- Simba kujipanga upya kurejea kwenye ubora kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri hivi karibuni
- Dakika 180 za kimataifa mateso matupu ilikuwa nje ndani dhidi ya Al Ahly
- Jambo kubwa linasukwa kwa ajili ya kurejea kwenye ubora kwa Mnyama

UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa utarejea kwenye ubora wake licha ya kutokuwa na mwendo mzuri kwenye mechi za ushindani ndani ya msimu wa 2023/24 katika mechi ambazo wanacheza kitaifa na kimataifa.
Ipo wazi kwamba Simba kwenye upande wa kufanya vizuri kwenye mechi ambazo inacheza kwa wakati huu imekuwa ni mwendo wa kinyonga jambo ambalo linawapa maumivu mashabiki kila wakati pamoja na viongozi.
Ikumbukwe kwamba inapambania Ligi Kuu Bara ambalo mabingwa watetezi ni Yanga inayodhamiwa na Kampuni ya SportPesa nao wameweka wazi kuwa wanahitaji taji hilo hivyo vita ni kali kila kona kwa timu zote kupambana kufanya vizuri ndani ya uwanja.
WAMEGOTEA ROBO FAINALI KIMATAIFA

Katika anga la kimataifa ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwendo wameumaliza baada ya kugotea hatua ya robo fainali LigI ya Mabingwa Afrika hivyo ni maumivu mengine kwa kuwa hakuna timu itakayoendelea kwa sasa kutoka Tanzania.
Ipo wazi kwamba watani zao wa jadi pia Yanga walikuwa kwenye anga la kimataifa lakini mwendo wao pia uligotea hatua ya robo fainali baada ya kufungashiwa virago na Mamelodi Sundowns kwenye mchezo wa mkondo wa pili uliochezwa nchini Afrika Kusini.
Simba wao walifungashiwa virago na Al Ahly klabu namba moja kwa ubora Afrika ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Hivyo Al Ahly wanakwenda hatua ya nusu fainali na Simba wakigotea hatua ya robo fainali.
DAKIKA 180 NI MATESO

Ngoma ilikuwa nzito kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly kwa kuwa mechi zote mbili ambazo ni dakika 180 Simba ilipoteza nje ndani ikiambulia mateso mwanzo mwisho kwa kufungwa kuanzia mkondo wa kwanza Uwanja wa Mkapa na ule mkondo wa pili wakiwa Uwanja wa taifa wa Cairo.
Mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa Dar mbele ya mashabiki wao waliojitokeza kwa wingi ubao ulisoma Simba 0-1 Al Ahly ambapo Simba walitengeneza nafasi nyingi walishindwa kuzitumia wakiwa nyumbani.
Kete ya pili ugenini ilikuwa ni ngumu kwa Simba kutusua baada ya dakika 90 ubao ulisoma Al Ahly 2-0 Simba hivyo hawajafanikiwa kupata hata bao Simba kwenye hatua ya robo fainali dhidi ya Al Ahly, Waarabu wa Misri.
Watakuwa ni mashuhuda wa bingwa mpya kwa mara nyingine tena kwa kuwa hawana tiketi ya kuendelea kuwa kwenye anga la kimataifa kwa sasa kama ilivyo kwa watani zao wa jadi Yanga.
NYUMBANI MAJANGA PIA
Majanga mengine kwenye CRDB Federation Cup wamekwama kutinga hatua ya robo fainali wakigotea hatua ya 16 bora wakifungashiwa virago na Mashujaa ya Kigoma kwenye mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mwisho wa reli Kigoma baada ya dakika 90 ubao ulisoma Mashujaa 1-1 Simba ambapo bao la Mashujaa ilikuwa mapema dakika ya 5 mtupiaji akiwa ni Relliats Lusajo na lile la Simba mwamba Fred Michael yeye alifunga dakika ya 52.
Kufuatia kutoshana nguvu mshindi alipatikana kwa mikwaju ya penalti ambapo ilikuwa Mashujaa 6-5 Simba. Matokeo hayo yanaipa nafasi Mashujaa ya Kigoma kutinga hatua ya robo fainali CRDB Federation Cup ikiungana na Yaga iliyopata ushindi dhidi ya Dodoma Jiji.
MSIKIE AHME ALLY
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa wanatambua matokeo ambayo wanayapata kwa wakati huu sio mazuri wanafanya kazi kubwa kurejea kwenye ubora wao.
“Kabisa matokeo ambayo tunayapata sio mazuri yaani hayafurahishi hata kidogo kwa kweli tunalitambua hilo lakini tunaamini kwamba tutarudi kwenye uimara wetu na kufanya kazi kubwa kwenye kutafuta matokeo.
“Mashabiki wa Simba ninawapa pole nyingi na kubwa kutokana na haya ambayo yanaendelea ila yana mwisho. Unajua hakuna ambaye hapendi kufurahi hakuna ambaye hapendi matokeo mazuri ni mwanzo ambao unamaanisha kwamba kuna kitu kizuri kwa ajili yetu kinakuja.
“Nguvu iwe ni moja na tuzidi kushikama kwakuwa hizi ni nyakati ambazo tunapaswa kushirikiana kwa kila namna kufikia malengo yetu. Wanasimba letu liwe moja kuwa pamoja na tunaamini kwamba kila kitu kitakuwa sawa.
“Wachezaji wanapenda kufanya kazi kwa umakini, makosa ambayo yanatokea nina amini kwamba tutayafanyia kazi ili kurejea tukiwa imara ndani ya uwanja kitaifa na kimataifa,”.

