Ngoma nzito

 

LIGI Kuu Bara 2023/24 mzunguko wa pili ngoma ni nzito dakika 90 za kazikazi, ukizubaa unapigwa.

Yanga waendeleza ubabe wao mbele ya Namungo dakika 180 wapoteza pointi sita. 

Simba yapiga mkwara wa maana baada ya kuwatuliza Coastal Union.

NGOMA nzito ndani ya Ligi Kuu Bara kwa kila timu kuvuja jasho ndani ya uwanja dakika 90 kusaka pointi tatu kwenye mechi ambazo wanacheza uwanjani ili kufikia malengo ambayo yapo kwenye timu hizo.

Ipo wazi kwamba mabingwa watetezi ndani ya ligi ni Yanga inayodhamiwa na Kampuni ya SportPesa mzunguko wa pili kwenye mechi zake ilizocheza uwanjani imekuwa na mwendo mzuri wa kupata matokeo chanya.

Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kwenye mchezo wao uliopita Ijumaa iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo ikiwa ugenini, Uwanja wa Majaliwa.

Kwenye mchezo huo dakika 45 za mwanzo ngoma ilikuwa ngumu kwa timu zote ambapo hakuna ambaye alifunga bao mambo yalibadilika kipindi cha pili Yanga walipokuja kwa kasi.

NGOMA ZILIBAILI UPEPO YANGA

Mudathir Yahya
KIUNGO wa Yanga Mudathir Yahya akiwa na mshambuliaji Clement Mzize wakishangilia moja ya bao walilofunga kwenye mchezo wa ligi. Source:Yanga

Nyota Mudathir Yahya alibadili upepo kipindi cha pili kwa kufunga bao la ufunguzi kisha Clement Mzize na Aziz KI wote walifunga bao mojamoja na kwa upande wa Namungo walipata bao kutoka kwa beki Ibrahim Bacca ambaye alijifunga katika harakati za kuokoa.

Upepo ulibadilika na kufanya ngoma nzito kwa Namungo kuambulia angalau pointi moja ikiwa nyumbani mwisho ikapishana na pointi tatu mazima.

SIMBA WAZINDUKA HUKO MKWAKWANI

Wakiwa na machungu ya kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya  Tanzania Prisons uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Machi 6 2024 ambao unakuwa ni wa pili kwao msimu wa 2023/24 kupoteza baadaya ubao kusoma soma Simba 1-2 Tanzania Prisons waliibuka Mkwakwani.

Kwenye mchezo huo wakiwa nyumbani mabao yote mawili ya Wajelajela yalifungwa na Samson Mbangula na lile la Simba mali ya Fabrince Ngoma ambaye ni kiungo wa kazi.

Machungu yao yaligotea pale Uwanja wa Mkwakwani, ubao ulisoma Coastal Union 1-2 Simba ilikuwa ni Machi 9 2024 huku mabao yakifungwa na Michael Fred na Willy Onana ambaye alianzia benchi kwenye mchezo huo na alipishana na Saido Ntibanzokiza.

ONANA
KIUNGO mshambuliaji Willy Onana akifunga bao kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Source Simba

Ikumbukwe kwamba bao la Coastal Union lilifungwa na Lukas Kikoti kwa shuti kali akiwa nje ya 18 likamshinda mlinda mlango Ayoub Lakred ambaye hakuwa na chaguo la kufanya zaidi na mpira huo.

SIMBA WENYEWE WANASEMAJE

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameweka wazi kuwa ukali wa Simba ni uleule licha ya kupoteza hivyo wapinzani wao wasiwachukulie poa.

“Ubora wa Simba ni uleule, kasi ya Simba ni ileile siku zote kwa kuwa tuna hasira kwelikweli kwenye mechi ambazo tunacheza. Wapinzani wetu wasituchukulie poa unajua kupoteza mchezo wetu dhidi ya Tanzania Prisons haina maana kwamba ubora umepungua hapana ile ilikuwa ni kuteleza lakini mnyama ni mkali vibaya sana.

“Kwenye mechi ambazo zinafuata tutaendelea kupambana kupata pointi tatu kwa kuwa tunahitaji kushinda mechi zetu ambazo tunacheza ipo hivyo na inawezekana, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,”.

WAZIR JUNIOR KAWAKA HUKO

Wazir Junior
Wazir Junior mshambuliaji wa KMC ambaye hana rasta akishangilia moja ya bao na wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi. Source:KMC

Mshambuliaji wa KCM ambaye ni chaguo la kwanza kwenye timu hiyo ya wakusanya mapato Wazir Junior Wazir Junior ndani ya Machi kawaka akiwa ni miongoni mwa nyota waliofunga hat trick ndani ya Ligi Kuu Bara.

Ilikuwa ni Machi 10 wakati ubao wa Uwanja wa Azam Complex baada ya dakika 90 ukasoma KMC 4-2 Tabora United ambao walipoteza mchezo huo wa ligi uliokuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili.

Mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kucheza katika kikosi cha Yanga kinachodhaminiwa na SportPesa ambapo alijiunga na timu hiyo akitokea ndani ya kikosi cha Mbao ambayo ilishuka daraja.

Junior alitupia kambani mabao matatu na kusepa na mpira wake mazima mbele ya nyuki wa Tabora, Tabora United waliopoteza pointi tatu baada ya dakika 90 kwenye mchezo huo wakiwa ugenini.

Ni dakika ya 49, 60, 67 alikamilisha hat trick na kufikisha mabao 11 ndani ya ligi sawa na Aziz Ki wa Yanga ambaye alifunga bao lake la 11 kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Majaliwa.

Bao lingine kwenye mchezo huo wa ligi lilifungwa  na Daruesh Saliboko huku Mabao ya Tabora United yalifungwa na Daniel Lukandamila dakika ya 84, 90 kwa mkwaju wa penalti.

Share this: