
SIMBA hakuna aliye salama ndivyo unavyoweza kusema kwani kumekuwa na mfululizo wa shukrani ‘Thank you’ au mkono wa kwaheri kwa mastaa wote ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao wa 2024/25.
Haya yote yanaendelea katika kipindi ambacho tajiri wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘MO’ kutangaza kurejea na kujihusisha moja kwa moja na timu hiyo katika kuhakikisha anarejesha utawala ambao walikuwa nao misimu minne iliyopita.
MO ameahidi kuisuka upya timu hiyo kwa kuachana na mastaa wote ambao wanahisi hawawezi kuirudisha timu hiyo kwenye makali.
BOCCO, SAIDO WAFUNGUA PAZIA

Katika harakati za maboresho hayo ya kikosi cha Simba tayari mastaa wawili wameagwa ambao ni nahodha wao, John Bocco na kiungo Saido Ntibazonkiza.
Bocco anayetajwa kuwa mshambuliaji bora wa muda wote akifunga zaidi ya mabao 100 kwenye Ligi Kuu Bara amemaliza utumishi wake ndani ya Simba kama mchezaji.
Nyota huyo Mei 28, mwaka huu kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Bocco aliweka chapisho akiwa na jezi ya Simba na kuandika ujumbe wa kuaga ameagwa rasmi na Simba Juni 17, mwaka huu.
Said Ntibanzokiza ambaye msimu uliopita alimaliza kama mfungaji bora na mabao yake 17, msimu huu pia aliibeba Simba mabegani baada ya kumaliza msimu akiwa kaweka kambani mabao 11 akiwa ndiye mfungaji bora wa kikosi hicho.
Nyota huyo akiwa na Simba ambao wamewahi kulamba dili la udhamini wa Kampuni boa SportPesa ndio alikabidhiwa jukumu la kupiga mipira ya adhabu kubwa yaani Penalti, ambapo alifanikiwa kuweka kambani mabao 7, idadi ambayo ni kubwa zaidi kwa mapigo ya Penalti.
FRED AIWEKA NJIA PANDA SIMBA

Huku panga hilo likiendelea straika wa Simba, Fredy Michael, ameonekana kuwagawa wadau wa michezo ikiwa anastahili kubaki au naye apewe Thank You.
Miongoni mwa wadau ambao wametoa maoni yao juu ya Fred ni mchambuzi, Edo Kumwembe ambaye amenukuliwa akisema: “Rafiki yangu Ahmed Ally wakati akijitamba na vifaa ambavyo vilitua Januari alimpachika jina la ‘Fungafunga’ mshambuliaji Fred Michael.
“Wakati huo tulikuwa hatujamuona uwanjani. Jina lilitokea mazoezini. Kama sio mazoezini basi alikuwa amelichukua kutokana na mabao aliyofunga Zambia.
“Baada ya hapo Fredy ametuchanganya akili. Kila tulipomuona uwanjani alituchanganya akili. Mpaka nyakati hizi nikiwasikiliza Wanasimba wenyewe wanajikuta wamechanganyikiwa kwa Fredy, hasa nyakati hizi ambazo Simba inataka kutoa ‘Thank You’ kwa wachezaji wake.
“Fredy aondoke au abaki? Kuna Wanasimba wanasema aondoke kuna ambao wanataka abaki. Tunaishi katika dunia ya namba. Kule alikoondoka amebakia kuwa mfungaji bora na hapa nchini tangu afike amefikisha mabao kumi katika michuano yote.
“Sio haba. Mara ya kwanza nilipomuona Fredy sikuona kama mshambuliaji wa maana. Lakini anafunga. Hapo ndipo anaponifunga mdomo. Mara ya pili nilipomuona sikuona kama alikuwa mchezaji tishio lakini alifunga.
“Kuna mechi anacheza ovyo anatukanwa kuliko mchezaji yeyote uwanjani lakini mechi inayofuata anafunga. Wakati mwingine nilikuwa namtazama na kuanza kuhoji ubora wa Ligi ya Zambia.
“Ilikuwaje akawa anacheka na nyavu pale Zambia mpaka ikafikia hatua ya kuwa mfungaji bora wakati Simba ilipokuwa inamchukua. Na hapo hapo unawaza namna ambavyo hata washambuliaji wengine wa Ligi hiyo walishindwa kumfikia wakati alipoondoka. Tumeanza kuwaacha Wazambia kiuwezo?
“Kati yake na Pah Omary Jobe unaona wazi kwamba tofauti yao ni mabao. Hauwezi kuwaamini kama washambuliaji lakini kinachomtofautisha Fredy na Jobe ni kwamba Fredy anafunga.
“Na sasa ametuachia mtihani wa kukata jina lake. Unajaribu kuangalia na kujiuliza, Simba wapo tayari kuusaka ubingwa wa Afrika huku mshambuliaji akiwa Fredy?”
“Nadhani kinachopaswa ni kumpa muda zaidi lakini Simba ni lazima wasajili straika mwinginge hatari, kwa kuwa hauwezi kwenda kwenye mashindano ya Afrika straika wako tegemeo akiwa ni Fred pekee.
“Ni lazima uhakikishe unakuwa na straika anayeweza kuongoza ushindani katika sauala la kufunga mabao, straika huyo ni lazima awe bora kuliko daraja la Fred Fungafunga hapo ndio suala la fainali ya Afrika linaweza kuwezekana.”

