
Willy Essomba Onana kiungo wa kimataifa wa Simba raia wa Cameroon amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuelekea mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Ijumaa hii.
ONANA AWAKILISHA MASTAA KAMBINI ZANZIBAR

Onana ni sehemu ya mastaa wa Simba ambao wapo na kikosi cha timu hiyo ambayo imeweka klambi ya muda ya kujiandaa na mchezo huo muhimu.
Kuendana na droo ya Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilifanyika Machi 12, mwaka huu huko kwenye makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), nchini Misri, mchezo wa kwanza wa Simba utapigwa Ijumaa ya Machi 29, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa saa tatu usiku.
Mara baada ya mchezo huo wa kwanza, mchezo wa marudiano utapigwa Aprili 5, jijini Cairo nchini Misri na mshindi wa jumla atasonga mbele na kutinga nusu fainali.
Droo hiyo ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilimefanyika mara baada ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumalizika kwa Tanzania kuandika rekodi ya kuwa Taifa pekee ambalo limefanikiwa kutoa timu mbili ambazo zimefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali.
Simba ilifanikiwa kufuzu kutokea kundi B la mashindano hayo wakimaliza kwenye nafasi ya pili na pointi zao tisa ambazo wamekusanya katika michezo sita. Kutoka kwenye kundi lao ni wao na Asec Mimosas ya Ivory Coast ndio wamefuzu Robo Fainali.
ALICHOSEMA ONANA
Akizungumzia maandalizi yao kuelekea mchezo huo, Onana amesema kikosi chao kinaendelea vizuri na kambi hiyo ya siku saba kujiandaa na mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Machi 29, mwaka huu huku wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
“Tangu tumewasili Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya siku saba kujiandaa na mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, tumekuwa na maendeleo mazuri.
“Binafsi hii kwangu ni mara ya kwanza nacheza hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na niko tayari kujitoa kwa kila hali kuhakikisha timu yangu inapata matokeo ya ushindi.
“Tunafahamu Al Ahly ni timu bora sana hasa inapokuwa kwenye hatua kama hii, hivyo ni lazima tuwaheshimu lakini pia tutambue hii ni nafasi yetu ya kuandika historia mpya.
“Mara kadhaa tumefika hatua ya Robo Fainali na kutolewa, nadhani sasa ni muda wa kupiga hatua moja mbele zaidi.
“Kama ambavyo nimesema nimejiandaa kujitoa kwa kila hali kuhakikisha Simba inaenda nusu fainali, kuhusu nani atacheza hilo ni jukumu la kocha kuendana na mbinu zake, lakini kazi yetu sisi wachezaji ni kuwa tayari, hata nikipewa dakika tano au moja nitahakikisha napambana,” amesema Onana.
SIMBA: MALENGO NI NUSU FAINALI

Uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa utaingia katika mchezo huo wakiwa na kiu kubwa ya kuvuka hatua ya robo fainali na kutinga nusu fainali ya michuano hii mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika.
Uongozi wa Simba pia umeweka wazi kuwa unafahamu Al Ahly ni timu yenye historia kubwa barani Afrika kwa kuchukua taji hili mara nyingi, huku wakiweka wazi kuwa safari hii watavuka.
KUMBUKUMU YA REKODI ZA ROBO FAINALI KWA SIMBA
Hii ni Robo fainali ya nne ya Ligi ya Mabingwa katika kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2019. Ikumbukwe mwaka 2020 ndio mwaka pekee ambao Simba haikutinga robo fainali ya michuano hii.
Haya hapa matokeo ya mechi tatu za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Simba zilizopita.
- Aprili 6, 2019
Simba 0 -0 Tp mazembe
Mechi ya marudiano Aprili 13, 2019
Tp mazembe 4 -1 Simba
- Mei 15, 2021
Kaizer Chiefs 4-0 Simba
Mechi ya marudiano Mei 22, 2021
Simba 3 -0 Kaizer Chiefs
- Aprili 22, 2023
Simba 1 -0 Wydad Casablanca
Mechi ya marudiano Aprili 28, 2023
Wydad 1-0 Simba
Penati 4-3
