
MAJINA ya Aziz Ki na Clatous Chama kwa mara nyingine yameendelea kutikisa vyombo vya habari ndani na nje ya Tanzania, wakati huu ni kuelekea dirisha kubwa la usajili ambalo kwa kawaida linatarajiwa kufunguliwa ndani ya mwezi ujao.
Kwa sasa kalenda ya msimu huu imesaliwa na mchezo mmoja tu wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB Bank ambao unatarajiwa kupigwa siku ya Jumapili kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Wachezaji wetu saba wameitwa katika timu zao kwa ajili ya kujiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Dunia mapema mwezi ujao.
KUHUSU AZIZ KI
Mara baada ya kuwa na msimu bora akiibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kuweka kambani mabao 21, taarifa kutoka ndani ya Yanga wanaotamba na udhamini wa Kampuni ya michezo ya SportPesa zinaeleza kuwa uongozi wa timu hiyo unapambana kumbakisha Aziz anayemaliza mkataba wake huku wakikutana na upinzani mkubwa kutoka timu mbalimbali za ndani na nje ya Bara la Afrika.
Taarifa zinaeleza kuwa muda wowote kuanzia sasa viongozi wa Yanga wanatarajiwa kukutana na wawakilishi wa Aziz Ki, ili kuanza mazungumzo ya kuweka ofa yao mpya mezani.
Imeelezwa kuwa Aziz Ki yuko tayari kubaki Yanga kwani anavutiwa na mazingira ya timu hiyo ikiwemo mashabiki wa timu hiyo na ardhi ya Tanzania.
Tayari wakala wa Aziz Ki, anayefahamika kama Mr Zambro ameonekana visiwani Zanzibar kwa ajili ya kushuhudia mchezo wa fainali ya CRDB Bank Federatin Cup lakini taarifa za ndani zimethibitisha kuwa yupo huko kwa ajili ya mazungumzo ya mkataba mpya.
KUHUSU CLATOUS CHAMA

Hali sio shwari miongoni mwa viongozi wa Simba ambapo inaelezwa kuwa wamekuwa na misimamo tofauti kuhusu mpango wa kumbakisha Chama Simba.
Imeripotiwa kuwa upande mmoja unataka kumbakisha Chama, huku upande wa pili ukiamini ni muda rasmi sasa Chama na baadhi ya wachezaji wakongwe wanatakiwa kuondoka na kusajili mastaa wapya ambao ni vijana.
Mgongano huu unaonekana kuwafaidisha Yanga ambao wanatajwa kuwa wamemalizana kila kitu na Chama na kwa sasa inasubiriwa asaini tu, mkataba huo.
MGUNDA AONDOKA NA MASTAA 7 SIMBA
Wakati sehemu kubwa ya mastaa wa Simba wakielekea makwao kwa ajili ya mapumziko ya mwishoni mwa msimu Kaimu, Kaimu kocha Mkuu wa Simba na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Juma Mgunda alitarajiwa kuwahi mchezo wao wa kwanza wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Indonesia unaotarajiwa kuchezwa Juni mbili mwaka huu.
Mgunda ameondoka nchini leo akiongozana na baadhi ya wachezaji kwenda kuungana na timu ya Taifa ambayo ipo nchini Indonesia kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu ushiriki wa Kombe la Dunia dhidi ya Zambia.
Mgunda amesema: “Nilisafiri na baadhi ya wachezaji ambao ni nahodha, Mohammed Husein ‘Tshabalala’, kipa Ally Salim na Edwin Barua kuelekea huko, tayari kwa ajili ya maandalizi ya kuwavaa Zambia kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia.
“Hatukupaswa kuwa na muda wa kupumzika kwa sababu mchezo upo karibu na kuna wengine wametangulia huko, hivyo naamini kuongezeka kwetu tukiwasubiri wengine kutoka Azam FC na Yanga kutaongeza nguvu kikosini,” amesema Mgunda.
Kutoka Simba nyota saba wameitwa kwenye timu za Taifa, watano wameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayojiandaa na mchezo dhidi ya Zambia ambapo wawili ni kutoka mataifa ya nje. Wengine ni washambuliaji Edwin Balua na Kibu Denis.
Kwa upande wa wachezaji wa Kimataifa walioitwa kwenye timu zao za Taifa ni Henock Inonga (DR Congo) na Sadio Kanoute wa (Mali).
FEI TOTO AKUBALI MZIKI WA AZIZ KI

Kufuatia mafanikio ambayo ameyapata Aziz Ki msimu huu, kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amempongeza mshindi huyo wa tuzo ya ufungaji bora msimu huu baada ya kupachika mabao 21 huku akiweka wazi kuwa alistahili.
Fei Toto ambaye amemaliza msimu na mabao yake 19 akiachwa mabao mawili na kinara huyo ambaye walikuwa wanakimbizana kwenye ushindani mpaka siku ya mwisho ya kufungwa kwa ligi, amesema licha ya kukosa kiatu cha dhahabu msimu huu anafurahi kuipambania timu yake kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Nampongeza Aziz Ki kwa kufanikiwa kutwaa kiatu cha dhahabu, alistahili kutokana na namna ambavyo amepambana, na mimi pia licha ya kukikosa ninafuraha kuipeleka Azam FC Ligi ya Mabingwa nafasi ambayo ndio ilikuwa katika malengo yetu msimu huu,” amesema na kuongeza
“Haikuwa rahisi, nafurahi mimi pia pamoja na kuipeleka Azam FC kimataifa nilionyesha ushindani kwenye mapambano ya kiatu, bahati haikuwa yangu kwani mchezo wa mwisho pia kafunga na mimi nimefunga lakini amekuwa bora kwasababu yeye kafunga mabao matatu mimi nimefunga moja ambalo lilikuwa muhimu na la faida,” amesema.

