Kampuni ya burudani na michezo ya ubashiri SportPesa, leo asubuhi imesaini mkataba wa kuendelea kuidhamini timu ya Namungo FC ya Lindi kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.
Waliohudhuria kutoka SportPesa ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Tarimba Abbas na Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Sabrina Msuya. Kutoka Namungo alikuwepo Omar Kaaya.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa udhamini, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi SportPesa Tarimba Abbas alianza kwa kusema anayofuraha kutangaza kuwa SportPesa imefikia makubaliano na timu ya Namungo FC ya kuendelea kuwa mdhamini mkuu kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.

“Ninayo furaha kuwajulisha kwamba SportPesa tutaendelea kuwa wadhamini wakuu wa timu ya Namungo kwa kipindi kingine cha msimu 2023/24.
Udhamini huu ni sehemu ya adhma yetu ambayo tumekuwa nayo katika kuunga mkono mpira wa Tanzania, ambapo tangu tumeanza rasmi shughuli zetu za kibiashara 2017, tumekuwa mstari wa mbele kuzishika mkono timu zetu kuliko kampuni yoyote ya ubashiri Tanzania’’.
Katika mkataba huu wa sasa tumeboresha zawadi ambazo Namungo FC atakuwa anapata pale atakapokuwa anafanya vizuri. Kwa ufupi udhamini huu unaenda kuboresha ufanisi wa timu ya Namungo katika maeneo mbali mbali katika timu yao. Mfano endapo watashika nafasi nzuri katika ligi na mashindano mengine kama FA na CAF.
Mkataba huu wenye gharama ya shilingi 1,055,000,000 TZS utaanza rasmi msimu wa ligi mwaka huu mpaka ifikapo mwaka 2024.
Akiongea kwa upande wa Namungo FC Afisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Omar Kaaya aliwashukuru SportPesa kwa kukubali kuendelea kudhamini timu hiyo na kuleta hali ya ushindani katika ligi.
‘’Mimi nikiwa kama mtendaji mkuu wa Namungo FC nipende kuwashukuru SportPesa kwa kutuamini na kuamua kuendelea kutudhamini, Lakini kipekee nikushukuru Tarimba na SportPesa kwa kupigania mafanikio ya soka la Tanzania kwa jitihada za udhamini mnazotupa’’.

Hiki walichofanya leo, cha kuendelea kutudhamini kwa Mwaka mmoja inaonyesha imani yao kwetu, na pia itakuwa chachu kwa benchi la ufundi na wachezaji katika kuhakikisha nembo ya mdhamini inapata zaidi ya kile wanachostaili.
Nadhani umeona ni jinsi gani tunaendelea kupanda katika nafasi ambapo mwaka huu tumemaliza ligi tukiwa nafasi ya tano. Hii inaonyesha ukomavu wa hali ya juu na kwa mkataba huu tutegemee mambo mazuri zaidi malengo yetu yakiwa ni kumaliza ligi tukiwa nafasi ya 3 au juu zaidi.
‘’Niwekeke wazi SportPesa imekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yetu na pia katika ukuaji endelevu wa tasnia ya soka inayotuzunguka.
Timu ya Namungo FC imemaliza msimu wa ligi ya NBC premier League 2022/2023 katika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi kuu Tanzania bara, ikiwa nyuma ya Singida Fountain Gate.
