
YANGA hii sasa sifa unaweza kusema hivyo kutokana na kukomba mataji yote makubwa ndani ya msimu wa 2023/24 walianza na Ligi Kuu Bara kwa kuwapoteza washindani wake 15 wakafunga na CRDB Federatin Cup kwenye mchezo wa funga msimu mbele ya Azam FC.
Miguel Gamondi Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kikubwa ambacho kilikuwa kinatakiwa kwenye mechi zao zote za 2023/24 ni matokeo mazuri na kucheza mchezo wa kutoa burudani kwa mashabiki wao.
Ipo wazi kwamba Yanga ni mabingwa wa CRDB Federation Cup wakipata ushindi mbele ya Azam FC matajiri wa Dar ambao walikuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa taji hilo bahati haikuwa yao. Kwenye mchezo huo dakika 120 zilikuwa za kazi nzito kwenye kutafuta taji hilo.
Jumapili ya kwanza Juni 2 ilikuwa Uwanja wa New Amaan Complex, dakika 90 za mwanzo ziligota mwisho ubao ukisoma Azam FC 0-0 Yanga na dakika 30 nazo ngoma ilikuwa vilevile kwa timu zote hivyo ndani ya dakika 120 ngoma ilikuwa nzito kwa kuwa nyavu hazikutikisika.
Ikumbukwe kwamba kipa wa Azam FC, Mohamed Mustafa alikuwa kwenye kiwango bora katika dakika 120 kwa kuwa alikuwa akipambana kuokoa michomo ya hatari ya Yanga kutoka kwa miamba waliokuwa wakiongozwa na Aziz KI mfungaji bora ndani ya ligi akiwa na mabao 21 na Clement Mzize mfungaji bora CRDB Federation akiwa kafunga mabao matano.
Miongoni mwa hatari ambazo aliokoa ilikuwa ni dakika ya 25, 27, 31, 51, 77, 107 na alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Ahmed Arajiga dakika ya 77 kwa kile alichotafsri kuwa anapoteza muda kwenye mchezo huo uliokuwa na kasi mwanzo mwisho.
NENO LA MASTA GAMONDI

Gamondi amesema: “Kikubwa kwenye mechi zetu ambazo tulikuwa tunacheza ambacho tunahitaji ilikuwa ni ushindi na kufanya vizuri hilo lilikuwa jambo la kwanza na tumefanikiwa.
“Kwenye penalti baada ya wachezaji wawili kukosa, bado tulikuwa na imani kwamba haijaisha mpaka iishe na mwisho tumefanikisha malengo tukitwaa ubingwa hii ni furaha kwetu.
“Ulikuwa ni mchezo mgumu na mkubwa lakini wachezaji walijituma katika kutimiza majukumu yao. Furaha kwa kila mmoja mashabiki na wachezaji kuona kwamba tumefanikiwa kutwaa taji hili. Niliwaambia wachezaji kwamba ni lazima watulie kwa kuwa fainali ni mchezo wa maamuzi.
“Pongezi kwa kila mmoja alivyohusika kwenye mchezo wetu na tunaamini kwamba hii ni zawadi nzuri. Niliweka wazi kuwa miongoni mwa timu ambazo zinacheza mchezo mzuri ni pamoja na Yanga hilo lipo wazi na limeonekana pia.”
HIVI NDIVYO AZAM FC WALIPISHANA NA TAJI
Azam FC walipata penalti 5-6 Yanga ambao ni mabingwa wapya wa CRDB Federation Cup msimu wa 2023/24. Kwenye penalti Yanga walianza kukosa kupitia kwa Aziz KI na mpigaji wa pili pia ambaye ni Joseph Guede alikosa baada ya mikono ya Mustapha Mohamed kufanya kazi yake.
Kwa wapigaji wawili wa mwanzo Azam FC walifunga ni Adolf Mutasiga na Sidibe na mpigaji wa tatu kwa Azam FC ambaye alikuwa wa kwanza kukosa alikuwa ni Yusuph Foutens.
FEI TOTO NA REKODI YAKE

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum anaingia kwenye orodha ya wachezaji waliokomba dakika zote 120 kwenye mchezo huo. Fei ambaye aliibuka ndani ya Azam FC alikuwa kwenye kiwango bora lakini alishindwa kufunga kwenye muda wa kawaida kama ilivyokuwa kwa mwamba Aziz KI.
Ikumbukwa kwamba Fei ni namba moja kwa watupiaji ndani ya kikosi cha Azam FC akiwa katupia mabao 19 kwenye ligi. Aziz Ki yeye ni mabao 21 katupia ndani ya ligi akiwa ni namba moja kwa Yanga na kwa wachezaji wote kiujumla ndani ya msimu wa 2023/24.
Katika changamoto za penalti, Fei alimtungua kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra huku Aziz Ki pigo lake la penalti likiokolewa na kipa wa Azam FC kwenye mchezo huo uliowavuta mashabiki wengi kutoka pande zote bara na visiwani.
YANGA BABA LAO

Ushindi huo kwa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa unawapa taji la nne wakiwa ni namba moja kwa timu iliyotwaa mataji mengi ya CRDB Federation Cup ambapo awali ilikuwa inaitwa Azam Sports Federation kwa sasa ina wadhamini wapya na timu ya kwanza kutwaa taji hilo ni Yanga.
Simba watani za jadi wa Yanga wao walitwaa taji hilo mara tatu tayari rekodi yao imeshavunjwa. Ikumbukwe kwamba safari hii Simba ilifungashiwa virago na Mashujaa ya Kigoma hivyo walikuwa wafuatiliaji nani ataibuka kuwa bingwa kati ya Azam FC na Yanga.
Ipo wazi kwamba mbali na kuwa baba lao kwenye upande wa CRDB Federation Cup mpaka kwenye mataji ya ligi ni namba moja. Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ina mataji 30 ya ligi ikifuatiwa na Simba yenye mataji 22 huku Azam FC ni taji moja la ligi inalo kabatini.

