salim-tryagain-------------------------------------------salim-tryagain-------------------------------------------

ZIMEBAKI saa chache tu, kabla ya kushuhudia mchezo mkali wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika kati ya wawakilishi wa Tanzania Simba na Jwaneng Gallaxy ambao unatarajiwa kupigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni mchezo wa mwisho kabisa kwenye kundi B la mashindano hayo ambao unatarajiwa kuamua nani anakata tiketi ya kwenda Robo Fainali ya mashindano hayo.

MSIMAMO WA KUNDI LA SIMBA

azamtvsports-------------------------------------------
Msimamo wa kundi la B

Mpaka sasa Mnyama ambaye amewahi kula shavu la udhamini wa SportPesa wanakamatia nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa wamekusanya pointi 6 katika michezo yao minne ya kwanza na wanahitaji angalau matokeo ya ushindi Jumamosi ili kufuzu Robo Fainali.

Kwenye msimamo wa kundi hilo vinara ni ASEC mimosas ya Ivory Coast ambao wamekusanya pointi 11 katika michezo minne ya kwanza na tayari wamejihakikishia kufuzu Robo Fainali ya mashindano hayo na kuongoza msimamo wa kundi.

Wydad Casablanca ya Morocco wao wanakamatia nafasi ya tatu na pointi zao 6, ambapo wao watamalizana na ASEC kwenye mchezo wa mwisho utakaopigwa Morocco.

Jwaneng Galaxy wao wanabuluza mkia na pointi zao 4 walizokusanya kwenye michezo minne.

SIMBA KISASI, JWANENG REKODI KWA MKAPA

Wanamsimbazi wameutangaza kuwa mchezo huu kwao ni wa kulipa kisasi kwa Jwaneng Galaxy kufuatia kumbukumbu mbaya ya kupoteza mabao 3-1 mara ya mwisho walipokutana kwenye Uwanja wa Mkapa na kushuhudia wenyeji wakitolewa kwenye mashindano hayo.

Katika mchezo huo straika wa Jwaneng Galaxy, Rudath Wendel aliitungua Wanasimba mabao mawili, hivyo Jwaneng wataingia na mpango mmoja tu, ambao ni kuhakikisha wanaendeleza rekodi yao ya kibabe kwa Mkapa.

AHMED AWAITA MASHABIKI KWA MKAPA

simbasctanzania------------------------------------------
Meneja wa habari wa Simba, Ahmed Ally 

Kuelekea mchezo wa Jumamosi, Meneja wa Habari na mawasiliano wa timu mwenyeji, Ahmed Ally amesema: “Ili timu ishinde inawahitaji Wanasimba wote, sio Mo, sio Try Again, sio Mangungu bali sisi wote kwa umoja wetu. Tutawafanya Jwaneng Galaxy kitu kibaya kama ilivyokuwa kwa Horoya.

“Wanasimba tukiunganisha nguvu Jwaneng hawezi kutoka salama Dar es Salaam. Robo fainali zote nne zilizopita nyie ndio mmeipeleka. Kama utakuja uwanjani sio tu kushangilia bali kuipeleka timu yetu yetu robo fainali. Mimi naamini Wanasimba tukiamua jambo letu hakuna wa kutuzia.

“Atakayegusa mechi yetu atasimulia vizazi vyao. Sisi tumeitwa Simba Sports Club hivyo tunatakiwa kuishi kwenye misingi ya mnyama husika. Kama hakuna mnyama anayemchezea Mfalme wa nyika basi na sisi hakuna timu inaweza kutuchezea. Mpira ni burudani lakini ni vita unapotafuta matokeo na unapoyatafuta hakuna kucheka na kima.

“Wote tunajua hali itakavyokuwa tusipomfunga Jwaneng, sasa kabla ya hilo tuchukue hatua ya kujiandaa na hiyo vita. Silaha zipo nyingi na silaha kubwa ni tiketi yako. Twendeni Wanasimba, twendeni kifua mbele, hatutawaangusha Jumamosi na Mnyama anakwenda robo fainali.

“Wydad kuruhusu magoli mawili kumfunga hapo shughuli yake iliishia pale, hata atume mwakilishi kwenye mechi ya Jwaneng hakuna kitakachobadilika. Hatuna presha ya kufunga magoli mengi, goli moja tu, linatosha.”

“Goli moja tu litatupeleka robo baada ya hapo tunatafuta magoli ya kufurahi, goli la pili, goli la tatu watu Wanasimbaaaaa ohooooo,” Ahmed Ally.

BODI YA SIMBA WANASEMAJE?

salim-tryagain-------------------------------------------
Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ akizungumzia mchezo huo amewataka wachezaji wake kucheza mchezo wa mwisho wa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama fainali ili kuhakikisha wanapata ushindi na kufuzu hatua ya Robo Fainali.

Simba inatarajiwa kuvaana dhidi ya Jwaneng Galaxy ya nchini Botswana katika mchezo wa mwisho wa kufuzu hatua Robo Fainali, ambao utapigwa kesho saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Katika mchezo huo, wenyeji wanahitaji ushindi wowote ili wafuzu hatua inayofuatia ya robo fainali

“Mechi yetu ya mwisho nyumbani Benjamin Mkapa dhidi ya Jwaneng Galaxy itakuwa zaidi ya fainali, Kila shabiki ajiandae kwa mchezo huo muhimu kwetu.” amesema Try again.

Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wadau mbalimbali wa soka hapa nchini unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia majira ya saa 1:00 usiku.

 

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.