Ihefu vs PolisiIhefu

Ligi Kuu Tanzania inaelekea ukingoni ambapo baadhi ya timu zimesalia na michezo minne na nyingine mitano na hadi sasa bado hakuna iliyothibitika kusalia au kushuka daraja kulingana na mahesabu ya alama.

Mkiani mwa msimamo timu za Mbeya City iliyopo katika nafasi ya 13 na KMC waliopo katika nafasi ya 14 zenyewe zinapambana ili zisicheze Play Off (mtoano) wakati Ruvu Shooting na Polisi zipo nafasi ya 15 na 16 na iwapo zitapoteza mechi zao zote zilizosalia watashuka daraja moja kwa moja,na kimahesabu wanahitaji kushinda kila mechi zao huku wakiwaombea mabaya walio juu yao.

Mbeya City ina alama 27 wakati KMC wana alama 26 lakini juu yao zipo Klabu za Coastal Union wenye alama 27, Dodoma Jiji wenye alama 28, Mtibwa wana alama 29.

Polisi Tanzania wanaoburuza mkia wana alama 19 hivyo iwapo wakishinda mechi zote watafikisha alama 31 wakati Ruvu Shooting wenye alama 20 iwapo watashinda mechi 4 zilizosalia watamaliza msimu wakiwa na alama 32.

Tafsiri nyepesi ni kwamba iwapo timu iliyo kwenye nafasi ya 8 ambayo ni Kagera Sugar yenye alama 32,na timu za chini yake ambazo ni Mtibwa Sugar yenye alama 29 iliyopo nafasi ya 9,Tanzania Prisons iliyipo nafasi ya 10 kwa alama zao 28,Coastal Union yenye alama 27 sawa na Mbeya City wakati KMC wenye alama 26 wanahitaji kufikisha alama kuanzia 33 ili kuhakikisha Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zinashuka daraja moja kwa moja.

Timu pekee ambazo zimeshajihakikishia kubaki Ligi Kuu Tanzania bara ni Yanga, Simba,Azam,Singida Big Stars,Geita Gold,Namungo na Ihefu ambazo tayari zina alama kuanzia 33 na kuendelea na hizi ndizo ambazo haziwezi kufikiwa na Polisi Tanzania na Ruvu Shooting.

Kwa takwimu hizo sasa,naweza kusema kwamba safari ya matumaini kwa Klabu hizi ina milima na mabonde na watahitaji kuwa bora zaidi kwenye mechi zilizosalia kuumaliza msimu.

Tukiwamulika Polisi Tanzania,safari yao ya matumaini itaanzia mikononi mwa Ihefu ambao katika mechi mbili zilizopita za mashindano yote wamejikuta wakichezea vichapo mfululizo kutoka kwa wekundu wa msimbazi Simba.

Ihefu ambao wameshajihakikishia kucheza Ligi Kuu msimu ujao,walipoteza kwa idadi kubwa ya mabao ambapo kwenye mchezo war obo fainali wa michuano ya Kombe la Shirikisho walinyukwa bao 5-1 kabla ya kuchapwa 2-0 kwenye dimba lao la nyumbani huko Mbarali watakuwa wanahitaji ushindi ili kuona uwezekano wa kuwaondoa Namungo,na Geita kwenye nafasi zao za 5 na 6Polisi TZ.

 

Polisi Tanzania inayonolewa na Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera wamepoteza dira muda mrefu kiasi kwamba iliwalazimu kulifuta benchi lake la ufundi lakini licha ya maamuzi hayo bado hawajaonyesha mabadiliko ya kiuchezaji tofauti na Ihefu ambao baada ya kusuwasuwa chini ya Zurei Katwila walimuajiri Juma Mwambusi ambaye alianza kubadili matokeo na hatimaye sasa wapo salama.

Mnamo April 21 saa 10 Jioni Polisi Tanzania watakuwa katika dimba lao la nyumbani katika dimba la Ushirikika mjini Moshi watakapokabiliana na  Ihefu kujaribu kuanza hesabu zao za vidole kabla msimu uliomalizika.

Katika mchezo wa kwanza Polisi Tanzania iliinyuka Ihefu bao 2-1 katika uwanja wao nyumbani na katika historia ya timu hizo tangu zikutane ,maafande hao hawajawahi kupoteza dhidi ya wakali hao kutoka Jiji la Mbeya.

 Katika mechi tano zilizopita,Polisi Tanzania imeshinda mara moja,sare moja na vipigo vitatu wakati Ihefu imeshinda mechi tatu,sare moja na kipigo mara moja.

Katika mechi 26 walizocheza Polisi Tanzania msimu huu,wameshinda mechi 4 pekee,sare 7 na wamepokea vipigo 15,wameruhusu mabao 38 huku wao wakifunga 19,wakati Ihefu wamecheza mechi 26,wameshinda 10,sare 3 huku wakipoteza mara 13,wameruhusu mabao 28 huku wao wakifunga mabao 25.

Ihefu kwasasa wanajivunia uwepo wa nyota kama Yacouba Sogne aliyejiunga nao akitokea Yanga na ndani ya muda mfupi alifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi,lakini pia Vicent Akpan na Nelson Okwa wote kwa mkopo kutokea Simba wamekuwa na mchango mkubwa katika kikosi hicho kinachonolewa na John Simkoko na Zuberi Katwila.

Share this: