KIMATAIFA KUMEKUCHA, WAPINZANI WA YANGA, AZAM, SIMBA, COASTAL 24/25

ByLunyamadizo Mlyuka

July 12, 2024
Kibu DennisKibu DennisKibu Dennis
Aziz- Pacome- Chama
Aziz- Pacome- Chama viungo wa Yanga 2024/25. Source:Yanga.

KIMATAIFA kumekucha baada ya wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kuwatambua wapinzani wao kwa msimu wa 2024/25 katika kusaka ushindi ndani ya uwanja baada ya droo kuchezwa Julai 11 2024 nchini Misri.

Tanzania ina timu nne ambazo zitakuwa kwenye anga la kimataifa kwa msimu wa 2024/25. Katika Ligi ya Mabingwa Afrika wapo mabingwa wa ligi Yanga inayodhaminiwa na SportPesa, matajiri wa Dar Azam FC.

Hawa wawili ambao wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika walimaliza katika nafasi mbili za juu. Yanga namba moja walisepa na pointi 80 huku Azam FC ikiwa na pointi 69 nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 30.

Simba ilikuwa nafasi ya tatu tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo. Coastal Union iligotea nafasi ya nne ikiwa na pointi 43 baada ya timu zote kucheza jumla ya mechi 30 msimu wa 2023/24.

Simba na Coastal Union hizi zitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Kwa sasa timu zote zipo kwenye maandalizi kuelekea msimu mpya ambapo Coastal Union hii inashiriki Kagame Cup huku Simba, Yanga na Azam FC hizi zipo kambini kuendelea na maandalizi.

HAWA HAPA KUKUTANA NA YANGA

GAMONDI
Kocha Mkuu wa Yanga 24/25 Miguel Gamondi. Source: Yanga.

Mabingwa wa Tanzania, Yanga chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi wao kwenye anga la kimataifa wataanzia ugenini dhidi ya Vital’O ya Burundi kusaka ushindi.

Mshindi wa matokeo ya jumla kati ya Yanga dhidi ya Vilal’O FC atakutana na mshindi wa matokeo ya jumla kati ya SC Villa ya Uganda dhidi ya Commercial Bank ya Ethiopia kwenye raundi ya kwanza.

Kazi kubwa inatarajiwa kufanyika kwa Yanga huku Gamondi akibainisha kwamba malengo makubwa ni kuona kwamba wanatinga hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tunatambua kwamba tunakazi kubwa kwenye ligi ya mabingwa Afrika lakini malengo makubwa ni kuona kwamba tunafika hatua ya makundi kwanza kisha mengine yatafuata. Hilo linawezekana kwa kuwa wachezaji wapo na wanatambua kuna kazi kubwa ya kufanya.”

MATAJIRI WA DAR AZAM FC HAPA

Fei Salum
Fei Salum kiungo mshambuliaji wa Azam FC 2024/25. Source: Azam FC.

Matajiri wa Dar, Azam FC wao wataanzia nyumbani kwenye mchezo wa hatua ya awali wakati Yanga wakianzia ugenini kusaka ushindi.  Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu Yusuph Dabo kete yake itakuwa dhidi ya APR FC ya Rwanda.

Aidha mshindi wa matokeo ya jumla kati ya Azam FC dhidi ya APR FC ya Rwanda atakabiliana na mshindi kati ya JKU FC ya Zanzibar dhidi ya Pyramids FC ya Misri kwenye hatua inayofuata.

HATUA YA AWALI

Vital’O  vs  Yanga

Azam FC  vs  APR FC

JKU FC  vs  Pyramids FC

SC Villa  vs  Commercial Bank

Mechi za mkondo wa kwanza wa hatua ya awali zinatarajiwa kuchezwa kati ya Agosti 16 – 18 huku marudiano yakitarajiwa kuchezwa kati ya Agosti 22 – 25, 2024.

Mechi mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza zitapigwa kati ya Septemba 13-15, 2024 huku marudiano yakitarajiwa kupigwa kati ya Septemba 20-22, 2024.

NGOMA NA FEI
Fabrince Ngoma na Feisal Salum wa Azam FC kwenye kazi 2023/24. Source: Simba.

MNYAMA KWENYE KOMBE LA SHIRIKISHO

Mnyama Simba kwenye anga la kimataifa kete yake itakuwa dhidi ya mshindi wa mchezo  kati ya Uhamiaji ya Zanzibar au Bingwa wa FA ya Libya, Libya 1 kwenye raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/25.

Uhamiaji ya visiwani Zanzibar imepangwa dhidi ya wawakilishi hao kutoka Libya katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ambapo mshindi wa matokeo ya jumla atakutana na Mnyama kwenye raundi ya kwanza.

Ikumbukwe kwamba Simba imeweka kambi nchini Misri haitaanzia kwenye hatua ya awali hivyo itakuwa ikimsubiri mshindi mmoja kwenye mchezo huo kupambana naye kupata nafasi ya kusonga mbele kimataifa.

Kutoka Tanga, Coastal Union yenyewe ina kazi ya kusaka ushindi dhidi ya FC Bravos ya Angola kwenye hatua ya awali ambapo mshindi wa matokeo ya jumla atachuana na Fc Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Timu mbili kutoka Tanzania zitapeperusha bendera kwenye anga la Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ni Simba na Coastal Union.

Yanga na Azam FC hizi timu mbili zitakuwa kwenye anga la kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na zote zitaanzia hatua ya awali ambapo Julai 11 2024 droo ilichezwa nchini Misri na kila timu ikamtambua mshindani wake.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari Simba ameweka wazi kuwa wanatambua kwamba ushindani ni mkubwa kimataifa watafanya maandalizi mazuri kupata matokeo chanya.

“Kimataifa kazi ni kubwa na kila mmoja anatambua namna ambavyo ushindani upo. Tutafanya maandalizi mazuri kuwapa furaha Wanasimba na kufikia malengo yetu.”

 

Share this: