- Yanga wanaitaka mechi yao kimataifa hatua ya robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini
- Mzunguko mashabiki washindwe wao hakuna uchakavu hata wa shilingi ni bure kabisa
- Siku ya wapinzani wa Yanga kutua Bongo yawekwa hadharani
UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa unaitaka mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ili kupata ushindi nyumbani kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali Machi 30 2024 Uwanja wa Mkapa.
Mchezo huo unasubiriwa kwa shauku kubwa kutokana na ubora wa timu zote mbili Yanga inayodhamiwa na SportPesa ndani ya ligi wakiwa wanaongoza huku wakikutana na wapinzani wao wenye kasi na matumizi makubwa ya nguvu ndani ya uwanja kwenye kusaka ushindi.
Ipo wazi kwamba ni timu mbili kutoka Tanzania zipo hatua ya robo fainali ikiwa ni Simba itakayokabiliana na Al Ahly ya Misri pamoja na Yanga ambayo itakuwa na kazi dhidi ya timu kutoka Afrika Kusini.

Ali Kamwe Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga ameweka wazi kuwa wanataka kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo kutokana na mipango waliyonayo kwenye mashindano ya kimataifa.
“Tunaitaka mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Mamelodi licha ya kwamba wengi hawatupi nafasi ya kufanya vizuri hilo tunalijua lakini tunaamini kwamba baada ya mchezo tukipata ushindi watakuja kueleza jambo jingine ambalo litakuwa limewashangaza,”.
JEZI YA YANGA MIKONONI MWA RAIS

Machi 22 2024 Yanga ikiwa kwenye maandalizi kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika ilimkabidhi jezi Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania pamoja na Makamu wake wa kwanza.
Yote haya ni kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa Machi 29 Uwanja wa Mkapa ambapo Yanga inapeperusha bendera ya Tanzania kimataifa kwenye hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alikuwa ni Meneja wa Habari na Mawasiliano Yanga, Ali Kamwe ambaye alikabidhi jezi ya Wananchi kwa Rais wa TFF, Wallace Karia na Makamu wake wa Kwanza, Athuman Nyamlani kwa ajili ya mtoko wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga itakuwa nyumbani kuvaana na Mamelodi Sundown ikiwa ni hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika. Ikumbukwe kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kutinga katika hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo mpango wao ni kupata matokeo mazuri.
MZUNGUKO NI BURE KABISA
Kwa upande wa viti vya mzunguko ambavyo vinabeba mashabiki wengi zaidi uongozi wa Yanga umebainisha kwamba ni bure kwa Watanzania wote na wale wanaopenda soka kuelekea kwenye mchezo huo.
Ipo wazi kwamba mchezo huo unatarajiwa kuwa na mashabiki wengi kutokana na ukubwa wa timu zote mbili zinazokutana uwanjani kwa kila mmoja kubainisha kwamba anahitaji kupata ushindi ndani ya dakika 90.
Kuhusu hilo Kamwe amebainisha kwamba wanatambua umuhimu wa mashabiki na umuhimu wa mchezo huo jambo ambalo limewafanya wakaondoa viingilio kwa upande wa eneo la mzunguko ili mashabiki wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu ya Wananchi.
“Viongozi wa Klabu yetu hawana tamaa ya fedha, ndio maana tumepunguza na kuondoa tiketi ya mzunguko kwa lengo la kuhakikisha wengi wanakuja Uwanjani. Tumeweka maslahi ya mpira wa Tanzania mbele.
“Mechi ya Mamelodi ni kubwa mno lakini kwa kuwa lengo sio fedha ni hamasa basi tunawasihi mashabiki kujitokeza kwa wingi. Kiasi cha fedha ambacho ungelipia tiketi ya mzunguko basi utatumia kama nauli ya usafiri wa kukufikisha uwanjani na baada ya mchezo wetu uweze kurudi nyumbani salama
“Wote tunakubaliana mechi ya Mamelodi ni mechi kubwa zaidi kwenye robo fainali ya CAFCL msimu huu na viingilio ni kama vifuatavyo: VIP C 10,000 VIP B 20,000, VIP A 30,000. Mashabiki tunaomba wajitokeze kwa wingi upande wa usalama tuna imani kabisa na vyombo vya ulinzi vimekuwa vikifanya kazi kubwa nasi tumekuwa tukishirikiana nao kuona kila kitu kinakwenda sawa,”.
MAMELODI WANATUA NAMNA HII
Kuhusu wapinzani wa Yanga Mamelodi kutua nchini bado haijawekwa wazi itakuwa ni lini lakini ni mapema ndani ya wiki wapinzani hao wanatarajiwa kuwasili Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo wa hatua ya robo fainali.
Kamwe amebainisha kwa kuweka wazi kuwa: “Mechi yetu na Mamelodi Sundowns itachezwa majira ya saa tatu usiku itakuwa ni Machi 30 2024 maandalizi yanaendelea na wapinzani wetu Mamelodi wataingia nchini siku ya Machi 28 2024 majira ya saa moja usiku wanatarajiwa kuwasili.
