusu mchezaji huyo, tunaomba muwe na subira.”
MSAFARA WA YANGA
Kuielekea ziara hiyo ya Yanga nchini Afrika Kusini sehemu ya mastaa ambao wamesafiri na kikosi cha timu hiyo leo Alhamisi ni kama ifuatavyo;
Makipa
Djigui Diarra
Aboutwalib Mshery
Khomeiry
Walinzi
Bakari Mwamnyeto
Ibrahim Bacca
Dickson Job
Yao Attohoula Kouasi
Nickson Kibabage
Chadrack Boka
Kibwana Shomari
Viungo;
Khalid Aucho
Salum Abubakar
Jonas Mkude
Mudathir Yahya
Maxi Nzengeli
Aziz Andembwile
Viungo washambuliaji
Pacome Peodoh Zouzoua
Stephane Aziz Ki
Farid Mussa
Denis Nkane
Clatous Chama
Duke Abuya
Washambuliaji
Clement Mzize
Kennedy Musonda
Prince Dube
Jean Baleke (Anasubiri kutambulishwa)

